020-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Viapo Na Nadhiri:Aina Za Yamini Za Viapo: Yamini Ya “Ghamuws” (Ya Uongo Ili Kudhulumu Haki Ya Mtu)

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

 

كِتَابُ الأَيْمَانِ وَالنُّذُوْرِ

 

Kitabu Cha Viapo Na Nadhiri

 

 

020- Aina Za Yamini Za Viapo: Yamini Ya “Ghamuws”  

(Ya Uongo Ili Kudhulumu Haki Ya Mtu)

 

Alhidaaya.com

 

 

 

 

 

1-     Taarifu Yake:

 

Ni mtu kuapa juu ya jambo lililokwishapita akikusudia uongo ili amege kwa kiapo hiki haki ya mtu mwingine.  Kinaitwa pia “Yamiyn Az-Zuwr” na “Yamiyn Al-Faajirah”.  Na katika Hadiyth kimeitwa kiapo cha “Swabr” (yaani, ambacho mtu anajifunga mwenyewe ndani yake ili ahakikishe anapata lengo lake kwa kiapo hicho).

 

Amesema katika An-Nihaayah:  Imeitwa “ghamuws”, kwa kuwa itamtosa mwapaji wake ndani ya moto.

 

·        Hukmu Yake:

 

Ni dhambi kati ya madhambi makubwa, na mwapaji wake anapata dhambi kwa itifaki ya Waislamu wote.

 

(a)  Toka kwa ‘Abdullaah bin ‘Amri kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"الكَبَائِرُ : الإشْرَاكُ بِاللهِ ، وَعُقُوْقُ الوَالِدَيْنِ ، وَقَتْلُ النَّفْسِ ، وَاليَمِيْنُ الغَمُوْسُ"

 

“Madhambi makubwa:  Ni kumshirikisha Allaah, kutowatii na kuwaasi wazazi wawili, kuua nafsi, na yamini ya uongo wa kukusudia”.  [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (6675), An-Nasaaiy katika Al-Kubraa (6/322) na At-Tirmidhiy (3021)].

 

(b)  Toka kwa Abu Umaamah, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"‏مَنِ اقْتَطَعَ حَقَّ امْرِئٍ مُسْلِمٍ بِيَمِيْنِهِ فَقَدْ أَوْجَبَ اللهُ لَهُ النَّارَ، وَحَرَّمَ عَلَيْهِ الْجَنَّةَ” فَقَالَ رَجُلٌ‏:‏ وَإِنْ كَانَ شَيْئًا يَسِيْرًا يَا رَسُوْلَ اللهِ ‏؟‏ فَقَالَ‏:‏ “وَإِنْ قَضِيبًا مِنْ أَرَاكٍ" 

 

 “Yeyote mwenye kumega haki ya mtu Muislamu kwa kutumia kiapo chake, basi hakika Allaah Amemwajibishia moto, na Amemharamishia Pepo.  Mtu mmoja akasema:  Hata japo kitu kidogo ee Rasuli wa Allaah?  Akasema:  Hata japo kijiti cha mti wa mswaki”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Muslim (137) na Ibn Maajah (2324)].

 

(c)  Ibn Mas-‘uwd (Radhwiya Allaah ‘anhu) amesema, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"مَنْ حَلَفَ عَلَى يَمِينِ صَبْرٍ وَهُوَ يَقْتَطِعُ بِهَا مَالَ امْرِئٍ مُسْلِمٍ لَقِيَ اللَّهَ وَهُوَ عَلَيْهِ غَضْبَانُ"

 

 “Mwenye kuapa yamini ya “swabr” (ya uongo) ili amege kwayo mali ya mtu Muislamu, basi atakutana na Allaah Akiwa na hasira naye”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (6676) na Muslim (38)].

 

(d)  Abu Dharri amepokea toka kwa Nabiy (Swallah Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:

 

"ثَلَاثَةٌ لَا يُكَلِّمُهُمُ اللَّهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ، وَلَا يَنْظُرُ إِلَيْهِمْ، وَلَا يُزَكِّيهِمْ، وَلَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ –ثَلاثًا- قَالَ أَبُوْ ذَرٍّ: خَابُوا وَخَسِرُوا مَنْ هُمْ يَا رَسُولَ اللَّهِ؟ قَالَ: «الْمُسْبِلُ وَالْمَنَّانٌ وَالْمُنَفِّقُ سِلْعَتَهُ بِالْحَلِفِ الْكَاذِبِ"

 

“Watu watatu, Allaah Hatowasemesha Siku ya Qiyaamah, wala Hatowaangalia wala Hatowatakasa, na watakuwa na adhabu iumizayo –akasema mara tatu- Abu Dharri akasema:  Wamepita utupu na wamekula hasara, ni nani hao ee Rasuli wa Allaah?  Akasema:  Mwenye kuteremsha nguo yake chini ya vifundo vya miguu, msimbuliaji na mchuuzi wa bidhaa zake kwa kiapo cha uongo”. [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Muslim (106), Abu Daawuwd (4087), An-Nasaaiy (2563), At-Tirmidhiy (1121) na Ibn Maajah (2208)].

