015-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Mavazi Na Mapambo Na Hukmu Za Kuangalia: Mavazi Na Mapambo Kwa Wanaume:Pambo La Pete Na Mfano Wake

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ اللِّبَاسِ وَالزِّيْنَةِ  وَأَحْكَامُ النَّظَرِ

 

 Kitabu Cha Mavazi Na Mapambo Na Hukmu Za Kuangalia 

 

اللِّبَاسُ وَالزِّيْنَةُ للرِّجَالِ 

Mavazi Na Mapambo Kwa Wanaume 

 

Alhidaaya.com 

 

 

 

015-  Mavazi Na Mapambo Kwa Wanaume:  Pambo La Pete Na Mfano Wake:

 

 

·        Wanaume Hawaruhusiwi Kuvaa Pete Ya Dhahabu

 

1-  Ibn ‘Umar amesema:

 

"أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ اصْطَنَعَ خَاتَمًا مِنْ ذَهَبٍ ، فَكَانَ يَجْعَلُ فَصَّهُ فِي بَاطِنِ كَفِّهِ إِذَا لَبِسَهُ، فَصَنَعَ النَّاسُ خَوَاتِيمَ ، ثُمَّ إِنَّهُ جَلَسَ عَلَى الْمِنْبَرِ فَنَزَعَهُ، فَقَالَ : ‏"‏إِنِّي كُنْتُ أَلْبَسُ هَذَا الْخَاتِمَ وَأَجْعَلُ فَصَّهُ مِنْ دَاخِلٍ ‏"‏‏.‏ فَرَمَى بِهِ ثُمَّ قَالَ ‏"‏وَاللَّهِ لاَ أَلْبَسُهُ أَبَدًا‏"‏‏.‏ فَنَبَذَ النَّاسُ خَوَاتِيمَهُمْ‏"

 

“Kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitengeneza pete ya dhahabu.  Alikuwa anapoivaa, huigeuza stoni yake kuwa ndani ya tumbo la kiganja chake.  Watu walipomwona, nao pia wakatengeneza pete.  Kisha baadaye alikuja akakaa juu ya mimbari, halafu akaitoa kwa nguvu na kusema:  “Hakika mimi nilikuwa navaa pete hii na kuelekeza stoni yake kwa ndani”, kisha akaitupa.  Halafu akasema:  Wa Allaah!  Sitoivaa tena kamwe”.  Na watu nao wakazitupa pete zao”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Muslim (2090)].

 

2-  Abu Hurayrah: 

 

"أَنَّهُ نَهَى عَنْ خَاتَمِ الذَهّبِ"

 

“Kwamba (Rasuli) amekataza pete ya dhahabu”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5863)].

 

3-  Abu Hurayrah: 

 

"أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ رَأَى خَاتَمًا مِنْ ذَهَبٍ فِي يَدِ رَجُلٍ فَنَزَعَهُ فَطَرَحَهُ فَقَالَ: يَعْمِدُ أَحَدُكُمْ إِلَى جَمْرَةٍ مِنْ نَارٍ فَيَجْعَلُهَا فِي يَدِهِ؟ فَقَالُوْا لِلرَّجُلِ بَعْدَمَا ذَهَبَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: خُذْ خَاتَمَكَ فَانْتَفِعْ بِهِ. قَالَ: لَا، وَاللَّهِ لَا آخُذُهُ أَبَدًا وَقَدْ طَرَحَهُ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ"

 

“Kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliona pete ya dhahabu kwenye kidole cha mtu mmoja, akaitoa na kuitupa, kisha akamwambia:  Inakuwaje mmoja wenu anakipania kijinga cha moto akakiweka kwenye mkono wake?!  Watu wakamwambia mtu yule baada ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuondoka:  Ichukue pete yako upate kunufaika nayo.  Akasema:  Hapana.  Naapa kwa Allaah kwamba sitoichukua kamwe madhali Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameitupa”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Muslim (2090)].

 

 4-  Abu Umaamah:  Kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"مَنْ كَانَ يُؤْمِنُ باللهِ وَاليَومِ الآخِرِ فَلَا يَلْبَسْ حَرِيْرًا وَلاَ ذَهَبًا"

 

“Yeyote ambaye anamwamini Allaah na Siku ya Mwisho, basi asivae hariri wala dhahabu”.  [Hadiyth Hasan.  Imekharijiwa na Ahmad (5/261), Al-Haakim (4/212) na At-Twabaraaniy (8/186)].

 

5-  Hadiyth iliyotangulia ya ‘Aliy (Radhwiya Allaah ‘anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"حُرِّمَ لِبَاسُ الْحَرِيرِ وَالذَّهَبِ عَلَى ذُكُورِ أُمَّتِي وَأُحِلَّ لإِنَاثِهِمْ"

 

“Kuvaa hariri na dhahabu kumeharamishwa kwa wanaume wa umati wangu, kumehalalishwa kwa wanawake wao”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Abu Daawuwd (4057), At-Tirmidhiy (1720), An-Nasaaiy (8/160) na Ibn Maajah (3595)].

