27-Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu Na Sharh Yake: Wake Na Watoto Kuwa Kitulizo Cha Jicho

Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu

 

Na Sharh Yake

 

Alhidaaya.com

 

 

27-Wake Na Watoto Kuwa Kitulizo Cha Jicho

 

 

  "رَبَّنَا هَبْ لَنَا مِنْ أَزْوَاجِنَا وَذُرِّيَّاتِنَا قُرَّةَ أَعْيُنٍ وَاجْعَلْنَا لِلْمُتَّقِينَ إِمَامًا"

 

Rabb wetu!  Tutunukie katika wake zetu na dhuria wetu viburudisho vya macho yetu, na Tujaalie kuwa waongozi kwa wenye taqwa”.  [Al-Furqaan: (74)].

 

Hii ni du’aa ya pili katika du’aa za Waja wema wa Ar-Rahmaan.  Wanamwomba Allaah Awatunuku wake na watoto wema katika Matunukio Yake makubwa na mengi kwao.  Wanamwomba hawa wawe ni wenye kumtii Yeye na hivyo kuwa ni viburudisho vya macho yao hapa duniani na huko aakhirah.  Viburudisho vya macho ni kinaaya ya furaha na sururi.  Muislamu hufurahika sana anapoona watoto wake wako kwenye mstari wa taqwaa, wako mbali na marafiki wabaya, na wako mbali na tabia zote chafu za vijana.  Furaha hii ataipata duniani, na akifa watoto hawa wema watakuwa wanamwombea maghfirah, wanamtolea swadaqah, wanatekeleza wasiya wake, wanaendeleza mema yake na kadhalika, na Siku ya Qiyaamah watakutana na kujumuika pamoja Peponi.  Pia hufurahi sana kwa mke mwema ambaye anapomwangalia humfurahisha, akimwamrisha humtii na anapokuwa naye mbali humlindia heshima yake na mali yake.

 

Na du’aa hii ya kuwaombea wake zao na watoto wao ni du’aa kwa wao wenyewe pia, kwa kuwa manufaa yake yatawarudia wao wenyewe, na yanadumu duniani na aakhirah.  Ni kama alivyosema Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

 

"إِذَا مَاتَ الْإِنْسَانُ انْقَطَعَ عنه عَمَلُهُ إِلَّا مِنْ ثَلَاثَةٍ: صَدَقَةٍ جَارِيَةٍ، أَوْ عِلْمٍ يُنْتَفَعُ بِهِ، أَوْ وَلَدٍ صَالِحٍ يَدْعُو لَهُ"

 

“Anapokufa mwanadamu ‘amali zake hukatika ila kwa matatu: Swadaqah endelevu, au elimu inayopatiwa manufaa, au mtoto mwema anayemwombea”. [Swahiyh Muslim.  Hadiyth Swahiyh]

 

Na huko aakhirah kwa kuwa pamoja nao kwenye Pepo ya Kudumu.  Allaah Amesema:

 

"وَالَّذِينَ آمَنُوا وَاتَّبَعَتْهُمْ ذُرِّيَّتُهُم بِإِيمَانٍ أَلْحَقْنَا بِهِمْ ذُرِّيَّتَهُمْ وَمَا أَلَتْنَاهُم مِّنْ عَمَلِهِم مِّن شَيْءٍ ۚ كُلُّ امْرِئٍ بِمَا كَسَبَ رَهِينٌ"

 

Na wale walioamini na wakafuatwa na dhuriya wao kwa iymaan, Tutawakutanisha nao dhuriya wao na Hatutawapunguzia katika ‘amali zao kitu chochote.  Kila mtu atafungika kwa yale aliyoyachuma”.  [At-Tuwr: (21)].

 

Na kama hiyo haitoshi, manufaa haya yatarudi pia kwa Waislamu wote.  Kwa wema wa waliotajwa, utakuwa ni sababu ya wema kwa wale wote watakaotangamana nao.  Na hawa hawa pia ndio watawaombea du’aa njema Waislamu wote walio hai na waliokufa.

 

Hii ndio hisia ya maumbile asili ya kiiymaan.  Hisia ya kuongezeka idadi ya wapitao katika njia ya kuelekea kwa Allaah ‘Azza wa Jalla wake zao na watoto wao wakiwa katika ngazi ya kwanza.  Hao ndio watu wa karibu zaidi na mtu, nao ndio amana ya kwanza atakayoulizwa Siku ya Qiyaamah.

 

Mbali na kumwomba Allaah Awatunukie watoto na wake wa kuyatuliza macho yao, wamemwomba Allaah pia Awajaalie kuwa viongozi na maimamu wa kuigwa na watu wema katika vitendo vyao, maneno yao na kuisimamisha kwao dini.  Ni ombi kwa Allaah Awahidi, Awape tawfiyq, Awafadhili kwa elimu nufaishi na vitendo vyema vya dhahiri na fiche vitakavyowafikisha katika ngazi hii ya juu.  Kuigwa kwa mema athari yake chanya ni ndefu na pana duniani na aakhirah, na kuigwa kwa mabaya athari yake hasi ni ndefu na pana duniani na aakhirah.

 

Ombi lao hili pia vile vile ni la kuomba daraja za juu kabisa za utumwa.  Ni daraja za uongozi na uimamu katika dini.  Daraja hii ya juu haipatikani bila subira na yaqini ya kweli kama Alivyosema Allaah:

 

"وَجَعَلْنَا مِنْهُمْ أَئِمَّةً يَهْدُونَ بِأَمْرِنَا لَمَّا صَبَرُوا ۖ وَكَانُوا بِآيَاتِنَا يُوقِنُونَ"

 

Na Tukawajaalia miongoni mwao Maimamu wanaongoza kwa Amri Yetu waliposubiri, na walikuwa wakiziyakinisha Aayaat (na Ishara) Zetu”.  [As-Sajdah: (24)].

 

 

Faida za du’aa hii:

 

 

1-  Ni du’aa muhimu kama iliyotangulia nyuma kutokana na kusifiwa waombaji na Allaah. Pia kutoiacha kwao na kuikariri mara kwa mara kutokana na kitenzi cha wakati uliopo: (يقولون)

 

 

2-  Tunukio  la Allaah ni katika neema kubwa. Na kwa ajili hiyo wametawassali kwalo.

 

 

3-  Kumwomba Allaah ‘Azza wa Jalla kutengenea mke na watoto ni katika makusudio muhimu ambayo mwombaji anatakiwa asiyasahau.

 

 

4-  Mwombaji anatakiwa akuze utashi wake katika du’aa, na amwombe Allaah matakwa yake ya juu kabisa.  Ni kama alivyotuusia Rasuli kuwa tusiombe tu Pepo, bali tuombe Al-Firdaws ambayo ndio Pepo ya daraja la juu kabisa.  Au tusiombe tu watoto mradi watoto, bali tuombe watoto wema.

 

 

 

Share