022-Al-Hajj:Utangulizi Wa Suwrah

 

022-Al-Hajj: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

 

 

Imeteremka: Makkah au Madiynah kwa kuwa ‘Ulamaa wamekhitilafiana kuteremshwa kwake. Wamesema kuwa, baadhi ya Aayah zimeteremka Makkah, na baadhi ya Aayah zimeteremka Madiynah. 

 

Idadi Za Aayah: 78

 

Jina La Suwrah: Al-Hajj

 

Suwrah imeitwa Al-Hajj, na inayodalilisha ni kutajwa kuhusu Hajj na taratibu zake kuanzia Aayah namba (25) hadi (37).

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Kumuadhimisha Allaah (سبحانه وتعالى), na kutukuza Ishara Zake. Na watu kuzikubali Amri zake. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Kuthibitisha kufufuliwa na hali za watu Siku ya Qiyaamah na jazaa njema za Waumini na jazaa mbaya za makafiri.

3-Kuibainisha Tawhiyd kwa Dalili Zake, na kukanusha ushirikina na kuradd mijadala yao.

 

4-Kubainisha Maajabu ya Uwezo Allaah (سبحانه وتعالى) ardhini.

 

5-Kubainisha manufaa ya Hajj ya duniani na Aakhirah, na kubainisha umuhimu wa kutukuza Ishara na Vitu Vitukufu vya Allaah (سبحانه وتعالى).

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

1-Suwrah imefunguliwa kwa kuamrisha kumcha Allaah (سبحانه وتعالى), na maelezo kuhusu uzito wa Siku ya Qiyaamah kama zilzala (tetemeko la ardhi) na kiwewe cha watu kitakavyokuwa Siku hiyo.

 

2-Imethibitishwa kufufuliwa kwa watu, kwa hoja na dalili ya uumbaji wa mwanaadamu, kuanzia udongo hadi tone la manii, na daraja za kuumbwa kwake tumboni hadi kuzaliwa kwake, na kuendelea hali yake hadi kufariki. Kisha ikapiga mfano wa ardhi kame inayomiminiwa maji ikahuika na kutoa mazao. Ikaendelea kuthibitisha kuwa Qiyaamah kitatokea tu na kwamba Allaah (سبحانه وتعالى) Atawafufua watu kutoka makaburini mwao.

 

3-Imetajwa mijadala ya washirikina na ibaada za wanafiki.

 

4-Imeabainisha Hukmu ya Allaah kati ya watu na dini zao na kwamba Allaah (سبحانه وتعالى) Atahukumu baina yao Siku ya Qiyaamah.

 

5-Imetajwa kuwa kila kitu hapa ulimwenguni kinamsujudia Allaah (سبحانه وتعالى) na wale wanaokana kumsujudia watastahiki adhabu.

 

6-Imebainishwa uwiano kati ya wawili waliogombana kwa ajili ya Rabb wao; Waumini na makafiri, pamoja na kubainisha mwisho wa kila mmoja kati yao.

 

7-Suwrah imetoa baadhi ya mwongozo wa Manaasik (taratibu na ibaada) ya Hajj, na manufaa yake ya duniani na Aakhirah, na amri ya kuwazuia washirikina wasiingie Masjidul-Haraam.

 

8-Wametahadharishwa watu na shirki na washirikina.

 

9-Imetolewa idhini kwa Waislamu ya kupigana Jihaad na kwamba Allaah (سبحانه وتعالى) Atawanusuru Waja Wake wanaonusuru Dini Yake.

 

10-Allaah (سبحانه وتعالى) Amemliwaza Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) kwa yale yaliyompata ya kukadhibishwa na kupingwa na watu wake, kwa kumkumbusha yaliyowapata nyumati za nyuma waliokadhibisha na kuwapinga Rusuli wao. 

 

11-Wamebashiriwa rizki njema na Jannah wale waliohajiri na kufanya Jihaad.

 

12-Imethibitishwa Tawhiyd ya Allaah na Uwezo Wake wa: (i) Kuleta usiku na mchana (ii) Kuteremsha maji ardhini (iii) Kutiisha ardhi na bahari (iv) Kuzuia mbingu zisianguke. (v) Kuhuisha na kufisha. Kwa Neema zote hizo za Allaah na Uwezo Wake (سبحانه وتعالى), kuanzia Aayah (58) hadi (65), Aayah zikamalizia kwa kutajwa Majina Yake Mazuri mbalimbali na Sifa za Allaah (سبحانه وتعالى).  

 

13-Umepigwa mfano wa kuthitisha Tawhiyd ya Allaah ya Ar-Rubuwbiyyah (Uola, Uumbaji n.k), kwamba wanaoabudiwa badala ya Allaah (سبحانه وتعالى), hawawezi kuumba nzi hata kama wote watajumuika kutaka kufanya! Na kwamba mfano wa hao wanaoabudiwa (walioshirikishwa) na wanaoabudu (washirikina) wote ni dhaifu! Na hakika Hawakumkadiria Allaah kama inavyostahiki kumkadiria.

 

14-Suwrah imekhitimishwa kwa amrisho la kufanya Jihaad, na kusimamisha Swalaah na kutoa Zakaa na kushikamana pamoja kwa ajili ya Allaah.   

 

Fadhila Za Suwrah:

 

Suwrah hii ya Al-Hajj ni Suwrah pekee yenye Sajdatut-Tilaawah (Sijdah ya kisomo) mbili, ingawa Sijda ya pili wamekhitilafiana ‘Ulamaa kuhusu kuwajibika kwake.

 

 

Share