027-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Viapo Na Nadhiri: Nadhiri

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

 

كِتَابُ الأَيْمَانِ وَالنُّذُوْرِ

 

Kitabu Cha Viapo Na Nadhiri

 

 

027- Nadhiri

 

Alhidaaya.com

 

 

 

·        Taarifu  Yake:

 

النُّذُوْرُ" nadhiri” ni wingi wa"نُذُرٌ"   Maana yake katika lugha ni ahadi ambayo mtu anajilazimishia mwenyewe kuitekeleza kwa khiyari yake.  Ama kisharia, ni mtu kujilazimishia mwenyewe kufanya jambo jema la utiifu kwa Allaah ambalo halikuwa ni waajib kwake, naye akalifanya liwe waajib kwake kwa tamshi linalohisisha hivyo.

 

·        Hukmu Ya Kujiwekea Nadhiri:

 

Hadiyth Swahiyh zinazogusia suala la nadhiri zinaonyesha kuwa mtu hatakikani kuweka nadhiri, na kwamba jambo hilo limekatazwa.  Na kwa ajili hiyo, Wanachuoni wengi wamesema ni makruhu, lakini kama mtu atajiwekea, basi ni lazima aitekeleze nadhiri hiyo.  [Al-Muhallaa (8/2), Subulus Salaam (4/1446) na Naylul Awtwaar (8/277)].

 

1-  Toka kwa Ibn ‘Umar, amesema:

 

 

"إنَّهُ لا يَرُدُّ شَيْئًا، وَإنَّمَا يُسْتَخْرَجُ بِهِ مِنَ اَلْبَخِيلِ".

 

“Hakika (nadhiri) hairudishi lolote (lililopangwa na Allaah), bali hutolewa kwayo (‘amali njema) toka kwa bakhili (wa kutenda mema)”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (6693) na Muslim (1639)].

 

2-  Toka kwa Abu Hurayrah, amesema:  Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

 

"لا تَنْذِرُوْا، فإنَّ النَّذْرَ لا يُغْنِي مِنَ القَدَرِ شيئًا، وإنَّمَا يُسْتَخْرَجُ بِهِ مِنَ البَخِيْلِ".

 

“Msiweke nadhiri, kwani nadhiri haisaidii lolote katika Qadar, bali hutolewa kwayo (‘amali njema) toka kwa bakhili (wa kutenda mema)”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Muslim (1640), At-Tirmidhiy 1538), An-Nasaaiy (7/16) na Ahmad (2/412)].

 

3-  Toka kwa Abu Hurayrah, amesema: Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

 

"إنَّ النَّذْرَ لا يُقَرِّبُ مِنِ ابْنِ آدَمَ شيئًا لَمْ يَكُنِ اللَّهُ قَدَّرَهُ له، وَلَكِنِ النَّذْرُ يُوَافِقُ القَدَرَ، فيُخْرَجُ بِذلكَ مِنَ البَخِيلِ ما لَمْ يَكُنِ البَخِيلُ يُرِيدُ أَنْ يُخْرِجَ".

 

“Hakika nadhiri haimsogezei mwanadamu lolote ambalo Allaah Hakuwa Amemkadiria, lakini nadhiri inasadifu Qadar, na hivyo kutolewa kwa hilo toka kwa bakhili jambo ambalo bakhili hakuwa anataka kulifanya”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (6694) na Muslim (1640)].

 

Qur-aan na Hadiyth zimedulisha ulazima wa kutekeleza nadhiri –ya jambo jema- na zimewasifu watekelezaji wake.

 

1-  Allaah Ta’aalaa Amesema:

 

"ثُمَّ لْيَقْضُوا تَفَثَهُمْ وَلْيُوفُوا نُذُورَهُمْ"

 

29.  Kisha wajisafishe taka zao na watimize nadhiri zao.  [Al-Hajj: 29].

 

2-  Toka kwa ‘Aaishah, Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

 

"مَنْ نذَرَ أنْ يُطيْعَ اللهَ فلْيُطِعْه وَمَنْ نَذَرَ أنْ يَعْصِيَ اللهَ فَلا يَعْصِهِ".

 

“Mwenye kuweka nadhiri kwamba atamtii Allaah, basi amtii, na mwenye kuweka nadhiri kwamba atamuasi Allaah, basi asimuasi”.  [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (6696), Abu Daawuwd (3289), At-Tirmidhiy (1526), An-Nasaaiy (7/17) na Ibn Maajah (2126)].

 

3-  Toka kwa ‘Imraan bin Huswayn, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"خَيْرُكُمْ قَرْنِي، ثُمَّ الَّذِينَ يَلُونَهُمْ، ثُمَّ الَّذِينَ يَلُونَهُمْ - قالَ عِمْرانُ: لا أدْرِي: ذَكَرَ ثِنْتَيْنِ أوْ ثَلاثًا بَعْدَ قَرْنِهِ - ثُمَّ يَجِيءُ قَوْمٌ، يَنْذِرُونَ ولا يَفُونَ، ويَخُونُونَ ولا يُؤْتَمَنُونَ، ويَشْهَدُونَ ولا يُسْتَشْهَدُونَ، ويَظْهَرُ فِيهِمُ السِّمَنُ".

 

“Wabora wenu zaidi ni wa karne yangu, kisha wale wanaowafuatia (Taabi’iyna), kisha wale wanaowafuatia hao (Taabi’ut-taabi’iyna) –‘Imraan akasema:  Sijui, ametaja karne mbili au tatu baada ya karne yake - kisha watakuja watu ambao wataweka nadhiri wala hawatozitekeleza, watafanya khiyana na watu hawatowaamini, na watatoa ushahidi bila kutakwa wautoe, na unene utaonekana kwenye miili yao”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (2651) na Muslim (2335)].

 

Hadiyth iko wazi kwamba wasio tekeleza nadhiri zao, wanabeba dhambi.

 

4-  Allaah Subhaanahu Akiwasifia wenye kutekeleza nadhiri zao Anasema:

 

إِنَّ الْأَبْرَارَ يَشْرَبُونَ مِن كَأْسٍ كَانَ مِزَاجُهَا كَافُورًا﴿٥﴾ عَيْنًا يَشْرَبُ بِهَا عِبَادُ اللَّـهِ يُفَجِّرُونَهَا تَفْجِيرًا﴿٦﴾ يُوفُونَ بِالنَّذْرِ وَيَخَافُونَ يَوْمًا كَانَ شَرُّهُ مُسْتَطِيرًا﴿٧﴾

 

 

5.  Hakika Waumini watendao wema kwa wingi watakunywa katika vikombe vya mvinyo, mchanganyiko wake ni Kaafuwr.  6.  Nayo ni chemchemu watakayokunywa toka humo Waja wa Allaah, wataibubujua kwa wingi.  7. Wanatimiza nadhiri na wanaiogopa siku ambayo shari yake ni yenye kuenea kwa upana.   [Al-Insaan: 5-7].

 

 

5-  Amesema tena Ta’aalaa:

 

 

"وَمَا أَنفَقْتُم مِّن نَّفَقَةٍ أَوْ نَذَرْتُم مِّن نَّذْرٍ فَإِنَّ اللَّـهَ يَعْلَمُهُ"

 

270.  Na chochote mtoacho au mkiwekacho nadhiri, basi hakika Allaah Anakijua. [Al-Baqarah: 270].

 

 

 

 

Share