 

·        Je, Kiapo Cha Ghamuws Kinaruhusiwa Kwa Dharura?

 

Hapana shaka yoyote kwamba kiasli, kiapo cha uongo ni haramu.  Lakini kinaweza kukabiliwa na mazingira halali ya kukitoa nje ya duara la uharamu na kukihalalisha.  Ni kama Muislamu aliyejificha kumkimbia dhalimu, kisha mtu akaulizwa kama amemwona.  Hapo ni lazima aongope ili kumficha, na hata akitakwa aape, basi ni lazima aape na atumie “tawriyah” (neno lenye kubeba maana mbili; ya juu dhahiri na ya ndani fiche) katika kiapo chake.  Kama ataapa na hakutumia neno hilo, hapa pana makhitalifiano.  Kuna baadhi wamesema atakuwa amevunja kiapo, na wengine wamesema atakuwa hakukivunja. 

 

Kigezo cha ruksa ya kuapa kutokana na kulazimika, ni Kauli Yake Ta’aalaa:

 

مَن كَفَرَ بِاللَّـهِ مِن بَعْدِ إِيمَانِهِ إِلَّا مَنْ أُكْرِهَ وَقَلْبُهُ مُطْمَئِنٌّ بِالْإِيمَانِ وَلَـٰكِن مَّن شَرَحَ بِالْكُفْرِ صَدْرًا فَعَلَيْهِمْ غَضَبٌ مِّنَ اللَّـهِ وَلَهُمْ عَذَابٌ عَظِيمٌ﴿١٠٦﴾

 

106.  Atakayemkufuru Allaah baada ya iymaan yake - isipokuwa yule aliyekirihishwa (kukanusha) na huku moyo wake umetua juu ya iymaan - lakini aliyekifungulia ukafiri kifua chake, basi hao juu yao ni ghadhabu kutoka kwa Allaah na watapata adhabu kuu.  [An-Nahl].

 

Ikiwa kulazimishwa kunahalalisha neno la ukafiri, basi kuhalalishwa kiapo cha uongo ni ruksa zaidi.

 

Toka kwa Suwayd bin Handhwalah amesema:

 

"خَرَجْنَا نُرِيدُ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ ، وَمَعَنَا وَائِلُ بْنُ حُجْرٍ فَأَخَذَهُ عَدُوٌّ لَهُ فَتَحَرَّجَ الْقَوْم أَنْ يَحْلِفُوْا فَحَلَفْتُ أَنَا أَنَّهُ أَخِيْ، فَذَكَرْتُ ذلِكَ لِلنَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فَقَالَ: ‏ "صَدَقْتَ ، الْمُسْلِمُ أَخُوْ الْمُسْلِمِ "

 

“Tulitoka kwenda kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) tukiwa pamoja na Waail bin Hujr.  Maadui zake wakamkamata, na watu wakaona uzito kuapa.  Mimi nikaapa kuwa ni ndugu yangu.  Nikamweleza hilo Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) naye akasema:  Umesema kweli, Muislamu ni ndugu ya Muislamu”.  [Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh. Imekharijiwa na Abu Daawuwd (3070), Ibn Maajah (2119), Al-Haakim (4/333) na wengineo].

 

·        Je, Kafara Ni Lazima Katika Yamini Ya Ghamuws?

 

‘Ulamaa wana kauli mbili kuhusu suala hili:  [Angalia Fat-hul Qadiyr (4/3), As-Swaawiy (1/330), Asnal Matwaalib (4/240), Al-Mughniy (11/177), Al-Muhallaa (8/36), Majmuw’ul Fataawaa (33/128-35/324) na Fat-hul Baariy (11/557)].

 

Kauli Ya Kwanza:  Haina kafara, bali ni lazima kutubia kwa kuapa na kuwarejeshea watu haki yao.  Ni madhehebu ya Jumhuri.  Dalili yao ni:

 

1-  Hadiyth zilizotangulia zinazowakhofisha watu waepuke yamini ya ghamuws.

