001-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Mavazi Na Mapambo Na Hukmu Za Kuangalia: Mavazi Na Mapambo Kwa Wanaume: Wajibu Wa Kusitiri Uchi:

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

 

كِتَابُ اللِّبَاسِ وَالزِّيْنَةِ  وَأَحْكَامُ النَّظَرِ

 

 Kitabu Cha Mavazi Na Mapambo Na Hukmu Za Kuangalia 

 

 

اللِّبَاسُ وَالزِّيْنَةُ للرِّجَالِ 

Mavazi Na Mapambo Kwa Wanaume 

 

 

Alhidaaya.com 

 

 

 

001-Mavazi Na Mapambo Kwa Wanaume: Wajibu Wa Kusitiri Uchi:

 

Maana ya uchi katika lugha, ni kila kasoro inayohofiwa kufichuka kutokana na mwanya au mvujo.  Na uchi ni sehemu ya kufichwa vizuri isiweze kuonekana kirahisi, na uchi wa mwanaume na mwanamke ni tupu zao mbili.  [Lisaanul ‘Arab 4/416].

 

Ama katika istilahi, uchi ni kila ambacho Allaah Ta’aalaa Ameharamisha kukionyesha mbele ya mtu ambaye si halali kwake kukiangalia.  [Nihaayatul Muhtaaj (2/5) na Tafsiyrul Qurtubiy (7/182)].

 

Sharia imewajibisha kuhifadhi na kusitiri nyuchi zisionekane na mtu ambaye si halali kwake kuziona.

 

1-  Allaah Ta’aalaa Amesema:

 

"يَا بَنِي آدَمَ خُذُوا زِينَتَكُمْ عِندَ كُلِّ مَسْجِدٍ وَكُلُوا وَاشْرَبُوا وَلَا تُسْرِفُوا ۚ إِنَّهُ لَا يُحِبُّ الْمُسْرِفِينَ ﴿٣١﴾"

 

31.  Enyi wana wa Aadam!  Chukueni mapambo yenu katika kila Masjid.  Na kuleni na kunyweni na wala msifanye israfu.  Hakika Yeye (Allaah) Hapendi wanaofanya israfu.  [Al-A’araaf 31].

 

Waarabu wakati wa enzi ya ujahili, walikuwa wakitufu Al-Ka’abah uchi, mpaka Allaah Alipomtuma Muhammad (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Aayah hii ikateremka.  Mpiga mbiu wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) akatangaza na kusema: 

 

"أَنْ لَا يَطُوفَ بِالْبَيْتِ عُرْيَان"

 

“Asitufu yeyote Nyumba akiwa uchi”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (369) na Muslim (1347)].

 

Al-Qurtubiy (Rahimahul Laah) amesema:  “Agizo katika Aayah hii linawahusu watu wote ingawa mlengwa hapo ni wale waliokuwa wakitufu Nyumba uchi miongoni mwa Waarabu.  Agizo hilo ni jumuishi kwa kila Msikiti wanaposwalia watu, kwa kuwa linalozingatiwa ni ujumuishi kuwahusisha wote, na si sababu kutokana na watu maalum”.   [Al-Jaami’u Liahkaamil Qur-aan (7/189)].

 

2-  Allaah Ta’aalaa Amewakataza watu kufunua nyuchi zao na Akaliita hilo fitna.  Amesema Ta’aalaa:

 

"يَا بَنِي آدَمَ لَا يَفْتِنَنَّكُمُ الشَّيْطَانُ كَمَا أَخْرَجَ أَبَوَيْكُم مِّنَ الْجَنَّةِ يَنزِعُ عَنْهُمَا لِبَاسَهُمَا لِيُرِيَهُمَا سَوْآتِهِمَا"

 

“Enyi wana wa Aadam!  Asikufitinisheni kabisa shaytwaan kama alivyowatoa wazazi wenu katika Jannah huku akiwavua nguo zao ili awaonyeshe sehemu zao za siri”.  [Al-A’araaf: (28)].

