021-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Viapo Na Nadhiri:Aina Za Yamini Za Viapo: Yamini Aliyojifunga Nayo Mtu

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

 

كِتَابُ الأَيْمَانِ وَالنُّذُوْرِ

 

Kitabu Cha Viapo Na Nadhiri

 

 

021- Aina Za Yamini Za Viapo: Yamini Aliyojifunga Nayo Mtu

 

Alhidaaya.com

 

 

 

 

·        Taarifu Yake:

 

Ni yamini kwa jambo la kulifanya mbeleni ambalo kiakili linawezekana, ni sawa ikiwa ni kwa kutolifanya au kulifanya.  Ni kama kusema:  “Wa Allaah, sitofanya kadhaa”.  Au:  “Wa Allaah, lazima nitafanya kadhaa”.

 

Mwapaji anakuwa ameazimia kwa moyo wake kufanya au kutofanya kisha ulimi wake unaeleza hayo kwa yamini.

 

Taarifu nyingine inasema kuwa ni kiapo kisicho cha ghamuws au jambo la kipuuzi.

 

·        Masharti Yake:

 

Ili kiapo hiki kiwe ni cha mtu kujifunga nacho, ni lazima yawepo masharti ambayo baadhi yake yanamhusu mwapaji, mengine yanalihusu jambo linaloapiwa, na mengine yanalihusu tamshi.  Haya matatu ndiyo nguzo ya yamini hii.

 

(a)   Masharti Ya Mwapaji

 

Ili kiapo cha mwapaji kifungike, ni lazima awe na masharti yafuatayo:

 

1-  Awe amebaleghe.  2-  Awe na akili timamu.  3-  Awe Muislamu (kwa Mahanafiy na Wamaalik).

 

Yamini ya kuapa kwa Allaah Ta’aalaa haifungiki kwa kafiri hata akiwa ni “dhimmiy” (kafiri aishiye chini ya himaya ya Dola ya Kiislamu).  Lakini Mashaafi’iy na Mahanbali wamesema kuwa Uislamu sio sharti ya kufungika kiapo au kubakia kwake.  Wanasema lau “dhimmiy” ataapa kwa Allaah kisha akavunja kiapo chake –naye ni kafiri- basi lazima atoe kafara.  Na kama atashindwa kutoa kafara kwa kulisha, basi hatofanya kafara kwa kufunga mpaka atakaposilimu.

 

4-  Kiapo kitamkwe kwa ulimi.

 

Haitoshi kiapo cha ndani ya nafsi.  Hili ni kwa mujibu wa Jumhuwr kinyume na baadhi ya Wamaalik.

 

5-  Kukusudia.

 

Kwa kuwa mtu haadhibiwi isipokuwa kwa kulikusudia jambo na kulipania.  Na kwa ajili hiyo, Allaah Ta’aalaa Ameipomosha kafara ya kiapo cha upuuzi.

 

6-  Kuwa na hiari.

 

Kama atakosea au akalazimishwa, basi kiapo hakifungiki, na hatoadhibiwa.  Hii ni kauli yenye nguvu ya Jumhuwr kinyume na Mahanafiy.  Ni kwa neno lake Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam):

 

"إنَّ اللَّهَ تَجَاوَزَ لِي عَنْ أُمَّتِي الْخَطَأَ وَالنِّسْيَانَ وَمَا اسْتُكْرِهُوا عَلَيْهِ" .

 

“Hakika Allaah Ameusamehe Umati wangu kwa ajili yangu wakikosea, wakisahau na kwa yale waliyolazimishiwa”.  [Hadiyth Hasan].

 

(b)   Masharti Ya Jambo Linaloapiwa

 

1-  Liwe ni jambo la wakati ujao, kwa kuwa yamini juu ya jambo lililokwishapita haina kafara kwa mujibu wa kauli yenye nguvu –kama ilivyotangulia-, na kwa neno lake Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam):

 

"فيُكَفِّرْ ، وَلِيَأْتِ الَّذِيْ هُوَ خَيرٌ "

 

“Basi atoe kafara, na afanye lile lililo la kheri zaidi”.  [Hadiyth Swahiyh.  Itakuja kwa ukamilifu pamoja na takhriyj yake].

 

2-  Liwe na picha ya uhalisia wa kuwepo wakati wa kuapa (lisiwe jambo lisilowezekanika).

 

(c) Masharti Ya Tamko La Kiapo

 

1-  Kiapo kisiwe kwa kiumbe.  Dalili za sharti hili zimeshatajwa mwanzoni mwa mlango huu.

 

2-  Asiachanishe kati ya mwenye kuapiwa (Allaah) na lenye kuapiwa (jambo) kwa mnyamao na mfano wake.

 

3-  Kiapo kisiwe na tamshi la:  “In Shaa Allaah”, yaani kufungamanisha na Matakwa ya Allaah na mfano wa hilo kwa namna isiyoleta picha ya kuweza kukivunja.  Hili litabainishwa mbeleni In Shaa Allaah.

