34-Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu Na Sharh Yake: Kheri Yoyote Wakati Wa Dhiki Mbaya

 

Du’aa Toka Kwenye Qur-aan Tukufu

 

Na Sharh Yake

 

Alhidaaya.com

 

 

34- Kheri Yoyote Wakati Wa Dhiki Mbaya

 

 

"رَبِّ إِنِّي لِمَا أَنزَلْتَ إِلَيَّ مِنْ خَيْرٍ فَقِيرٌ"

 

“Rabb wangu! Hakika mimi ni mhitajia wa kheri yoyote Utakayoniteremshia”.  [Al-Qaswas: (24)]

 

Ni mlolongo wa du’aa za Nabiy Muwsaa (‘Alayhis Salaam) baada ya kuua mtu na kukimbilia Madyana.  Allaah Amezitaja kutokana na umuhimu wake. Ndanimwe kuna kheri na manufaa mengi ya kidunia na kiaakhirah.  Hivyo tuzizingatie na tuzifahamu.

 

 

Baada ya kuchoka sana kwa safari ya muda mrefu kwa miguu na kupata njaa kali huku akiwa hana chochote cha kula, Nabiy Muwsaa (‘Alayhis Salaam) alijua wapi aelekee na wapi pa kutokea.  Akaelekea kwa Mola wake Ambaye Alimwangalia na kumhifadhi tokea udogoni mpaka hapo alipofikia.  Hapo ndipo akaomba du’aa hii tukufu, kwa maneno laini kabisa yenye kuhisisha dhiki aliyonayo na msaada wa haraka wa faraja kwake.

 

 

Allaah kama Anavyopenda kwa mwombaji atawassal Kwake kwa Majina Yake, Sifa Zake na Neema Zake, pia Anapenda atawassali Kwake kwa udhaifu wake, ajizi yake, uhitajio wake, na kukosa uwezo wa kupata maslaha yake na kujiondoshea madhara.  Kwa hayo, mwombaji anaonyesha udhalili wake na uhitajio wake Kwake tu pasi na mwingine.

 

 

Ndani ya Kitabu cha Qur-aan, kuna aina tofauti za namna ya kuomba du’aa. Kuna du’aa ya ombi la moja kwa moja kama:

 

"وَقُلْ رَبِّ اغْفِرْ وَارْحَمْ وَأَنْتَ خَيْرُ الرَّاحِمِينَ"

 

Na sema:  Rabb wangu!  Ghufuria na Rehemu, Nawe Ni Mbora wa wenye kurehemu”.  [Al-Muuminuwn: (118)].

 

 

Na pia kuna ombi la muundo wa sentensi taarifu kama la Nabiy Ayyuwb:

 

"وَأَيُّوبَ إِذْ نَادَىٰ رَبَّهُ أَنِّي مَسَّنِيَ الضُّرُّ وَأَنتَ أَرْحَمُ الرَّاحِمِينَ"

 

“Na Ayyuwb, alipomwita Rabb wake:  Hakika mimi imenigusa dhara, Nawe Ndiye Mbora zaidi wa Kurehemu kuliko wengine wote wenye kurehemu”. [Al-Anbiyaa: (83)].

 

Au la Nabiy Zakariyyaa:

 

"قَالَ رَبِّ إِنِّي وَهَنَ الْعَظْمُ مِنِّي وَاشْتَعَلَ الرَّأْسُ شَيْبًا وَلَمْ أَكُن بِدُعَائِكَ رَبِّ شَقِيًّا"

 

Akasema: Rabb wangu!  Hakika mimi mifupa imeninyong’onyea na kichwa kimeng’aa mvi, na wala sikuwa mwenye kunyimwa katika kukuomba du’aa, ee Rabb wangu”.  [Maryam: (04)].

