021-Al-Anbiyaa: Utangulizi Wa Suwrah

 

021-Al-Anbiyaa: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

Imeteremka: Makkah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.

 

Idadi Za Aayah: 112

 

Jina La Suwrah: Al-Anbiyaa

 

Suwrah imeitwa Al-Anbiyaa (Manabii), na inayodalilisha ni kutajwa katika Hadiyth iliyonukuliwa chini katika Fadhila za Suwrah. Na pia kutokana na kutajwa kwa Manabii mbalimbali katika Suwrah.

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Kuthibitisha Risala ya Allaah (سبحانه وتعالى) na kubainisha kuwa Manabii wote walikuwa na lengo moja, na ndio lengo la Allaah kwao. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Kubainisha haqq (ukweli) unavyoshinda baatwil, kwa kutaja mifano ya Rusuli na jinsi walivyowashinda watu wao. Na kuthibitisha kwamba Manabii na Rusuli wote walilingania Dini moja ya asili yake ambayo ni Tawhiyd ya Allaah, na kusimamisha dalili zake, kama kubainisha kwamba, ingelikuwa mbinguni na ardhini kulikuwa na waabudiwa wasiokuwa Allaah (سبحانه وتعالى) wenye kuyaendesha mambo yake, ungeliharibika mpango wa mbingu na ardhi.

 

3-Maonyo na kuthibitisha matokeo ya Siku ya Qiyaamah na kurejea viumbe kwa Allaah, na kuzibainisha dalili zake, kama kutokea baadhi ya alama zake kubwa, kama Yaajuwj na Maajuwj.  

 

4-Kubainisha yale waliyokutana nayo Rusuli katika njia ya daawah (ulinganiaji), na kuwakumbusha makafiri yale yaliyowasibu nyumati za nyuma kwa sababu ya kuwakanusha Rusuli, na kwamba ahadi ya Allaah (سبحانه وتعالى) kuwaadhibu makafiri hao haibadiliki.

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

1-Suwrah imefunguliwa kwa kuwaonya watu kwa kuwathibitishia kwamba Qiyaamah kiko karibu. 

 

2-Imetaja baadhi ya shubha ambazo walizizusha washirikina dhidi ya Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) katika kubalighisha Risala ya Allaah (سبحانه وتعالى).

 

3-Suwrah imemliwaza Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) juu ya yale aliyokuwa akiambiwa na washirikina.

 

4-Suwrah imethibitisha kwamba Rusuli wote walitumwa kwa ajili ya kulingania Tawhiyd ya Allaah; Laa ilaaha illa-Allaah.

 

5-Suwrah imetaja usingiziaji wa washirikina kwamba Allaah (سبحانه وتعالى) Ana mwana ilhali Yeye Ametukuka na hilo. Basi imewathibitishia jazaa yao ya Jahannam kwa usingiziaji huu wa kuvuka mipaka!

 

6-Suwrah inawakumbusha watu juu ya waliyoyapata nyumati zilizopita baada ya kuwakadhibisha Rusuli wao.

 

7-Suwrah imethibitisha Neema za Allaah (سبحانه وتعالى), Ishara na Dalili Zake za Tawhiyd kwamba: Yeye Ndiye Aliyezibandua mbingu na ardhi baada ya kuwa ziliambatana. Na Akajaalia uhai wa kila kitu kutokana na maji. Na Akajaalia milima kuwa thabiti isiyumbe yumbe. Akajaalia katika ardhi njia pana za kupitika ili watu wapate kujua waendako. Na Akajaalia mbingu kuwa ni paa lililohifadhiwa. Na kwamba Ameumba usiku na mchana. Na Ameumba jua na mwezi. Na kwamba Yeye Allaah (سبحانه وتعالى) Ndiye Mwenye kuhuisha na kufisha.  

 

8-Suwrah imetaja khabari za baadhi ya Manabii ambao ni Muwsaa, Haaruwn, Ibraahiym, Is-haaq, Ya’quwb, Luutw, Nuwh, Daawuwd, Sulaymaan, Ayyuwb, Ismaa’iyl, Idriys, Dhul-Kifl, Yuwnus (Dhan-Nuwn) na Zakariyyaa (عليهم السلام).

  

9-Baada ya kutajwa Manabii Suwrah ikafuatilia kumtaja kwa kumsifia Maryam mama wa Nabiy ‘Iysaa (عليه السّلام).

 

10-Wametajwa Yaajuwj na Maajuwj kama ni miongoni mwa alama kubwa za Qiyaamah.

 

11-Imetahadharisha kuwa washirikina na waabudiwa wao wote wataingizwa moto wa Jahannam wadumu humo milele.

 

12-Kisha Suwrah imewabashiria Waja wema wa Allaah (سبحانه وتعالى) kwamba wao wataepushwa na moto, na wala hawatosikia mvumo wake, wala hautowahuzunisha mfazaiko mkubwa, bali watadumu katika Jannah ambamo humo watapata  yale wanayotamani nafsi zao na kubashiriwa mema na Malaika.

 

13-Suwrah imekhitimishwa kwa kutajwa kwamba Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) ametumwa kuwa ni rehma kwa walimwengu wote na ikathibitisha tena Tawhiyd ya Allaah kwamba Yeye Allaah (سبحانه وتعالى) Pekee Anayestahiki kuabudiwa. Na maonyo kwa washirikina wakiendelea kukengeuka na kwamba Allaah (سبحانه وتعالى) Ndiye Mwenye Kuombwa msaada kwa yale wanayomvumishia.

 

Fadhila Za Suwrah:

 

Suwrah Al-Anbiyaa ni miongoni mwa Suwrah zilizotangulia kuteremshwa, na Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akazitaja kuwa ni pato lake la mwanzo:

 

حَدَّثَنَا آدَمُ، حَدَّثَنَا شُعْبَةُ، عَنْ أَبِي إِسْحَاقَ، قَالَ سَمِعْتُ عَبْدَ الرَّحْمَنِ بْنَ يَزِيدَ، سَمِعْتُ ابْنَ مَسْعُودٍ، يَقُولُ فِي بَنِي إِسْرَائِيلَ وَالْكَهْفِ وَمَرْيَمَ وَطَهَ وَالأَنْبِيَاءِ إِنَّهُنَّ مِنَ الْعِتَاقِ الأُوَلِ وَهُنَّ مِنْ تِلاَدِي‏.‏

 

Amesimulia ‘Abdur-Rahmaan bin Yaziyd (رضي الله عنه): Nimemsikia  ‘Abdullaah bin Mas‘uwd (رضي الله عنه) akisema: Suwrah Bani Israaiyl, Al-Kahf, Maryam, Twaahaa na Al-Anbiyaa ndio miongoni mwa pato langu la kwanza na mali yangu kongwe, na (hakika ni) ndio mali yangu kongwe.” [Al-Bukhaariy]

 

 

 

Share