 

2-  Ni Al-Ash-‘ath aliposema -kuhusu Hadiyth iliyotangulia ya Ibn Mas-‘uwd-:

 

"فِيَّ أُنْزِلَتْ هذِهِ الآيَاتُ وَهِيَ قَوْلُهُ تَعَالى :  إِنَّ الَّذِينَ يَشْتَرُونَ بِعَهْدِ اللَّـهِ وَأَيْمَانِهِمْ ثَمَنًا قَلِيلًا أُولَـٰئِكَ لَا خَلَاقَ لَهُمْ فِي الْآخِرَةِ وَلَا يُكَلِّمُهُمُ اللَّـهُ وَلَا يَنظُرُ إِلَيْهِمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَلَا يُزَكِّيهِمْ وَلَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ ﴿٧٧﴾

 

“Aayaat hizi ziliteremshwa kunizungumzia mimi, nayo ni Kauli Yake Ta’aalaa:

 

77.  Hakika wale wanaobadilisha Ahadi ya Allaah na viapo vyao kwa thamani ndogo, hao hawana sehemu yoyote katika Aakhirah, na wala Allaah Hatowasemesha, na wala Hatowatazama Siku Ya Qiyaamah, na wala Hatowatakasa, na watapata adhabu iumizayo.  [Aal ‘Imraan].

 

Wamesema:  “Matini hizi zimethibitisha kuwa hukmu ya ghamuws ni adhabu Aakhirah.  Hivyo mwenye kuwajibisha kafara, basi amezidisha lisilokuwepo ndani ya matini”.

 

3-  Hadiyth ya Abu Hurayrah toka kwa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

"خَمْسٌ لَيْسَ فِيهِنَّ كَفَّارَةُ : الشِّرْكُ بِاللَّهِ عَزَّ وَجَلَّ، وَقَتْلُ النَّفْسِ بِغَيْرِ حَقِّ، وَبُهْتُ الْمُؤمِنِ، وَالْفِرَارُ مِنَ الزَّحْفِ ، ويَمِينٌ صابِرَةً يَقْتَطِعُ بِهَا مَالَا بِغَيْرِ حَقِّ"

 

“Matano hayana kafara:  Kumshirikisha Allaah ‘Azza wa Jalla, kuua nafsi bila haki, kumzulia Muumini, kukimbia Jihaad, na yamini ya ghamuws anamega kwayo mali pasina haki”.  [Hadiyth Dhwa’iyf.  Imekharijiwa na Ahmad (2/362), At-Twabaraaniy katika “Musnadu Ash-Shaamiyyiyna” (1183), Ibn Abi ‘Aaswim katika “Al-Jihaad” na katika “Ad-Diyaat” (1/16)].

 

4-  Toka kwa Ibn Mas-‘uwd amesema:

 

"كُنَّا نَعُدُّ الذَّنْبَ الَّذِيْ لَا كَفَّارَةَ لَهُ الْيَمِيْنَ الْغَمُوْسَ ، فَقِيْلَ : مَا الْيَمِيْنُ الْغَمُوْسُ؟ قَالَ : اقْتِطَاعُ الرَّجُلِ مَالِ أَخِيْهِ بِالْيَمِيْنِ الْكاذِبَةِ "

 

“Tulikuwa tunahesabu kati ya dhambi zisizo na kafara ni yamini ya ghamuws. Pakaulizwa:  Ni ipi yamini ya ghamuws?  Akasema:  Ni mtu kumega mali ya nduguye kwa kiapo cha uongo”.  [Isnaad yake ni Hasan.  Imekharijiwa na Al-Bayhaqiy (10/383)].

 

Wamesema:  “Hakuna Swahaba yeyote tumjuaye ambaye alipingana na Ibn Mas-‘uwd, bali hata Wanazuoni kadhaa wamenukuu itifaki ya Maswahaba wote juu ya hilo”.

 

5-  Yamini hii ni kubwa zaidi ya kutolewa kafara, na madhambi makubwa hayatolewi kafara.  Ni kama kuiba, kuzini na kunywa pombe, haya hayana kafara.

 

Kauli Ya Pili:  Yamini ina kafara.  Ni madhehebu ya Ash-Shaafi’iy, riwaya toka kwa Ahmad na Ibn Hazm.   Hoja yao ni:

 

1-  Ghamuws ni yamini iliyochumwa, iliyokusudiwa, na chumo ni tendo la moyo.  Na kukusudia ni kuazimia, na yeyote mwenye kuapa kwa uwongo na kwa kukusudia, basi huyo ni mtendaji kwa moyo wake kwa kupania.  Huyu atawajibishwa kwa mujibu wa Kauli Yake Ta’aalaa:

 

"وَلَـٰكِن يُؤَاخِذُكُم بِمَا كَسَبَتْ قُلُوبُكُمْ"

 

“Lakini Atakuchukulieni kwa yaliyochuma nyoyo zenu”.  [Al-Baqarah (2:225)].

