019-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Viapo Na Nadhiri: Aina Za Yamini Za Viapo: Yamini Ya Upuuzi

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الأَيْمَانِ وَالنُّذُوْرِ

 

Kitabu Cha Viapo Na Nadhiri

 

019- Aina Za Yamini Za Viapo: Yamini Ya Upuuzi

 

Alhidaaya.com

 

 

 

 

Tumesema nyuma kwamba yamini za Waislamu zinakuwa ima za kiapo au za shurutisho (sharti na matokeo yake, yaani; likifanyika hili, litafanyika lile).  Ama yamini za viapo, hizi ziko za aina tatu kwa upande wa kufungika kwake na kwa upande wa wajibu wa kutoa kafara mtu akivivunja.  Na zifuatazo ndizo aina hizi tatu pamoja na vidokezo vya ahkaam husika kwa kila aina:

 

Aina Ya Kwanza:  Yamini Ya Upuuzi

 

·        Taarifu Yake:

 

Allaah Ta’aalaa Amesema:

 

 لَّا يُؤَاخِذُكُمُ اللَّـهُ بِاللَّغْوِ فِي أَيْمَانِكُمْ وَلَـٰكِن يُؤَاخِذُكُم بِمَا كَسَبَتْ قُلُوبُكُمْ ۗ وَاللَّـهُ غَفُورٌ حَلِيمٌ ﴿٢٢٥﴾

 

225.  Allaah Hatokushikeni kwa viapo vyenu vya upuuzi, lakini Atakuchukulieni kwa yaliyochuma nyoyo zenu.  Na Allaah Ni Mwingi wa Kughufuria, Mpole, Mvumilivu.  [Al-Baqarah].

 

‘Ulamaa wamekhitalifiana kwa kauli kadhaa katika kufasiri maana ya “Yamini ya upuuzi”.  Kauli mashuhuri zaidi ni mbili ambapo kila mojawapo inabeba maana ya neno upuuzi.

 

Kauli Ya Kwanza:  Upuuzi ni neno linaloteleza ulimini bila kukusudia yamini kama kusema:  “Laa, wa Allaah  لا وَاللهِ” au “Balaa, wa Allaah بَلَى وَاللهِ ” ambapo mtu husema katika hali ya kuunga maneno yake, au katika hali ya ghadhabu, ni sawa likiwa hilo kwa wakati uliopita, au uliopo, au ujao.

 

Hii ni kauli ya Ash-Shaafi’iy na Hanbali ambao kigezo chao ni kauli ya ‘Aaishah (Radhwiya Allaah ‘anhaa) alipoizungumzia Kauli Yake Ta’aalaa:

 

لَّا يُؤَاخِذُكُمُ اللَّـهُ بِاللَّغْوِ فِي أَيْمَانِكُمْ

 

Allaah Hatokushikeni kwa viapo vyenu vya upuuzi….ambapo alisema:

 

" أُنزِلَ فِي قَوْلِه : لا وَاللهِ، وَبَلى وَاللهِ"

 

“Imeteremshwa kuhusu neno la mtu kusema: Laa, wa Allaah na balaa wa Allaah”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (6663) na ‘Abdur Razzaaq (15952)].

 

Amesema pia ‘Aaishah:

 

"أيمانُ اللَّغْوِ ما كَانَ فِي الْهَزْلِ و المِراءِ وَالْخُصُوْمَةِ، وَالْحَدِيْثُ  الَّذِيْ لا يُعقَدُ عَلَيْه القَلْبُ"

 

“Yamini za upuuzi ni zile zinazokuwa katika mzaha, mabishano na ugomvi, na maneno ambayo hayajakusudiwa na moyo.”  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na At-Twabariy (2/245) na Al-Bayhaqiy (10/49)].

 

Na kwa vile pia Allaah Taa’alaa Ameikabilisha yamini ya upuuzi katika Aayah Tukufu na yamini iliyochumwa na moyo (kuonyesha tofauti kati yao). Iliyochumwa na moyo ni ile iliyokusudiwa, hivyo isiyokusudiwa inaingia katika kigawanyo cha yamini za upuuzi bila kupambanua kati ya wakati wake uliopita, au wakati wake uliopo, au wakati wake ujao ili ulinganishi ufanikike.

 

Kauli Ya Pili:  Upuuzi ni mtu kuapa juu ya kitu anachokiitakidi kwa njia ya uhakika kamili au dhana isiyo na shaka kuwa ndicho, kisha inabainika ndivyo sivyo.  (Ni kama kuapa kuwa ndege yule ni kware, kumbe ni njiwa).

 

Ni kauli ya Hanafiy na Maalik.  Kigezo chao ni yaliyothibiti toka kwa Zaraarah bin Awfaa (Radhwiya Allaah ‘anhu) aliyesema:

 

"هُوَ الرَّجُلُ يَحْلِفُ عَلى الْيَمِيْنِ لا يَرَى إِلَّا أَنَّهَا كَمَا حَلَفَ"

 

“Ni mtu anaapa yamini haoni isipokuwa kwamba yamini iko kama alivyoapa”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na At-Twabariy (2/245)].

 

Ninasema:  “Kauli mbili zimekaribiana, na upuuzi umo ndani ya zote mbili.  Kwa kuwa, katika tafsiri ya kwanza, hakukusudia kabisa kufunga yamini.  Na katika ya pili, hakudhamiria kuvunja kiapo na wala hakukusudia isipokuwa kweli ambayo ana uhakika nayo.  Allaah Ndiye Mjuzi wa yote”.  [Al-Muhallaa (8/34), Al-Mughniy (11/181) na Adhwaaul Bayaan (2/108)].

 

·        Hukmu Ya Kiapo Cha Upuuzi

 

Allaah Ta’aalaa Amesema:

 

"لَّا يُؤَاخِذُكُمُ اللَّـهُ بِاللَّغْوِ فِي أَيْمَانِكُمْ"

 

“Allaah Hatokushikeni kwa viapo vyenu vya upuuzi”.  [Al-Baqarah (2:225)].

 

Aayah inadulisha kuwa Allaah Hatomwadhibu mtu kwa kiapo cha upuuzi.  Hii inahusu dhambi na kafara, kwa maana, hakuna dhambi, hakuna kafara.

 

  

Share