026-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Viapo Na Nadhiri: Kafara Ya Yamini

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

 

كِتَابُ الأَيْمَانِ وَالنُّذُوْرِ

 

Kitabu Cha Viapo Na Nadhiri

 

026- Kafara Ya Yamini

 

Alhidaaya.com

 

 

  الكَفَّارَةُ “kafara” limenyambulika toka neno الْكُفْرُ  “ukafiri” lenye maana ya kusitiri na kufunika.   Na kafara ya yamini ni kile ambacho ni waajib kukifanya kwa kuvunja kiapo.  Imeitwa hivyo kwa kuwa “inakaffir” yaani inafunika dhambi la kutotekeleza kiapo, hivyo mhusika hatoadhibiwa kwalo Siku ya Qiyaamah.

 

Kafara ya yamini ya kuapa kwa Jina la Allaah Ta’aalaa imethibiti katika Qur-aan, Sunnah na ‘Ijmaa.

 

Allaah Ta’aalaa Ameitaja katika Kitabu Chake Aliposema:

 

"لَا يُؤَاخِذُكُمُ اللَّـهُ بِاللَّغْوِ فِي أَيْمَانِكُمْ وَلَـٰكِن يُؤَاخِذُكُم بِمَا عَقَّدتُّمُ الْأَيْمَانَ ۖ فَكَفَّارَتُهُ إِطْعَامُ عَشَرَةِ مَسَاكِينَ مِنْ أَوْسَطِ مَا تُطْعِمُونَ أَهْلِيكُمْ أَوْ كِسْوَتُهُمْ أَوْ تَحْرِيرُ رَقَبَةٍ ۖ فَمَن لَّمْ يَجِدْ فَصِيَامُ ثَلَاثَةِ أَيَّامٍ ۚ ذَٰلِكَ كَفَّارَةُ أَيْمَانِكُمْ إِذَا حَلَفْتُمْ ۚ وَاحْفَظُوا أَيْمَانَكُمْ ۚ كَذَٰلِكَ يُبَيِّنُ اللَّـهُ لَكُمْ آيَاتِهِ لَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ"

 

89. Allaah Hatokuchukulieni kwa viapo vyenu vya upuuzi, lakini Atakuchukulieni kwa (kuvunja) viapo mlivyoapa kwa niyyah mlioifunga thabiti. Basi kafara yake ni kulisha maskini kumi chakula cha wastani mnachowalisha ahli zenu, au kuwavisha nguo, au kuacha huru mtumwa.  Lakini asiyeweza kupata (katika hayo), basi afunge Swiyaam siku tatu.  Hiyo ndio kafara ya viapo vyenu mnapoapa.  Na hifadhini yamini zenu.  Hivyo ndivyo Allaah Anavyokubainishieni Aayaat (na Hukmu) Zake ili mpate kushukuru.”  [Al-Maaidah 89].

 

Aayah hii Tukufu imebainisha kwamba kafara ya yamini iliyofungika ni waajib kwa kuchaguzwa mhusika kwa mujibu wa utaratibu ufuatao:

 

1-  Kulisha.          2-  Kuvisha Nguo.          3-  Kuacha Huru Mtumwa.

 

Akishindwa haya matatu, basi ni lazima afunge siku tatu.  Na haijuzu kufanya kafara hii ya kufunga ila baada ya kushindwa kuyafanya mambo matatu hayo ya kwanza.  Hili ndilo lililokubaliwa kwa ‘Ijmaa ya ‘Ulamaa wote.

 

Hebu sasa tuyachambue mambo haya na vipengele vyake.

 

1-       Kulisha

 

·        Idadi Ya Masikini Wa Kulishwa

 

[Al-Mabsuwtw (8/50), Al-Ummu (7/91), Al-Mughniy (11/258), Al-Muhallaa (8/72) na Fiqhul Aymaan (uk 214-215)].

 

Katika Aayah Tukufu imeelezwa kwamba kafara inakuwa kwa kuwalisha masikini kumi.  Sasa je itajuzu kumlisha masikini mmoja mara kumi, au masikini wawili mara tano kila mmoja na kama hivi?