 

Na ikiwa Nabiy Muwsaa (‘Alayhis Salaam) alimwomba Allaah kheri kwa muundo wa kugusia hali mbaya aliyokuwa akiipitia, basi pia imethibiti kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwomba Allaah kwa muundo wa ombi la moja kwa moja.  Ni kama katika Hadiyth Adhimu ambapo Rasuli alimwambia Mama yetu ‘Aaishah (Radhwiya Allaah ‘anhaa):

“Shikamana na du’aa kusanyifu jumuishi. (Omba):

 

 "اللَّهمَّ إنِّي أسألُكَ مِنَ الخيرِ كلِّهِ عاجلِهِ وآجلِهِ ، ما عَلِمْتُ منهُ وما لم أعلَمْ ، وأعوذُ بِكَ منَ الشَّرِّ كلِّهِ عاجلِهِ وآجلِهِ ، ما عَلِمْتُ منهُ وما لم أعلَمْ ، اللَّهمَّ إنِّي أسألُكَ من خيرِ ما سألَكَ عبدُكَ ونبيُّكَ ، وأعوذُ بِكَ من شرِّ ما عاذَ بِهِ عبدُكَ ونبيُّكَ ، اللَّهمَّ إنِّي أسألُكَ الجنَّةَ وما قرَّبَ إليها من قَولٍ أو عملٍ ، وأعوذُ بِكَ منَ النَّارِ وما قرَّبَ إليها من قولٍ أو عملٍ ، وأسألُكَ أن تجعلَ كلَّ قَضاءٍ قضيتَهُ لي خيرًا"

 “Ee Allaah!  Hakika mimi ninakuomba kheri zote; za karibu yake na za mbali yake, ninazozijua kati yake na nisizozijua.  Na najilinda Kwako na shari zote; za karibu yake na za mbali yake, ninazozijua kati yake na nisizozijua.  Ee Allaah!  Hakika mimi ninakuomba kheri alizokuomba Mja Wako na Nabiy Wako, na najilinda Kwako na shari alizojilinda nazo Kwako Mja Wako na Nabiy Wako.  Ee Allaah!  Hakika mimi ninakuomba Jannah na yote ya kuniwezesha kuifikia katika maneno au vitendo.  Na najilinda Kwako na moto na yote ya kunisogeza kuukaribia katika maneno au matendo.  Na ninakuomba Uifanye kila qadhwaa Uliyoipitisha kwangu kuwa kheri”.  [Imesimuliwa na ‘Aaishah na kukharijiwa na Ibn Maajah.  Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh]

 

 

Tunapata faida zifuatazo kutokana na du’aa hii:

 

 

1-  Kumshtakia Allaah hali yako hakupingani na subra, bali hilo ni katika ukamilifu wa iymaan kwa Allaah Ta’aalaa na kuridhia Qadar Yake.  Tatizo ni kuwashtakia viumbe.  Hapo ndipo linapokuja kosa.

 

 

2-  Ni juu ya mwombaji atawassal kwa Allaah kwa aina tofauti za tawassulaat za kisheria.  Hilo ni katika ukamilifu wa utumwa Anaoupenda Allaah ‘Azza wa Jalla.

 

 

3-  Uhalali wa kujilinda na umasikini.  Huo ni mwenendo wa Manabii na Mitume.  Pia ilikuwa ni katika du’aa za Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuwa akiomba:

 

"اللّهُمَّ إنِّي أَعُوذُ بِكَ مِنَ الْفَقْرِ، وَالْقِلَّةِ، وَالذِّلَّةِ، وَأَعُوذُ بِكَ مِنْ أَنْ أَظْلِمَ أو أُظْلَمَ"

 

“Ee Allaah!  Hakika mimi najilinda Kwako kutokana na ufukara, uhaba (wa kila kinachohitajia ukamilifu) na udhalili.  Na najilinda Kwako kudhulumu au kudhulumiwa”.  [Imekharijiwa na Abu Daawuwd (1544), Ahmad (8294) na tamko ni lao, na Ibn Maajah (3842)]

 

 

 

Share