012-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Viapo Na Nadhiri: Mwenye Kusema: أَشْهَدُ باللَّـهِ “Ninashuhudia kwa Allaah” au أَشْهَدُ “Ninashuhudia”

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الأَيْمَانِ وَالنُّذُوْرِ

 

Kitabu Cha Viapo Na Nadhiri

 

012-Mwenye Kusema: أَشْهَدُ باللَّـهِ “Ninashuhudia kwa Allaah”

au أَشْهَدُ “Ninashuhudia”

 

Alhidaaya.com

 

 

1-  Mwenye kusema:  “Ninashuhudia kwa Allaah”, basi tamshi lake hili ni kiapo kwa mujibu wa rai ya Fuqahaa wote.  Kwa kuwa neno: “Kwa Allaah” linatosha peke yake kuwa kiapo kwa kuwa linamaanisha:  “Ninaapa kwa Allaah”. Tumeshasema nyuma kwamba katika Neno Lake Ta’aalaa:

 

"أَن تَشْهَدَ أَرْبَعَ شَهَادَاتٍ بِاللَّـهِ"

 

“Atakapotoa ushahidi mara nne kwa kiapo cha Allaah”.  [An-Nuwr (24:8)]… ni kwamba “Li’aan” (mume kumtuhumu mkewe kuwa amezini kwa kutamka shahaadah) kwa mujibu wa ‘Ulamaa wengi ni viapo vinavyotiliwa nguvu kwa kumshuhudilia Allaah.  Lakini Ash-Shaafi’iy amekhitalifiana na wenzake kwa kuifungamanisha kauli yake hii na niya.

 

2-  Ama akisema:  “Ninashuhudia”, hapa ‘Ulamaa wamekhitalifiana kama kitakuwa ni kiapo katika kauli tatu kama zile zile za suala lililotangulia.  Mashiko ya mwenye kulizingatia neno “Ninashuhudia” kuwa kiapo, ni Neno Lake Ta’aalaa:

 

"إِذَا جَاءَكَ الْمُنَافِقُونَ قَالُوا نَشْهَدُ إِنَّكَ لَرَسُولُ اللَّـهِ"

 

“Watakapokujia (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) wanafiki wakisema: Tunashuhudia kwamba wewe bila shaka ni Rasuli wa Allaah”.

 

Kisha Akasema baada ya kauli hii:

 

"اتَّخَذُوا أَيْمَانَهُمْ جُنَّةً فَصَدُّوا عَن سَبِيلِ اللَّـهِ"

 

“Wamefanya viapo vyao kuwa ni ngao, hivyo wakazuia Njia ya Allaah”.  [Al-Munaafiquwn (63: 1 na 2)].  Wamesema: Allaah Ameuita ushuhuda wao kiapo.

 

‘Ulamaa wengine wamejibu hoja hii wakisema kuwa Aayaat haziko bayana kutolewa dalili juu ya hili kwa kuwepo uwezekano wa kuwa Kauli Yake Ta’aalaa:

 

اتَّخَذُوا أَيْمَانَهُمْ “Wamevifanya viapo vyao” hairejei ikafungamana na Kauli Yake:

 

نَشْهَدُ إِنَّكَ لَرَسُولُ اللَّـهِ Tunashuhudia kwamba wewe bila shaka ni Rasuli wa Allaah, bali inarejea kwenye sababu ya kuteremshwa Aayaat, nayo ni kuwa ‘Abdullaah bin Ubayya aliapa aliyoyasema.  Yamesemwa haya na Al-Qurtubiy.

 

Ninasema:  “Kauli hii ya ‘Ulamaa hawa pengine inatiliwa nguvu na Hadiyth ya Ibn Mas-‘uwd aliyeripoti kwamba:  “Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliulizwa:  Ni watu wapi walio bora zaidi?  Akasema:

 

" قَرْنِي ثُمَّ الَّذِينَ يَلُونَهُمْ ثُمَّ الَّذِي يَلُونَهُمْ ثُمَّ يَجِيءُ قَوْمٌ تَسبِقُ شَهَادَة أحدِهمْ يَمِينه وَيَمِينه شَهَادَته"

 

“Ni kizazi changu [cha Maswahaba], kisha wale wanaowafuatia [cha Taabi’iyna], kisha kizazi kinachowafuatia [cha baada ya Taabi’iyna].  Halafu watakuja watu ambao ushahidi wa mmoja wao utatangulia kiapo chake, na kiapo chake ushahidi wake”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (6658) na Muslim (2533)].

 

Al-Haafidh kasema:  “Mpishano wa maana uko wazi kati ya yamini na ushahidi”.  [Fat-hul Baariy (11/544)].

 

 

 

 

Share