011-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Viapo Na Nadhiri: Mwenye Kusema: أَقْسَمْتُ “Nimeapa” au أُقْسِمُ “Ninaapa”

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الأَيْمَانِ وَالنُّذُوْرِ

Kitabu Cha Viapo Na Nadhiri

 

011- Mwenye Kusema: أَقْسَمْتُ “Nimeapa” au أُقْسِمُ “Ninaapa”

 

Alhidaaya.com

 

 

1-  Mwenye kusema:  “Ninaapa kwa Allaah” au “Nimeapa kwa Allaah”, basi hiki ni kiapo bila mvutano wowote, ni sawa mtu amenuwia yamini au hakunuwia.  Kwa kuwa akisema:  “Kwa Allaah” na hakusema:  “Naapa”, basi inakuwa ni kiapo kwa kukadiria kitenzi kabla yake (naapa).  Halafu matumizi ya kiada na kimazoea yamelazimisha hivyo.  Allaah ‘Azza wa Jalla Amesema:

 

"فَيُقْسِمَانِ بِاللَّـهِ"

 

“Kisha waape kwa Allaah”.  [Al-Maaidah (5:107)].

 

Na Amesema tena:

 

"وَأَقْسَمُوا بِاللَّـهِ جَهْدَ أَيْمَانِهِمْ"

 

“Na waliapa kwa Allaah kwa viapo vya nguvu”.  [Al-An’aam (6:109)].

 

2-  Akisema:  أُقْسِمُ  “Ninaapa” au  أَقْسَمْتُ “Nimeapa”, je kitakuwa ni kiapo?

 

Kuna kauli tatu kuhusu hili:

 

Kauli Ya Kwanza:  Ni Yamini Kwa Vyovyote

 

Ni madhehebu ya Hanafiy na Ahmad, na Ibn Qudaamah ameyatilia nguvu. Dalili zao ni:

 

1-  Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas toka kwa Abu Hurayrah -kuhusu kisa cha mtu aliyemhadithia Rasuli (Swalla Allaah ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) njozi yake na Abu Bakr akaifasiri.  Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:

 

"‏ أَصَبْتَ بَعْضًا وَأَخْطَأْتَ بَعْضًا ‏"‏ ‏.‏ فَقَالَ ‏:‏ أَقْسَمْتُ - بِأَبِي أَنْتَ وأمي-  لَتُحَدِّثَنِّي مَا الَّذِي أَخْطَأْتُ ‏.‏ فَقَالَ النَّبِيُّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ ‏:‏ ‏"‏ لاَ تُقْسِمْ ‏"‏

 

“Umepatia sehemu na umekosea sehemu”.  Akasema:  Nimekuapia -kwa baba yangu na mama yangu- utanieleza lipi nimekosea.  Rasuli akamwambia: “Usiape”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na At-Tirmidhiy (2293), Abu Daawuwd (3268), na Ibn Maajah (3918) kwa tamko hili.  Na katika Swahiyh Mbili kwa tamko la:  “Wa Allaah, hakika utanieleza”].

 

Hapa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amelihesabu neno la Abu Bakr “Nimeapa” kuwa yamini.  Likathibiti kwa hivyo kimatumizi na kwa ada ya kisharia.

 

2-  Katika mkasa wa Bi ‘Aaishah kuzushiwa tuhuma kwamba amezini, Abu Bakr (Radhwiya Allaah ‘anhu) alimwambia ‘Aaishah:

 

 "أَقْسَمْتُ عَلَيْكِ يَا بُنَيَّةُ إِلاَّ رَجَعْتِ إِلَى بَيْتِكِ"

 

“Nimekuapia na nakusihi ee mwanangu urudi nyumbani kwako”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (4757)].

 

3-  Katika kisa cha ‘Abdul Rahmaan bin Abiy Bakr pamoja na wageni wa Abu Bakr walipokataa kula chakula, Abu Bakr akaja, na ‘Abdul Rahmaan akajificha kwa kumwogopa, Abu Bakr akasema:

 

"يَا غُنْثَرُ أَقْسَمْتُ عَلَيْكَ إِنْ كُنْتَ تَسْمَعنِي"

 

“We mpumbavu wee, nimekuapia kama unanisikia [toka huko ulikojificha]”. [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Muslim (2057)].  

 

4-  Neno Lake Ta’aalaa:

 

"إِذْ أَقْسَمُوا لَيَصْرِمُنَّهَا مُصْبِحِينَ وَلَا يَسْتَثْنُونَ"

 

“Walipoapa kuwa bila shaka watayavuna (mazao yake) watakapopambaukiwa asubuhi •  Na wala hawakusema In-Shaa Allaah”.  [Al-Qalam (68: 18 na 19)].

 

Allaah Hakusema: “Wakaapa kwa Allaah”.  Hivyo Ameizingatia ni yamini, na kusema “In -Shaa Allaah” kunakuwa ndani ya yamini.

 

5 -  Ni kuwa yamini haijuzu ila kwa Allaah ‘Azza wa Jalla tu.  Hivyo, haifai kuapa isipokuwa kwa Allaah tu.  Ni kama Kauli Yake Ta’aalaa:

 

"وَاسْأَلِ الْقَرْيَةَ"

 

“Na uliza mji”.  [Yuwsuf (12:82)].

 

“Yaani watu wa mji”.  Na Waarabu wanakijua kiapo kwa njia hii (bila kumtaja Allaah).

 

Kauli Ya Pili:  Ni Yamini Kama Atanuwiya Kuapa Kwa Allaah, Kama Hakunuwiya Basi Si Kiapo.

 

Ni madhehebu ya Al-Hudhayl bin Zufar –Faqiyh mkubwa wa Kihanafiy, Is-Haaq, Maalik na Ibn Al-Mundhir.  Kwa kuwa inaweza kubeba kiapo kwa Allaah au kwa kitu kingine.  Hivyo haiwi yamini mpaka aielekeze kwenye hali ya kuwajibisha kafara.

 

Kauli Ya Tatu:  Si Yamini, Ni Sawa Akinuwiya Au Asinuwiye.

 

Ni kauli ya Ash-Shaafi’iy, Ibn Hazm, Al-Hasan, Az-Zuhriy, Qataadah, na Abu ‘Ubayd.  Kwa kuwa yamini haifungiki ila kwa Jina Tukuzwa au Sifa Tukuzwa ili Mwapiwa Ahudhurishwe, na hapa Hakutajwa.

 

Al-Khattwaabiy amelitolea dalili dhehebu hili kwa Hadiyth iliyotangulia nyuma kidogo ya tafsiri ya Abu Bakr ya njozi mbele ya Rasuli.  Na hii ni kwa kuwa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameamuru mtu kutekeleza kiapo chake ili kujisafisha nacho.  Na lau kama neno lake (Abu Bakr) “nimeapa” lingekua kiapo, basi angelimwamuru awajibike nacho.

 

Dalili hii imeandamiziwa kwa jibu lisemalo kwamba katika riwaayah ya Swahiyh mbili imeelezwa kwamba Abu Bakr aliitamka yamini wazi bayana akisema:  “Wa Allaah, utanieleza”.  Rasuli akamwambia:  “Usiape”.

 

Kauli Yenye Nguvu:

 

Kwa mujibu wa hoja hizo, inaonekana kuwa mwenye kusema “nimeapa” basi neno lake hilo linazingatiwa kama yamini iliyofungika.  Lakini, inatakikana yamini hii ifungwe kwa masharti mawili.  Kwanza mwapaji aape kwa khiyari yake mwenyewe, na pili akusudie kuapa, asiwe anatamka tu na mfano wa hivyo. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.

 

 

Share