 

Kuna kauli mbili za ‘Ulamaa kuhusu hili.  Ya kwanza inasema kwamba inavyoonekana kiuwazi ni kuwa ni lazima kuwalisha masikini kumi kutokana na ubainisho wa Aayah.  Ni madhehebu ya Ash-Shaafi’iy, Ahmad na Ibn Hazm.

 

Ya pili ambayo ni ya Abu Haniyfah inasema inatosha kumlisha masikini mmoja mara kadhaa kwa sharti ya kupewa chakula kwa mpigo!!

 

·        Aina Ya Chakula Na Kipimo Chake

 

[Ibnu ‘Aabidiyna (3/478), Rawdhwatut Twaalibiyna (8/304), Al-Mudawwanah (2/39), Al-Muhallaa (8/72) na Majmuw’ul Fataawaa (35/349)].

 

Mielekeo ya ‘Ulamaa imetofautiana kuhusiana na kiasi cha chakula cha kafara. Jumhuwr –kinyume na Maalik- wanasema kafara ya chakula hukadiriwa kwa vipimo vya kisharia.

 

Madhehebu ya Abu Haniyfah yanasema atalisha kila masikini pishi moja ya ngano, au tende, au shayiri au unga.

 

Ama madhehebu ya Ash-Shaafi’iy, haya yanasema inamtosheleza kibaba, na hii pia ni kauli ya Mahanbali.  Hoja yao ya kukadiria kwa kibaba ni Hadiyth ya Naafi’u aliyesema:

 

"كَانَ ابْنُ عُمَرَ يُعْطِي زَكَاةَ رَمَضَانَ بِمُدِّ النَّبِيِّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ الْمُدِّ الأَوَّلِ، وَفِي كَفَّارَةِ الْيَمِينِ بِمُدِّ النَّبِيِّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ ".

 

“Ibn ‘Umar alikuwa akitoa Zakaah ya Ramadhwaan (fitr) kwa kipimo cha kibaba cha Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kibaba cha mwanzo.  Na katika kafara ya yamini kwa kipimo cha kibaba cha Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam)”.  [Hadiyth Swahiyh].

 

Na hoja ya waliokadiria kwa pishi ni athar ya ‘Umar bin Al-Khattwaab yeye alikuwa:

 

"يُطْعِمُ عَشَرَةَ مَسَاكِيْنَ –كُلَّ مِسْكِيْنِ- صَاعًا مِنْ شَعِيْرٍ أَوْ صَاعًا مِنْ تَمْرٍ أَوْ نِصْفِ صَاعٍ مِنْ قَمْحٍ".

 

“Analisha masikini kumi –kila masikini- pishi ya shayiri, au pishi ya tende, au nusu pishi ya ngano”.  [Swahiyh.  Imekharijiwa na ‘Abdul Razzaaq (10675) na At-Twabariy (5/13)].

 

Lakini kwa upande mwingine, Al-Imaam Maalik na Ibn Hazm –nalo pia ni chaguo la Sheikh wa Uislamu- wanaona kwamba chakula cha kuwalisha masikini kinakadiriwa kwa mujibu wa ada na mazoea ya watu, na si kwa mujibu wa kipimo cha kisharia.  Hivyo watu wa kila mkoa (mji, kijiji, nchi n.k) watalisha chakula cha daraja la wastani ambacho wanawalisha watu wao kwa kiasi na kwa aina.  Na hii ni kutokana na Neno Lake Ta’aalaa:

 

"فَكَفَّارَتُهُ إِطْعَامُ عَشَرَةِ مَسَاكِينَ مِنْ أَوْسَطِ مَا تُطْعِمُونَ أَهْلِيكُمْ"

 

“basi kafara yake ni kulisha maskini kumi chakula cha wastani mnachowalisha ahli zenu”.  [Al-Maaidah: 89].

 

Sheikh wa Uislamu amesema (35/349):  “Lililonukuliwa toka kwa Maswahaba na Taabi’iyna ni kauli hii.  Na kwa ajili hiyo walikuwa wanasema:  Cha wastani ni mkate na maziwa, mkate na siagi (samli), mkate na tende, na cha juu zaidi mkate na nyama.  Tumezielezea kwa upana aathaar zinazowahusu mahala pengine, na tumebainisha kwamba kauli hii ndiyo sahihi ambayo imegusiwa na Qur-aan, Sunnah na kuzingatia hali halisia…”.