 

Kutokana na Hadiyth hizi na nyinginezo, tunapata kujua kwamba ni haramu kwa wanaume kuvaa pete ya dhahabu.  Basi je baadhi ya Waislamu watayasikia haya na kuachana na pete za uchumba za dhahabu wanazozivaa kwa kuiga tamaduni za makafiri wanaodai kuwa hilo linaenzi maisha ya ndoa!!

 

·        Hakuna Ubaya Kuvaa Pete Ya Fedha

 

Kuvaa pete ya fedha kunaruhusiwa kwa wanaume.  Anas amesema:

 

"اتَّخَذَ النَّبِيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ خَاتَمًا مِنْ فِضَّةٍ نَقْشُهُ : "مُحَمَّدٌ رَسُولُ اللَّهِ" ، فَكَأَنِّي بِوَبِيصِ -أَوْ بِبَصِيصِ - الْخَاتَمِ فِي إِصْبَعِ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ أَوْ فِي كَفِّهِ"

 

“Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alichongesha pete ya fedha iliyotiwa nakshi isomekayo: “Muhammad Rasuli wa Allaah”, kana kwamba mimi naona mng’ao wa pete katika kidole cha Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) au katika kijanja chake”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5872) na Muslim (2092)].

 

·        Ni Karaha Kwa Mwanaume Kuvaa Pete Kwenye Kidole Chake Cha Kati Au Cha Shahada

 

Abu Burdah:  ‘Aliy (Radhwiya Allaah ‘anhu) amesema:

 

"نَهَانِي رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ أَنْ أَتَخَتَّمَ فِي إِصْبَعِي هَذِهِ أَوْ هَذِهِ قَالَ: فَأَوْمَأَ إِلَى الْوُسْطَى وَالَّتِي تَلِيهَا"

 

“Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alinikataza kuvaa pete katika kidole changu hiki au hiki.  Akaashiria cha kati na cha shahada”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imekharijiwa na Muslim (2078), Abu Daawuwd (4225), At-Tirmidhiy (1786) na An-Nasaaiy (5210)].

 

Na katika tamko jingine:  “Akaashiria kidole chake cha shahada na cha kati”.

 

An-Nawawiy (Rahimahul Laah) amesema:  “Waislamu wote wamekubaliana kwamba ilivyo sunnah, ni mwanaume kuvaa pete kwenye kidole kidogo cha mwisho.  Ama mwanamke, yeye anavaa pete kwenye vidole vyake vyote.   Ni karaha kwa mwanaume kuvaa kwenye kidole chake cha kati na cha shahada kutokana na Hadiyth hii, nayo ni karaha hafifu “tanziyh”.  [Sharhu Muslim cha An-Nawawiy (14/71)].

 

·        Je, Kutumia Dhahabu Kwa Dharura Kunaruhusiwa?

 

"عَنْ عَبْدِ الرَّحْمَنِ بْنِ طَرَفَةَ أَنَّ جَدَّهُ عَرْفَجَةَ بن أَسْعَد قُطِعَ أَنْفُهُ يَوْمَ الْكُلَابِ ، فَاتَّخَذَ أَنْفًا مِنْ وَرِقٍ فَأَنْتَنَ عَلَيْهِ ، فَأَمَرَهُ النَّبِيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ أَنْ يَتَّخِذَ أَنْفًا مِنْ ذَهَبٍ"

 

Toka kwa ‘Abdurrahmaan bin Twarafah toka kwa babu yake ‘Arfajah bin As-’ad:  “Kwamba alikatwa pua katika vita vya Al-Kulaab (enzi ya ujahili).  Akatengeneza pua ya silva, lakini ilimwozea.  Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwamuru atengeneze pua ya dhahabu”.  [Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh.  Imekharijiwa na Abu Daawuwd, At-Tirmidhiy na An-Nasaaiy (4/164)].

 

Al-Khattwaabiy amesema:  “Hadiyth hii inatufahamisha kwamba inaruhusiwa kutumia dhahabu kidogo kwa wanaume kutokana na dharura kama kukazia meno na mfano wa hayo”.  [Tuhfat Al-Ahwadhiy (11/198)].

Na hii ni kauli ya ’Ulamaa wengi. 

 

Ninasema:  “Ama kwa jambo lisilo la dharura, uharamu utabakia pale pale kwa wanaume.  Hairuhusiwi kuweka vifungo vya dhahabu kwenye nguo au kuvaa saa ya dhahabu, kwa kuwa hakuna dharura kwa mambo kama haya.  Kufanya hivyo bila dharura, kunahesabiwa kuwa ni israfu, kibri, na kujiona.  Allaah Ndiye Mjuzi zaidi”.

 

Na haya yote ni kwa upande wa wanaume.  Ama kwa wanawake, dhahabu kwao kiasili inaruhusiwa ijapokuwa bila dharura kama ilivyotangulia.

 

Share