17-Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu Na Sharh Yake: Maghfirah Kwa Wazazi Na Waumini

Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu

 

Na Sharh Yake

 

Alhidaaya.com

 

17-Maghfirah Kwa Wazazi Na Waumini

 

 

 

 

"رَبَّنَا اغْفِرْ لِي وَلِوَالِدَيَّ وَلِلْمُؤْمِنِينَ يَوْمَ يَقُومُ الْحِسَابُ"

 

“Rabb wetu! Nighufurie mimi na wazazi wangu wawili na Waumini Siku itakayosimama hesabu”.  [Ibraahiym: (41)]

 

Hii pia ni katika du’aa za Nabiy Ibraahiym (‘Alayhis Salaam).  Ndanimwe kuna maombi ya kupata uokozi katika nyumba ya aakhirah kwake yeye na kwa Waumini wote.  Inaonyesha huruma kubwa aliyopewa Nabiy huyu kwa Waumini wote; wa mwanzo wao hadi wa mwisho wao.

 

Ameanza akitawasali kwa Jina la Rabbu kwa kusema:  “Rabbi wetu!  Nighufurie mimi”.  Amejikhusisha mwenyewe kwa kujiombea maghfirah kuonyesha taksiri ambayo hakuna mwanadamu anayeweza kusalimika nayo.  Halafu akawaombea wazazi wake wawili maghfirah kutokana na haki yao kubwa kwake. Alimwombea baba yake maghfirah kutokana na ahadi aliyoahidiana naye.  Nayo ni pale alipomwambia:

 

"قَالَ سَلَامٌ عَلَيْكَ ۖ سَأَسْتَغْفِرُ لَكَ رَبِّي ۖ إِنَّهُ كَانَ بِي حَفِيًّا"

 

(Ibraahiym) akasema:  Salaamun ‘Alayka (Amani iwe juu yako).  Nitakuombea maghfirah kwa Rabb wangu.  Hakika Yeye daima Ni Mwenye Kunihurumia sana.  [Maryam: (47)]

 

Lakini baba yake huyo aliposhikilia ukafiri, alijivua naye kama Anavyosema Ta’aalaa:

 

"وَمَا كَانَ اسْتِغْفَارُ إِبْرَاهِيمَ لِأَبِيهِ إِلَّا عَن مَّوْعِدَةٍ وَعَدَهَا إِيَّاهُ فَلَمَّا تَبَيَّنَ لَهُ أَنَّهُ عَدُوٌّ لِّلَّـهِ تَبَرَّأَ مِنْهُ ۚ إِنَّ إِبْرَاهِيمَ لَأَوَّاهٌ حَلِيمٌ "

 

Na haikuwa Ibraahiym kumuombea maghfirah baba yake isipokuwa kwa sababu ya ahadi aliyoahidiana naye.  Lakini ilipombainikia kwamba yeye ni adui wa Allaah, alijiepusha naye.  Hakika Ibraahiym ni mwenye huruma mno na mvumilivu”.  [At-Tawbah: (114)]

 

Aayah hii inadulisha kwamba haijuzu kuwaombea washirikina maghfirah madhali bado wako kwenye ukafiri na ushirikina, ni sawa wakati wa uhai wao au baada ya kufa.  Lakini inajuzu kuwaombea hidaayah na tawfiyq ya kumwamini Allaah.

 

Halafu akawaombea na Waumini wote wa kiume na wa kike Allaah Awaghufirie madhambi yao siku hiyo ngumu ya kusimama mbele ya Allaah kuhisabiwa.  Kila mtu atateseka sana kwa makosa na madhambi yaliyosajiliwa kwenye daftari lake, kwa kuwa atakuwa hajui hatima yake itakuwaje.  Kwa kuling’amua hili, Nabiy Ibraahiym akatuombea sote tughufiriwe hapo.  Na hii ni bishara kubwa kwa kila Muumini, kwa kuwa Allaah Ta’aala Hairejeshi du’aa hii aliyoiomba Kipenzi Chake.

 

Na kwa ajili hiyo, Muislamu anatakikana akithirishe kuwaombea nduguze Waislamu  maghfirah wa tokea Aadam (‘Alayhis Salaam) hadi kusimama Qiyaamah.  Mbali na kuonyesha penzi lake kwa nduguzo hao, ataandikiwa jema kwa kila Muislamu.  Ni mabilioni mangapi ya mema ataandikiwa kwa idadi ya Waislamu tokea Aadam hadi Qiyaamah!  ‘Ubaadah bin Swaamit anasema: Nimemsikia Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:

 

"من استغفر للمؤمنين والمؤمنات كتب اللَّه له بكل مؤمن ومؤمنة حسنة"

 

“Atakayewaombea Waumini wanaume na Waumini wanawake maghfirah, Allaah Atamwandikia jema kwa kila Muumini mwanamume na kila Muumini mwanamke”.

 

Na kama tujuavyo, Allaah Huongeza jema moja hadi kumi mfano wake.  Basi hongera kwa atakayejumuishwa ndani ya du’aa hii.

 

 

Tunayojifunza katika du’aa hii:

 

 

1-  Umuhimu wa kuomba maghfirah.  Maghfirah ndiyo salama na mafanikio kwa Muislamu duniani na aakhirah.

 

 

2-  Mwombaji anatakiwa atenge sehemu ya du’aa yake kwa wazazi wake wawili. Yeye ni chumo lao, nao wana fadhila kubwa kwake.

 

 

3-  Thawabu kubwa zitokanazo na du’aa hii kutokana na:

 

 

(a)  Kuwa imetajwa ndani ya Kitabu cha Allaah kama Qur-aan itakayosomwa mpaka Siku ya Qiyaamah.

 

(b)  Malipo yake kuwa makubwa.  Kwani mwombaji huandikiwa jema moja kwa kila Muislamu mwanamume na Muislamu mwanamke.  Na kila jema moja Allaah Hulipa kumi mfano wake.  Ni mabilioni mangapi ya Waislamu waliotangulia, waliopo hivi sasa, na watakaokuja baadaye hadi Siku ya Qiyaamah!  Bila shaka si du’aa ya Muislamu kuisahau hata kidogo.

 

(c)  Ni du’aa ya Kipenzi cha Allaah (Khaliylur Rahmaan), na Allaah Hairejeshi du’aa ya Kipenzi Chake.

 

(d)  Ni du’aa yenye kujibiwa.  Kwa kuwa du’aa ya Muislamu kwa nduguye Muislamu kwa siri ni yenye kujibiwa.

 

 

4-  Mwombaji anatakiwa atenge sehemu ya du’aa zake kuwaombea nduguze Waislamu.  Na haya ndio mapenzi ya dhati na udugu wa kweli kati ya Waislamu.  Ni vizuri pia aanze kujiombea yeye mwenyewe kisha nduguze.

 

 

5-  Mwombaji aombe zaidi mambo ya aakhirah.

 

 

6-  Umuhimu wa du’aa za kisharia toka kwenye Qur-aan au kwa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam).  Ndani yake kuna makusudio adhimu na maana ambazo zinakusanya mahitajio yote anayoyatamani mtu kwa matamshi mafupi na maneno mazuri.

 

 

 

Share