002-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Mavazi Na Mapambo Na Hukmu Za Kuangalia: Mavazi Na Mapambo Kwa Wanaume:Mpaka Wa Uchi Wa Mwanaume:

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

 

 

كِتَابُ اللِّبَاسِ وَالزِّيْنَةِ  وَأَحْكَامُ النَّظَرِ

 

 Kitabu Cha Mavazi Na Mapambo Na Hukmu Za Kuangalia 

 

 

اللِّبَاسُ وَالزِّيْنَةُ للرِّجَالِ 

Mavazi Na Mapambo Kwa Wanaume 

 

 

Alhidaaya.com 

 

 

 

002-  Mavazi Na Mapambo Kwa Wanaume: Mpaka Wa Uchi Wa Mwanaume:

 

Hakuna makhitilafiano yoyote kati ya ‘Ulamaa kuhusiana na wajibu wa kuusitiri uchi ili usionekane na watu isipokuwa ule uliovuliwa na dalili.  Lakini, ni upi mpaka wa uchi kwa upande wa mwanaume? 

 

‘Ulamaa katika hili wana kauli nyingi ambazo zinaweza kuchujwa na kuwa kauli mbili tu:

 

Ya kwanza:  Uchi wa mwanaume ni kati ya kitovu na magoti. 

 

Wenye kauli hii ni madhehebu ya Jumhuwr na wengineo.  Lakini pia wanavutana katika kuingia kitovu na magoti ndani ya duara la uchi.  Dalili zao ni:

 

1-  Hadiyth ambayo Al-Bukhaariy ameifanya “Mu’allaq” -ikiwa na anuani “Kuuguza”- toka kwa Ibn ‘Abbaas, Jarhad, na Muhammad bin Jahsh toka kwa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

"الفَخْذُ عَوْرَةٌ"

 

“Paja ni uchi”.  [Hadiyth Mu’allaq.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy]. 

 

2-  ‘Aliyy (Radhwiya Allaah ‘anhu):  Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliniambia:

 

"لَا تُبْرِزْ فَخِذَكَ ، وَلَا تَنْظُرْ إِلَى فَخِذِ حَيٍّ وَلَا مَيِّتٍ"

 

“Usiliwache wazi paja lako, na wala usiangalie paja la aliye hai wala la maiti”. 

 

Lakini Hadiyth hii ni Dhwa’iyf sana.  Imekharijiwa na Abu Daawuwd (3140, 4015), Ibn Maajah (2/228) na Al-Bayhaqiy (2/228). 

 

3-  Yaliyosimuliwa toka kwa ‘Amri bin Shu’ayb, toka kwa baba yake, toka kwa babu yake, kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"فَإِنَّ مَا تَحْتَ السُّرَّةِ إلى رُكْبَتِهِ مِنَ العَوْرَةِ"

 

“Kwani sehemu iliyo chini ya kitovu hadi kwenye goti lake ni uchi”.  [Al-Albaaniy ameihasinisha.  Imekharijiwa na Ahmad (2/187) na Ad-Daaraqutwniy (1/230).  Angalia Al-Irwaa (271)].

 

4-  Al-Musuwr bin Makhramah (Radhwiya Allaah ‘anhu) amesema:

 

"أَقْبَلْتُ بِحَجَرٍ ثَقِيلٍ أَحْمِلُهُ وَعَلَىَّ إِزَارٌ خَفِيفٌ ، فَانْحَلَّ إِزَارِي وَمَعِيَ الْحَجَرُ لَمْ أَسْتَطِعْ أَنْ أَضَعَهُ حَتَّى بَلَغْتُ بِهِ إِلَى مَوْضِعِهِ ، فَقَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ :‏ "‏ارْجِعْ إِلَى ثَوْبِكَ فَخُذْهُ وَلاَ تَمْشُوا عُرَاةً"

 

“Nilikakamia kulibeba jiwe zito nikiwa nimejifunga chini kipande hafifu cha shuka (izari).  Mara kipande hicho kikafunguka na kudondoka na jiwe nimeshalibeba, na sikuweza kulitua, nikaenda nalo hivyo hivyo mpaka nikalifikisha sehemu yake husika.  Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaniambia:  “Rejea ukaichukue nguo yako, na wala msitembee uchi”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Muslim (341) na Abu Daawuwd (4016)].