 

3-  Kutokana na umuhimu wa kusitiri uchi na hadhi yake katika Uislamu, Allaah Ameliambatanisha hili sambamba na taqwa pale Aliposema:

 

يَا بَنِي آدَمَ قَدْ أَنزَلْنَا عَلَيْكُمْ لِبَاسًا يُوَارِي سَوْآتِكُمْ وَرِيشًا ۖ وَلِبَاسُ التَّقْوَىٰ ذَٰلِكَ خَيْرٌ"

 

“Enyi wana wa Aadam!  Kwa yakini Tumekuteremshieni libasi inayositiri tupu zenu (nguo), na libasi ya mapambo.  Na libasi ya taqwa ndiyo bora zaidi”.  [Al-A’araaf (26)].

 

4-  Toka kwa Bahz bin Hakiym toka kwa baba yake toka kwa babu yake, amesema, nilisema: 

 

"يَا رَسُولَ اللَّهِ ، عَوْرَاتُنَا مَا نَأْتِي مِنْهَا وَمَا نَذَرُ؟ قَالَ: ‏"‏احْفَظْ عَوْرَتَكَ إِلاَّ مِنْ زَوْجَتِكَ أَوْ مِمَّا مَلَكَتْ يَمِينُكَ‏"‏ ‏.‏ فَقَالَ:  الرَّجُلُ يَكُونُ مَعَ الرَّجُلِ؟ قَالَ: ‏"‏إِنِ اسْتَطَعْتَ أَنْ لاَ يَرَاهَا أَحَدٌ فَافْعَلْ" 

 

“Ee Rasuli wa Allaah!  Kuhusu nyuchi zetu, ni zipi ambazo tunaweza kuzifunika, na ni zipi ambazo tunaweza kuziachia?  Akasema:  Uhifadhi uchi wako isipokuwa kwa mkewe au watumwa wako.  Nikasema:  Ee Rasuli wa Allaah!  Vipi mwanaume akiwa na mwanaume mwenzake?  Akasema:  Ukiweza asiuone yeyote, basi fanya.  Nikasema:  Na mwanamume akiwa peke yake?  Akasema:  Allaah Ana haki zaidi ya kuonewa haya kuliko watu”.  [Hadiyth Hasan.  Imekharijiwa na Abu Daawuwd (7/40), At-Tirmidhiy (2769) na Ibn Maajah (1920)].

 

5-  Abu Sa’iyd Al-Khudriy (Radhwiya Allaah ‘anhu) amesema:  Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"لَا يَنْظُرُ الرَّجُلُ إِلَى عَوْرَةِ الرَّجُلِ وَلَا الْمَرْأَةُ إِلَى عَوْرَةِ الْمَرْأَةِ ، وَلَا يُفْضِي الرَّجُلُ إِلَى الرَّجُلِ فِي ثَوْبٍ وَاحِدٍ وَلَا تُفْضِي الْمَرْأَةُ إِلَى الْمَرْأَةِ فِي ثَوْبٍ وَاحِدٍ "

 

“Mwanaume haruhusiwi kuangalia uchi wa mwanaume mwenzake, wala  mwanamke kuangalia uchi wa mwanamke mwenzake.  Na mwanaume asigusane ngozi kwa ngozi na mwanaume mwenzake ndani ya nguo moja, na mwanamke pia asigusane ngozi kwa ngozi na mwanamke mwenzake ndani ya nguo moja”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Muslim (338), At-Tirmidhiy (2793) na Abu Daawuwd (4018)].

 

6-  Ni pamoja na dalili nyingine lukuki kuhusiana na wajibu wa kuinamisha chini macho, kuharamisha kuangalia uchi, wajibu wa kupiga hodi na mfano wa hayo ambayo yatakuja kufafanuliwa katika sehemu husika In Shaa Allaah.

 

 

 

Share