 

2-  Allaah Ta’aalaa Amesema:

 

"لَا يُؤَاخِذُكُمُ اللَّـهُ بِاللَّغْوِ فِي أَيْمَانِكُمْ وَلَـٰكِن يُؤَاخِذُكُم بِمَا عَقَّدتُّمُ الْأَيْمَانَ ۖ فَكَفَّارَتُهُ إِطْعَامُ عَشَرَةِ مَسَاكِينَ مِنْ أَوْسَطِ مَا تُطْعِمُونَ أَهْلِيكُمْ أَوْ كِسْوَتُهُمْ أَوْ تَحْرِيرُ رَقَبَةٍ ۖ فَمَن لَّمْ يَجِدْ فَصِيَامُ ثَلَاثَةِ أَيَّامٍ ۚ ذَٰلِكَ كَفَّارَةُ أَيْمَانِكُمْ إِذَا حَلَفْتُمْ" 

 

89. “Allaah Hatokuchukulieni kwa viapo vyenu vya upuuzi, lakini Atakuchukulieni kwa (kuvunja) viapo mlivyoapa kwa niyyah mlioifunga thabiti.  Basi kafara yake ni kulisha maskini kumi chakula cha wastani mnachowalisha ahli zenu, au kuwavisha nguo, au kuacha huru mtumwa.  Lakini asiyeweza kupata (katika hayo), basi afunge Swiyaam siku tatu.  Hiyo ndio kafara ya viapo vyenu mnapoapa”.  [Al-Maaidah: 5].

 

Hapa Aayah inaeleza kuwa inaingia kiujumla kila yamini ambayo mwapaji wake ameivunja.  Na kafara haifutiki ila kwa dalili bayana.

 

3-  Neno lake Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

 "فَلِيَأْتِ الَّذِيْ هُوَ خَيْرٌ وَيُكَفِّرْ عَنْ يَمِينهِ"

 

“…..basi na afanye lile alionalo la kheri zaidi, na atolee kafara yamini yake”. [Isnaad yake ni Hasan.  Imekharijiwa na Al-Bayhaqiy (10/38)].

 

Wamesema:  Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) akamwamuru akivunje kiapo chake na akamwajibishia kafara.

 

4-  Yamini ya ghamuws inastahiki zaidi kutolewa kafara kuliko yamini nyinginezo zilizoazimiwa, kwa kuwa uwazi wa Aayah mbili zilizotangulia unatekelezeka juu yake bila “taqdiyr” (kuchomeka neno ili maana kusudiwa ikae sawa).  Pia kiapo hiki kinakuwa batili na chenye kuvunjika tokea pale anapokikusudia mtu na kukitamka.  Hivyo adhabu inakutanishwa na kiapo hiki kinyume na viapo vingine vilivyoazimiwa ambavyo havina adhabu ila tu kama vitavunjwa.  Viapo hivi ili Aayah hizi mbili zitekelezeke juu yake, zinahitajia “taqdiyr” kwa kusemwa:

 

"وَلَـٰكِن يُؤَاخِذُكُم بالحنث بِمَا كَسَبَتْ قُلُوبُكُمْ"

 

“Lakini Atakuchukulieni kwa kuvunja yaliyochuma nyoyo zenu”.

 

Na katika Kauli Yake:

 

"إِذَا حَلَفْتُمْ" أَيْ : حَلَفْتُمْ وَحَنَثْتُمْ

 

“mnapoapa na mkavunja kiapo”.

 

·        Kauli Yenye Nguvu:

 

Linaloonekana ni kuwa kutowajibishwa kafara ndiko kwenye nguvu zaidi.  Dalili za wenye kupinga hili zinaradiwa kwa kuambiwa kuwa yamini ya ghamuws si yamini kiuhalisia, kwa kuwa yamini ni kifungo halali cha kisheria, lakini ghamuws ni dhambi kubwa lisilo na shaka yoyote, na dhambi kubwa ni kinyume ya jambo halali la kisheria.  Na yamini hii ya ghamuws imeitwa yamini kimajazi tu kwa kuwa inafanyika katika picha ya kiapo.  Isitoshe, yamini inakuwa ni ghamuws kwa kuwa mtu anakusudia kusema uongo na hana niya ya kuivunja.  Hivyo Hadiyth haitoshelezi kwa dalili.

 

Na yaliyotangulia katika mlango wa “Al-Li’aan” (mume kumtuhumu mkewe zinaa) yanatilia nguvu hili pale Rasuli  (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) alipowaambia wenye kulaaniana wawili:

 

"‏ اللَّهُ يَعْلَمُ أَنَّ أَحَدَكُمَا كَاذِبٌ، فَهَلْ مِنْكُمَا تَائِبٌ ‏"‏‏

 

“Allaah Anajua kwamba mmoja wenu ni mwongo, basi je mmoja wenu atatubu?”.  [Hadiyth Swahiyh].

 

Lau kama kafara ingekuwa ni lazima kwa mmoja wao kwa kuwa amekusudia uongo, basi kubainisha hilo kungehitajika zaidi kuliko kubainisha suala la tawbah.  Allaah Ndiye Ajuaye zaidi lililo sahihi.

                                               

  

 

 

Share