 

Kauli ya pili:  Uchi ni nyeti ya mbele na ya nyuma tu.

 

Ni riwaayah nyingine ya Ahmad, na riwaayah katika madhehebu ya Maalik, na ni kauli ya Adh-Dhwaahiriyyah.  Wametoa dalili kwamba paja si uchi kwa haya yafuatayo:

 

1-  Hadiyth ya Anas bin Maalik (Radhwiya Allaah ‘anhu):  ‏

 

"أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ  صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ غَزَا خَيْبَرَ ، فَصَلَّيْنَا عِنْدَهَا صَلاَةَ الْغَدَاةِ بِغَلَسٍ ، فَرَكِبَ نَبِيُّ اللَّهِ  صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ وَرَكِبَ أَبُو طَلْحَةَ وَأَنَا رَدِيفُ أَبِي طَلْحَةَ ، فَأَجْرَى نَبِيُّ اللَّهِ  صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فِي زُقَاقِ خَيْبَرَ ، وَإِنَّ رُكْبَتِي لَتَمَسُّ فَخِذَ نَبِيِّ اللَّهِ  صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ ، ثُمَّ حَسرَ الإِزَارُ عَنْ فَخِذِه حَتَّى إِنِّي أَنْظُرُ إِلَى فَخِذِ النَّبِيِّ  صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ"

 

“Kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliivamia Khaybar.  Tukaswali hapo Swala ya Alfajiri mwanzo wa wakati giza likiwa bado limetanda.  Halafu Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akampanda mnyama wake, na Abu Twalha naye akampanda wake, nami akanipakia nyuma.  Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwendesha kwa kasi mnyama wake kwenye vichochoro vya Khaybar.  Goti langu lilikuwa likigusa paja la Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam).  Halafu izari yake Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ilishuka kidogo ikaliwacha wazi paja lake kiasi cha mimi kuweza kuliona”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (371) na Muslim (1365)].

 

Ibn Hazm amesema:  “Imekuwa wazi bayana kwa hili kwamba paja si uchi.  Na kama lingekuwa ni uchi, basi Allaah ‘Azza wa Jalla Asingeliwacha likamfunuka Rasuli Wake aliyetwaharishwa na kulindwa kutokana na watu katika Unabii na Urasuli wake, na wala Asingelimfanya Anas wala mwingine yeyote aweze kuliona.  Na Yeye Allaah Alimlinda uchi wake usionekane tokea utotoni na kabla ya kupewa Utume”.   [Al-Muhallaa (3/272)].

 

Lakini Ibn Hazm anajibiwa akiambiwa kwamba hili lina uwezekaniko wa kuwa izari ilishuka yenyewe, na si kwa kitendo cha yeye kuishusha wala kukusudia kufanya hivyo.  Na hili linathibitishwa na riwaayah ya “Swahiyhayn” isemayo:

 

"فَانْحَسَرَ الإِزَارُ"

 

“Izari ikashuka”. 

 

2-  Hadiyth ya ‘Aaishah: 

 

"أَنَّ النَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم كَانَ جَالِسًا كَاشِفًا عَنْ فَخِذِهِ ، فَاسْتَأْذَنَ أَبُو بَكْرٍ فَأَذِنَ لَهُ وَهُوَ عَلَى حَالِهِ ، ثُمَّ اسْتَأْذَنَ عُمَرُفَأَذِنَ لَهُ وَهُوَ عَلَى حَالِهِ ،‏ ثُمَّ اسْتَأْذَنَ عُثْمَانُ فَجَلَسَ رَسُولُ اللهِ صلى الله عليه وسلم وَسَوَّى ثِيَابَهُ ، فَلَمَّا خَرَجَ ‏ قُلْتُ‏:‏ يَا رَسُولَ اللهِ، دَخَلَ أَبُو بَكْرٍ فَلَمْ تَهَشَّ وَلَمْ تُبَالِهِ، ثُمَّ دَخَلَ عُمَرُ فَلَمْ تَهَشَّ وَلَمْ تُبَالِهِ، ثُمَّ دَخَلَ عُثْمَانُ فَجَلَسْتَ وَسَوَّيْتَ ثِيَابَكَ‏؟‏ قَالَ‏:‏ أَلاَ أَسْتَحِي مِنْ رَجُلٍ تَسْتَحِي مِنْهُ الْمَلاَئِكَةُ‏؟"