 

·        Hukmu Ya Kutekeleza Na Kukivunja Kiapo Hiki

 

Yamini yenye kufungika inakuwa ima:

 

(a)  Kwa kuapa kufanya jambo la waajib, au kuacha maasia.  Ni kama kusema: “Wa Allaah, nitaswali Adhuhuri”, au “Wa Allaah, sitoiba usiku”.  Kiapo hiki ni lazima kukitekeleza, na kukivunja ni haramu bila makhitalifiano.

 

(b)  Au kuapa kufanya maasia au kuacha la waajib.  Kiapo hiki ni haramu kukitekeleza, na ni waajib kukivunja.

 

Mfano wa hili ni mtu kuapa yamini kuhusu mkewe na wanawe ambapo kama hatoivunja basi watapata madhara, na kuivunja kunakuwa sio ma’aswiyah.  Hapo anatakiwa avunje kiapo chake, afanye hilo jambo, na atoe kafara ya kiapo chake.  Imesimuliwa na Abu Hurayrah kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) amesema:

 

"‏ وَاللَّهِ لأَنْ يَلِجَّ أَحَدُكُمْ بِيَمِينِهِ فِي أَهْلِهِ آثَمُ لَهُ عِنْدَ اللَّهِ مِنْ أَنْ يُعْطِيَ كَفَّارَتَهُ الَّتِي افْتَرَضَ اللَّهُ عَلَيْهِ ‏"

 

“Naapa kwa Allaah, hakika mmoja wenu kushikilia atekeleze kiapo chake kwa watu wake (ambapo watadhurika) ni madhambi makubwa zaidi kwake mbele ya Allaah kuliko kutoa kafara yake ambayo Allaah Amemfaradhishia”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al Bukhaariy (6624) na Muslim (1655)].

 

(c)  Au kuapa kufanya jambo lililosuniwa au kuacha jambo ambalo ni makruhu.  Ni kama kusema:  “Wa Allaah, nitaswali Sunnah ya As Subh”, au “Sitogeuka ndani ya Swalaah yangu”.  Hapa kutekeleza kiapo inakuwa ni jambo linalopendeza na kukivunja ni makruhu.  Na baadhi ya ‘Ulamaa wamesema:  Bali ni waajib kukitekeleza na haijuzu kukivunja kutokana na Neno Lake Ta’aalaa:

 

"وَاحْفَظُوا أَيْمَانَكُمْ"

 

Na hifadhini yamini zenu.”  [Al-Maaidah: 89].

 

(d)  Au kuapa kufanya jambo la makruhu au kuacha jambo la Sunnah.  Hapa itapendeza kuvunja kiapo na kutoa kafara, na itakuwa makruhu kukitekeleza.  Ni kutokana na neno lake Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam):

 

"‏ مَنْ حَلَفَ عَلَى يَمِينٍ فَرَأَى غَيْرَهَا خَيْرًا مِنْهَا فَلْيُكَفِّرْ عَنْ يَمِينِهِ وَلْيَفْعَلْ ‏"

 

“Mwenye kuapa kiapo, kisha akaona jingine ni bora zaidi kuliko aliloliapia, basi atoe kafara kwa kiapo chake, na alifanye (hilo lililo bora zaidi).  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al Bukhaariy (1650) na At Tirmidhiy (1530)]. 

 

Na Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alimwambia ‘Abdul Rahmaan bin Samurah:

 

"وإذا حَلَفْتَ علَى يَمِينٍ، فَرَأَيْتَ غَيْرَها خَيْرًا مِنْها، فَكَفِّرْ عن يَمِينِكَ، وأْتِ الَّذِيْ هُوَ خَيْرٌ"

 

“Na kama ukila kiapo, na ukaona jingine ni bora zaidi kuliko uliloliapia, basi toa kafara kwa kiapo chako, kisha fanya hilo ambalo ni bora zaidi”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (6622) na Muslim (1652)].

 

Na kuhusiana na suala hili hili, Abu Bakr (Radhwiya Allaah ‘Anhu) aliapa kwamba hatompa tena pesa ya masurufu Mistwah ambaye alimzushia kwa dhulma binti yake ‘Aaishah uzushi wa kuwa amezini.  Na hapo ikashuka Kauli Yake Ta’aalaa:

 

"وَلَا يَأْتَلِ أُولُو الْفَضْلِ مِنكُمْ وَالسَّعَةِ أَن يُؤْتُوا أُولِي الْقُرْبَىٰ"

 

Na wala wasiape wale wenye fadhila miongoni mwenu na wenye wasaa wa mali kuwa hawatowapa (swadaqah) jamaa wa karibu”.  [An-Nuwr: 22]  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al Bukhaariy (4750) na Muslim (2770) kutoka Hadiyth ndefu ya ‘Aaishah ikizungumzia kisa cha kuzushiwa yeye zinaa].

 

(e)  Au kuapa kufanya jambo la mubaah.  Hapa kutekeleza kiapo inakuwa ni bora zaidi madhali hakuna ndani yake madhara, na hakuna kheri katika kukivunja kwa mujibu wa Hadiyth zilizotangulia.

 

 

 

 

Share