 

[Angalia aathaar hizo katika Tafsiyr At-Twabariy (5/12-13), Muswannaf ‘Abdul Razzaaq (8/507) na Sunan Al-Bayhaqiy (10/55).  Ndugu yetu ‘Iswaam amezitaja baadhi ya zilizo swahiyh kwake katika kitabu cha Fiqhul Aymaan (uk. 217-219)].

 

Sheikh wa Uislamu ameendelea kusema (35/353):  “Linalochaguliwa, ni kurejeshwa suala kwenye ada na desturi za watu.  Katika mji fulani kinaweza kutosheleza alichokiwajibisha Abu Haniyfah, katika mji mwingine alichokiwajibisha Ahmad, na katika mji mwingine kati ya hiki na kile kwa mujibu wa ada za kila mji kwa mujibu wa Kauli Yake Ta’aalaa:

 

"مِنْ أَوْسَطِ مَا تُطْعِمُونَ أَهْلِيكُمْ"

 

“cha wastani mnachowalisha ahli zenu”.  [Al-Maaidah: 89].

 

Ninasema:  “Na hili ndilo sahihi kutokana na yaliyotangulia.  Na wala halipingani na kafara walizozitoa baadhi ya Maswahaba, kwani hilo lilikuwa linaendana na ada na desturi za miji yao.  Na kwa ajili hiyo Maalik amesema: “Ama kwetu sisi hapa, basi atoe mtu kafara yake kwa kibaba cha Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika yamini.  Ama watu wa miji mingine, basi hao maisha yao ni tofauti na maisha yetu.  Hivyo naona watoe kafara ya chakula cha wastani kwa mujibu wa maisha yao”.

 

·        Je, Yatosheleza Kuwalisha Tu Masikini Au Ni Lazima Kuwakabidhi Mlo?

 

1-  Jumhuwr;  Maalik, Ash-Shaafi’iy na Ahmad wanasema ni lazima kuwakabidhi masikini chakula.  Na kama atawalisha mlo wa mchana au mlo wa usiku, basi haitoshelezi, kwa kuwa yaliyonukuliwa toka kwa Maswahaba ni kuwa wao walimpa kibaba kimoja kila masikini, na kwa vile pia chakula hicho ni mali ambayo imekuwa ni waajib kuwapa masikini kisharia, hivyo basi ni lazima kuwakabidhi kama Zakaah.  Isitoshe, kuwakabidhi kunaingia ndani ya wigo wa kuwalisha kama ilivyo katika Hadiyth:

 

"أَطْعَمَ رَسُولُ اللَّهِ الجَدَّ السُدُسً"

 

“Rasuli wa Allaah alimpa babu sudusi”.  [Hadiyth Dhwa’iyf.  Angalia Al-Irwaa (6/121)].

 

2-  Lakini Abu Haniyfah –na riwaayah toka kwa Ahmad- Ath-Thawriy, Al-Awzaa’iy, Al-Hasan na wengineo wanaona kwamba inatosheleza kuwalisha chakula cha mchana au cha usiku.  Hili pia ni chaguo la Sheikh wa Uislamu, kwa kuwa makusudio hasa ni ulishaji na si umilikishaji, na hili limegusiwa na naswi, na kwa kuwa kumwezesha masikini kupata chakula ndio kumlisha kwenyewe. Allaah Ta’aalaa Amesema:

 

"وَيُطْعِمُونَ الطَّعَامَ عَلَىٰ حُبِّهِ مِسْكِينًا وَيَتِيمًا وَأَسِيرًا"

 

8.  Na wanalisha chakula, juu ya kukipenda, masikini na mayatima na mateka. [Al-Insaan:  08].

 

Hivyo, kwa namna yoyote ile akimlisha, itaingia ndani ya maana ya Aayah.  Na ndio pia katika kumkabidhi, ni sawa na kumlisha kamili.  Na kwa yote mawili, wajibu unatekelezeka.

 

Ninasema:  “Na hili ndilo sahihi zaidi.  Lau atawalisha masikini kumi chakula cha mchana au cha usiku, chakula cha wastani walichozoea kukipika, basi atakuwa ametekeleza kafara yake na itakuwa imemtosheleza.  Allaah Ndiye Ajuaye zaidi”.