 

“Kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa ameketi huku akiwa amelifunua paja lake.  Abu Bakr akapiga hodi, akamruhusu kuingia akiwa hivyo hivyo (akazungumza naye akatoka).  Kisha ‘Umar naye akapiga hodi, akamruhusu kuingia akiwa hivyo hivyo (akazungumza naye akatoka).  Halafu ‘Uthmaan akapiga hodi, na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaketi sawa, akaiweka vizuri nguo yake. Alipoondoka nilimuuliza: Ee Rasuli wa Allaah!   Abu Bakr ameingia, ukabaki ulivyokuwa wala hukujali, kisha ‘Umar akaingia, ukabaki hivyo hivyo, lakini ‘Uthmaan alipoingia, uliketi sawa na kuiweka vizuri nguo yako.  Akasema: “Iwaje nisimwonee haya mtu ambaye Malaika wanamwonea haya?!”  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Muslim (2401)].

 

3-   Jaabir amesema:

 

"احْتَجَمَ النَّبِيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ عَلَى وَرِكِهِ مِنْ وَثْءٍ كَانَ بِهِ"

 

“Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alifanya hijama sehemu ya juu ya paja lake kutokana na vilio la damu lililompata”.  [Hadiyth Dhwa’iyf.  Imekharijiwa na Abu Daawuwd (3763)].

 

Hili linajibiwa:  Kwamba kufunua Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) sehemu ya juu ya paja lake kwa mfanyaji hijama, haionyeshi kwamba si paja si uchi, kwa kuwa alilifunua kutokana na udharura wa kupatiwa tiba, na hili linajuzu kwa makubaliano ya ‘Ulamaa wote.

 

Kauli yenye nguvu:

 

Linaloonekana ni kuwa dalili za Jumhuwr (ambazo ni za maneno ya Rasuli) zinazatitiana zenyewe kwa zenyewe na zinapanda kufikia ngazi ya kuwa hoja thibitishi.  Na  kwa muktadha huu, dalili hizi zinapewa kipaumbele na kutangulizwa kabla ya dalili za kundi la pili, kwa kuwa dalili zao ni matukio ya kibinafsi yaliyomhusu Nabiy pekee na wala hayahusishwi na watu wote.  Na katika kesi kama hii,  kauli ya Rasuli hutangulizwa kabla ya kitendo chake. 

 

Na kama itaulizwa:  Kwa nini mmepita mrengo wa “tarjiyh” (kuzipa uzito dalili kadhaa zinazoonekana kuwa na nguvu zaidi na kuziacha zingine) na wala hamkufanya “jam-‘u” (kuzikusanya dalili zote na kuzifanyia kazi), pamoja na kwamba kuzitumia dalili zote zilizopo ni bora zaidi kuliko kuzitelekeza zingine?

 

Jibu ni:  Kwamba paja, ima liwe uchi au lisiwe, hakuna namna ya tatu, na kwa hivyo imebidi kufanya “tarjiyh”.  Na kwa picha hii, inajulikana kwamba Hadiyth alizozikusanya Ibn Al-Qayyim katika Kitabu cha “Tahdhiyb As-Sunan” na Al-Albaaniy (Rahimahul Laahu) akapendezwa na hilo katika “Al-Irwaa” (1/301), Hadiyth ambazo zinagusia kwamba uchi ni wa aina mbili: Uchi mwepesi na uchi mzito.  Mzito ni tupu mbili; ya mbele na nyuma, na mwepesi ni mapaja mawili.  Na hakuna makinzano baina ya amri ya kuinamisha macho chini kutoyaangalia mapaja mawili kwa kuwa kwake ni uchi, na kati ya kuyaacha wazi kwa kuwa kwake ni uchi mwepesi.  Hili halina mwelekeo .  Na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.

 

 

Share