023-Al-Muuminuwn: Utangulizi Wa Suwrah

 

023-Al-Muuminuwn: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

Imeteremka: Makkah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.

 

Idadi Za Aayah: 118

 

Jina La Suwrah: Al-Muuminuwn

 

Suwrah imeitwa Al-Muuminuwn (Waumini), na inayodalilisha ni kutajwa katika Hadiyth iliyonukuliwa chini katika Faida. Na pia kutokana na neno hili kutajwa katika Aayah ya kwanza.

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Kubainisha kufaulu kwa Waumini, na hasara kwa makafiri. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Kuthibitisha kufaulu kwa Waumini ambao sifa zao zimetajwa, na kwamba wao ndio wenye kufaulu duniani na Aakhirah.

 

3-Kueleza jinsi mwanaadam alivyoumbwa, na kubainisha hatua za maisha ya mwanaadam ambazo anazipitia hadi anaishia katika kifo kama hali ya wanaadamu wote.

 

4-Kuthibitisha Tawhiyd ya Allaah na kubatilisha ushirikina.

 

5-Kutajwa Neema nyingi za Allaah (سبحانه وتعالى) juu ya viumbe Vyake na kudhihirisha Uadhimu na Miujiza Yake.

 

6-Kuthibitisha Unabiy wa Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) na kuwaraddi makafiri wanaopinga.

 

7-Tahadharisho la uchochezi wa shaytwaan na mwongozo wa kujikinga naye.

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

1-Suwrah imefunguliwa kwa kutajwa sifa za Waumini na ibaada zao, na waliyoandaliwa na Allaah (سبحانه وتعالى) ya Jannatul-Firdaws.

 

2-Imetajwa hatua za maumbile ya mwanaadam, zinazothibitisha uwezekano wa kufufuliwa kwake.

 

3-Imebainishwa baadhi ya Neema kadhaa za Allaah (سبحانه وتعالى) na baadhi ya mambo yanayoonyesha Uwezo wa Allaah (سبحانه وتعالى) hapa ulimwenguni.

 

4-Imetajwa sehemu fulani ya visa vya baadhi ya Rusuli, na misimamo yao pamoja na watu wao, na mwisho wao ulikuwaje.

 

5-Suwrah imewaelekeza Rusuli wale rizki za halali, na wadumishe kutenda mema, na kuoneysha kuwa Rusuli wote dini yao ilikuwa moja.

 

6-Imebainishwa misimamo ya washirikina dhidi ya daawah ya Kiislamu, na mafikio yao Siku ya Qiyaamah.

 

7-Imetajwa tena baadhi ya Neema za Allaah (سبحانه وتعالى) kwa Waja Wake kama kusikia, kuona na nyoyo za kutafakari.

 

8-Imebainishwa dalili zinazoonyesha kuwa Allaah (سبحانه وتعالى) ni Mmoja tu, na Muweza wa kila kitu kama kuhuisha na kufisha, na kuleta mabadiliko ya usiku na mchana.

 

9-Imetambulishwa kuwa washirikina waliamini Tawhiyd ya Ar-Rubuwbiyyah (Kumpwekesha Allaah katika Uola; yaani Yeye ni Rabb Anapaswa Kupwekeshwa katika Uumbaji, Ufalme, Uendeshaji, Utoaji Rizki, Uhuishaji, Ufishaji). Lakini walipinga Tawhiyd ya Al-Uluwhiyyah (Kumpwekesha Allaah (سبحانه وتعالى) katika ibaada). Basi Allaah (سبحانه وتعالى) Amekanusha kabisa waliyomshirikisha kwa kuthibitisha kwamba Hakujichukulia mwana wala Hana mshirika.

 

10-Imetolewa mwongozo kwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) juu ya kupuuza miamala mibaya ya washirikina na aizuie kwa kuwarudishia yaliyo bora, na ajilinde na shaytwaan.

 

11-Imetajwa majuto ya kafiri na mwenye kuasi, pindi atakapokuwa anatolewa roho, akitamani kurudi duniani atende mema, lakini hilo haliwezekani kabisa kwani baada ya hapo, kuna al-barzakh ambayo ni kipindi baina ya mtu kufariki hadi kufufuliwa.

 

12-Imetajwa hali ya washirikina na makafiri itakapokuwa Siku ya Qiyaamah, ya moto kuwababua nyuso zao, na sura zao kubadilika kabisa kuwa zina hali ya kutisha! Pia majuto yao ya kuwafanyia dhihaka Waumini walipokuwa duniani.

 

13-Suwrah imekhitimishwa kwa kutajwa lengo la kuumbwa binaadam, na Allaah (سبحانه وتعالى) Anajitukuza kwa Uluwa. Ikatajwa pia onyo la kumuomba asiyekuwa Allaah. Kisha amri kwa Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) (na Waumini) kuomba Rehma ya Allaah (سبحانه وتعالى) na Maghfirah. 

 

Faida:

 

عَنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ السَّائِبِ، قَالَ صَلَّى بِنَا رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم الصُّبْحَ بِمَكَّةَ فَاسْتَفْتَحَ سُورَةَ الْمُؤْمِنِينَ حَتَّى إِذَا جَاءَ ذِكْرُ مُوسَى وَهَارُونَ - أَوْ ذِكْرُ مُوسَى وَعِيسَى ابْنُ عَبَّادٍ يَشُكُّ أَوِ اخْتَلَفُوا - أَخَذَتْ رَسُولَ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم سُعْلَةٌ فَحَذَفَ فَرَكَعَ وَعَبْدُ اللَّهِ بْنُ السَّائِبِ حَاضِرٌ لِذَلِكَ ‏.‏

 Amesimulia ‘Abdullaah Bin As-Saaib (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alituswalisha Swalaah ya Asubuhi Makkah akaanza kwa Suwrah Al-Muuminuwn (23), mpaka alipofikia kutajwa kwa Muwsaa na Haaruwn  (Aayah 45) au kutajwa kwa Iysaa (Aayah 50). Ibn ‘Abbaad alitilia shaka au wasimulizi wengine wamekhitilafiana baina yao kwa neno hili la kikohozi kumshika Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akaacha (kisomo) akarukuu. ‘Abdullaah Bin Saaib alikuweko kushuhudia (tukio) hilo. [Sunan Abiy Daawuwd na riwaaya kama hiyo ya Muslim]

 

 

 

Share