 

2-      Kuvisha Nguo

 

Inamtosheleza kutoa kile ambacho kinajulikana na wote kuwa ni kivazi ambacho kikawaida huvaliwa na watu masikini.  Maalik na Ahmad wamekikadiria kuwa na upana wa kusitiri uchi katika Swalaah, kwa mwanamume au mwanamke. [Al-Mudawwanah (2/44), Al-Ummu (8/92), Al-Mughniy (11/260), na Al-Muhallaa (8/75).  Ndani kuna maneno yenye faida kubwa].

 

·        Faida:

 

Haitoshelezi kutoa pesa badala ya chakula na nguo.  Ni kauli ya Jumhuwr kinyume na Abu Haniyfah.  [Al-Ummu (7/91), Al-Mudawwanah (2/40), Al-Muhallaa (8/69), Al-Mughniy (11/256) na Al-Mabsuwtw (8/154)].

 

3-      Kuacha Huru Mtumwa

 

Ni kumkomboa na kumwacha huru.  Jumhuwr kinyume na Abu Haniyfah wameshurutisha anayeachwa huru awe Muislamu kwa kuibebesha Aayah ya kafara ya yamini isiyo ainishi (mutwlaq) juu ya Aayah ainishi (muqayyad) ya kafara ya kuua na dhwihaar pale Aliposema Allaah:

 

"فَتَحْرِيرُ رَقَبَةٍ مُّؤْمِنَةٍ"

 

basi aachilie huru mtumwa Muumin”.  [An-Nisaa: 92].

 

Ninasema:  “Kuna mvutano wa kiuswuul katika kubebesha (Aayah) isio ainishi juu ya ainishi wakati wa kukubaliana hukmu na kutofautiana sababu.  La sahihi ni kuwa haibebeshwi juu yake.  Hivyo madhehebu ya Abu Haniyfah yanakuwa na nguvu zaidi, na kwa hivyo haishurutishwi anayeachwa huru katika kafara ya yamini awe Muislamu.  Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi”.

 

4-      Kufunga (Kama Atashindwa Kufanya Lolote Katika Matatu Yaliyotangulia)

 

Akishindwa kulisha, au kuvisha, au kuacha huru, basi atafunga siku tatu.

 

·        Je, Ni Lazima Afunge Siku Tatu Mfululizo?

 

Abu Haniyfah, Ath-Thawriy na Ahmad, wanasema ni waajib kuandamisha siku tatu mfululizo.  Wametoa dalili ya kisomo cha Ibn Mas-‘uwd na Ubayya ambapo wawili hawa wamelisoma Neno Lake Ta’aalaa:

 

" فَصِيَامُ ثَلَاثَةِ أَيَّامٍ مُتَتَابِعَاتٍ"

 

basi afunge Swiyaam siku tatu mfululizo”.  Wamesema hii ni Qur-aan, kwa hiyo ni hujjah.  Na kama si Qur-aan, basi ni riwaayah toka kwa Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kuwa inawezekanika kuwa wawili hao wameisikia kama tafsiyr toka kwa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wakadhania ni Qur-aan.  Na kwa makadirio yote mawili, hiyo ni hujjah!! Isitoshe, wakaongeza kusema kuwa na kwa vile hiyo ni Swiyaam ya kafara, imekuwa lazima kuandamisha siku mfano wa kafara ya kuua na ya dhwihaar!!

 

Lakini kwa upande wa Maalik, Ash-Shaafi’iy, Ahmad na Ibn Hazm, hawa wanasema si lazima kufululiza siku katika funga ya kafara ya yamini.  Hujjah yao ni kwamba Swawm haikushurutishwa kufululiza siku zake katika Miswahafu tuliyonayo, na kisomo cha Ibn Mas-‘uwd na Ubayya ni kisomo kisichojulikana na wengi, hivyo hakuna hujjah ndani yake.  Hivyo basi, mwenye kufunga siku tatu kwa picha yoyote ile, itatosha.

 

Na kwa vile pia hakuswihi kuibebesha ainishi juu ya isiyo ainishi pamoja na kutofautiana sababu kama lilivyogusiwa hilo nyuma.

