018-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Viapo Na Nadhiri: Kuapa Kwa Mila Isiyo Ya Uislamu

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الأَيْمَانِ وَالنُّذُوْرِ

 

Kitabu Cha Viapo Na Nadhiri

 

 

018- Kuapa Kwa Mila Isiyo Ya Uislamu

 

 

Alhidaaya.com

 

 

 

 

 

Rasuli amesema :

 "‏مَنْ حَلَفَ بِمِلَّةٍ سِوَى الإِسْلاَمِ كَاذِبًا مُتَعَمِّدًا فَهُوَ كَمَا قَالَ، وَمَنْ قَتَلَ نَفْسَهُ بِشَىْءٍ عَذَّبَهُ اللَّهُ بِهِ فِي نَارِ جَهَنَّمَ ‏"‏‏ ‏

 

“Mwenye kuapa kujinasibisha na dini nyingine isiyo Uislamu kwa uongo wa kusudi, basi anakuwa kama alivyojinasibishia.  Na yeyote mwenye kujiua kwa kitu chochote, Allaah Atamwadhibu nacho ndani ya Moto wa Jahannam”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (1363) na Muslim (110)].

 

Na Hadiyth ya Buraydah, amesema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

"‏مَنْ حَلَفَ فَقَالَ‏:‏ إِنِّي َبَرِيْءٌ مِنَ الإِسْلامِ، فَإِنْ كَانَ كَاذِبًا، فَهُوَ كَمَا قَالَ، وَإِنْ كَانِ صَادِقًا، فَلَنْ يَرْجِعَ إِلَى الإِسْلامِ سَالِمًا‏"‏‏

 

“Mwenye kuapa akasema:  Mimi nitaachana na Uislamu,  ikiwa amesema uongo, basi anakuwa kama alivyosema.  Na kama amesema kweli, basi hatorudi akiwa salama katika Uislamu”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Abu Daawuwd (3258), An-Nasaaiy (3772), Ibn Maajah (2100) na Ahmad (5/356)].

 

Kisha ‘Ulamaa wamekhitalifiana kuhusu kama kiapo hiki ni cha kishariah au la.

 

Maalik, Ash-Shaafi’iy, Ahmad katika moja ya riwaya mbili, Al-Layth, Abu Thawr na Ibn Al-Mundhir wamesema si kiapo, na dalili yao ni kuwa hakikuapiwa kwa Jina la Allaah wala kwa Sifa Yake.  Hivyo hakiwi kiapo na hakuna kafara ndani yake.

 

Lakini Mahanafi, Ahmad katika -riwaayah nyingine-, Al-Hasan, Ath-Thawriy, Al-Awzaa’iy na Is-Haaq, ikiwa pia ni chaguo la Sheikh wa Uislamu wamesema ni kiapo, kwa kuwa amefungamanisha kutokufanya kitendo na ukafiri wake ambao ni kujiweka mbali na Allaah.  Hivyo anakuwa ameunganisha kitendo na iymaan yake kwa Allaah.  Na huu hasa ndio uhakika wa kuapa kwa Allaah.  Hivyo, kuunganisha kitendo na Ahkaam za Allaah kati ya kuwajibisha au kuharamisha ni hali hafifu zaidi kuliko kukiunganisha na Allaah moja kwa moja.  Na kwa muktadha huu, akivunja kiapo, ni lazima kafara.

 

·        Hukmu Kwa Mwapaji Mwenyewe

 

Kama atakuwa ni mwongo (yaani hakusudii kikweli ukafiri), na kwa kiapo chake hicho alikuwa anakusudia kujiepusha mwenyewe na kitu au kujihimizia kwacho, basi anakuwa hakukufuru.  Lakini pamoja na hivyo, atakuwa ameingia ndani ya wigo wa makamio makali.  Na kama alikusudia kwa neno hilo kuridhia ukafiri kama atalifanya jambo, basi hapo hapo anakuwa kafiri.

 

Ama akiwa ni mkweli (anakusudia kweli ukafiri), basi hawi salama, kwa kuwa ndani yake kuna aina ya dharau kwa Uislamu, na atapata madhambi kwa kiapo hicho hicho.  Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi.

                                               

 

Share