 

Ninasema:  “Kauli hii ya kutolazimu kufuatanisha siku ndio yenye nguvu zaidi katika funga ya kafara ya yamini”.

 

·        Kutoa Kafara Kunatosheleza Kabla Ya Kuvunja Kiapo Na Baada Yake?

 

Hakuna makhitilafiano yoyote kati ya ‘Ulamaa ya kwamba kafara haimwajibikii mtu ila baada ya kuvunja kiapo chake.  Kisha wakakhitilafiana kuhusu kama atatanguliza kafara kabla ya kuvunja kiapo, je itamtosheleza?

 

Jumhuwr wanasema itamtosheleza, ingawa ubora ni kuichelewesha hadi baada ya kuvunja kiapo.  Kauli hii imenasibishwa kwa Maswahaba kumi na nne na idadi kubwa ya Taabi’iyna.

 

Abu Haniyfah na Maswahibu zake wanaona kwamba haitoshelezi kabla ya kuvunja kiapo.

 

Ash-Shaafi’iy kasema:  “Haitoshelezi kwa Swawm, lakini kwa mengine inatosheleza”.  [Al-Mughniy (11/222), Al-Muhallaa (8/67), Al-Mabsuwtw (8/148) na Sharhu Muslim cha An-Nawawiy].

 

Ninasema:  “La sawa na sahihi ni kauli ya Jumhuwr.  Lau kama atafanya kafara ya yamini yake kabla ya kuvunja kiapo chake au baada ya yamini, basi itamtosha.  Matamshi ya Hadiyth kadhaa yanazatiti mwelekeo huu.  Katika Hadiyth ya ‘Abdul Rahmaan bin Samurah, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia:

 

"إِذَا حَلَفْتَ عَلَى يَمِينٍ، فَرَأَيْتَ غَيْرَهَا خَيْراً مِنْهَا، فَكَفِّرْ عَنْ يَمِيْنِكَ، وَائْتِ اَلَّذِي هُوَ خَيْرٌ".

 

“Ukiapa yamini, kisha ukaona jambo jingine ni bora zaidi ya uliloliapia, basi fanyia kafara yamini yako, na ufanye hilo ambalo ni bora zaidi”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na An-Nasaaiy (7/10) na Abu Daawuwd (3278)].

 

Hadiyth hii iko wazi kabisa katika kujuzu kutanguliza kafara kabla ya kuvunja kiapo, bali pia inaonyesha wajibu wa hilo lau si ‘Ijmaa ya ‘Ulamaa iliyo kinyume chake, ingawa ubora zaidi ni kuichelewesha kafara ili kutoka nje ya duara la mvutano.  Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.

 

·        Je, Idadi Ya Kafara Inaongezeka Kwa Idadi Ya Viapo?

 

1-  Hakuna makhitalifiano yoyote kuhusu mwenye kuapa yamini kisha akaivunja na akatekeleza kafara iliyomwajibikia, kwamba lau ataapa yamini nyingine na akaivunja ni lazima atoe kafara nyingine.

 

2-  Akiapa yamini zaidi ya moja kwa mambo tofauti tofauti, la sawa ni kuwa lau atavunja kiapo kwenye jambo lolote kati ya hayo, basi ni lazima alitolee kafara. Na akivunja kwenye jingine, basi pia atalitolea kafara na hivyo hivyo.  Na kafara haziingiliani, kafara ya jambo fulani haiingii kwenye jambo jingine.

 

3-  Akiapa viapo kadhaa kwa jambo moja katika majlisi moja au majilisi tofauti, hapa Abu Haniyfah, Maalik na Ahmad wamesema itamlazimu kafara kwa kila kiapo.

 

Ash-Shaafi’iy kasema:  “Akinuwia kwa kiapo cha pili kusisitizia kiapo cha kwanza, basi atatoa kafara ya kiapo kimoja tu”.

 

Ahmad amesema katika riwaayah nyingine na ambapo ni chaguo la Sheikh wa Uislamu na Ibn Hazm:  “Itamwajibikia kafara moja tu kwa hali yoyote”.

 

Ninasema:  “Hili ndilo lililo karibu zaidi.  Allaah Ndiye Mjuzi zaidi”.

 

                                                            ……………………………

 

 

 

 

 

 

 

 

Share