033-Al-Ahzaab: Utangulizi Wa Suwrah

 

033-Al-Ahzaab: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

Imeteremka: Madiynah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.

 

Idadi Za Aayah: 73

 

Jina La Suwrah: Al-Ahzaab

 

Suwrah imeitwa Al-Ahzaab (Makundi Yaliyoshirikiana), na inayodalilisha ni kutajwa katika Hadiyth iliyonukuliwa katika Faida, na pia kutajwa katika Aayah namba (20) makundi ya washirikina waliokusanyika kuzunguka mji wa Madiynah kutaka kuwapiga vita Waislamu. 

 

Na pia Suwrah imeitwa Al-Khandaq (Shimo) kutokana na uchimbaji wa Khandaq kuizunguka Madiynah kwa ajili ya kuwazuia washirikina kutokuingia mjini kuwapiga vita.

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Ubainisho juu ya Allaah (سبحانه وتعالى) kushughulikia jambo la Nabiy Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) na kumhami yeye pamoja na watu wa nyumbani mwake. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Mahimizo juu ya kumuelekea Muumba, bila kuangalia nafasi ya Viumbe na heshima zao.

 

3-Kubainisha Ulinzi wa Allaah kwa Nabiy Wake (صلى الله عليه وآله وسلم). 

 

4-Kuwekwa wazi hukmu nyingi za Sharia na adabu za kijamii, kwa mujibu wa Uislamu.

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

1-Suwrah imefunguliwa kwa wito kwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) juu ya kumcha Allaah na kutowatii makafiri na wanafiki.

 

2-Imeharamishwa baadhi ya mila na desturi ambazo zilikuwa zimetangaa kwenye jamii yao, kama vile dhwihaar (aina ya talaka ambapo mume anamwambia mkewe: “Wewe kwangu ni kama mgongo wa mama yangu” na hivyo kumfanya kuwa ni haraam kwake kujamiana naye), na at-tabanniy (mtoto wa kumlea ukamuunganisha na nasabu yako).

 

3-Imetajwa baadhi ya hukumu za Sharia, kama vile: kumtii Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم), na pia imeelezewa kwamba Wake zake ni Mama wa Waumini, na kubatilisha watu kurithiana kwa njia ya undugu (wa kuunganisha).

 

4-Imetajwa matukio ya Vita vya Ahzaab na pia kuhusu Bani Quraydhwah, na matokeo ya mwisho wa vita.

 

5-Imetajwa kuhusu kufadhilishwa wake wa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم), na kubainisha ubora wao, na kutolewa mwongozo kwao.

 

6-Imetajwa sifa kadhaa za Waumini ambazo mwishowe wameahidiwa maghfirah na ujira adhimu.

 

7-Imetajwa kisa cha kuozeshwa kwa Zaynab Bint Jahsh (رضيَ الله عنها), baada ya kuachwa na Zayd Bin Haarithah (رضي الله عنه), na hekima yake ni kubatilisha athari za at-tabanniy (watoto wa kuwalea wasiwe sawa na watoto wa kuwazaa).

 

8-Imethibitishwa kuwa Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) hakubakia kuwa ni baba wa yeyote na kuthibitishwa kuwa yeye ni Nabiy wa mwisho.

 

9-Amri ya kukithirisha kumdhukuru Allaah (سبحانه وتعالى) na kumsabbih na fadhila zake.

 

10-Imebainishwa hukmu ya talaka kwa mke asiye ingiliwa.

 

11-Amri ya kumswalia Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم).

 

12-Imetajwa laana ya Allaah kwa wanaomuudhi Allaah na Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم), na wanaowaudhi Waumini, na tahadharisho kuwa wasipokoma hatima yao ni kama ilivyo Desturi ya Allaah.

 

13-Amri ya vazi la hijaab kwa Waumini wanawake.

 

14-Imetajwa majuto ya watu Siku ya Qiyaamah kuwafuata wakubwa wao waliowapoteza duniani.

 

15-Suwrah imekhitimishwa kwa kubainishwa mwanaadam kukubali kuibeba amana.

 

Faida:

 

عَنِ الزُّهْرِيِّ، قَالَ أَخْبَرَنِي خَارِجَةُ بْنُ زَيْدِ بْنِ ثَابِتٍ، أَنَّ زَيْدَ بْنَ ثَابِتٍ، قَالَ لَمَّا نَسَخْنَا الصُّحُفَ فِي الْمَصَاحِفِ فَقَدْتُ آيَةً مِنْ سُورَةِ الأَحْزَابِ، كُنْتُ أَسْمَعُ رَسُولَ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم يَقْرَؤُهَا، لَمْ أَجِدْهَا مَعَ أَحَدٍ إِلاَّ مَعَ خُزَيْمَةَ الأَنْصَارِيِّ، الَّذِي جَعَلَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم شَهَادَتَهُ شَهَادَةَ رَجُلَيْنِ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ رِجَالٌ صَدَقُوا مَا عَاهَدُوا اللَّهَ عَلَيْهِ‏

Amesimulia Zayd Bin Thaabit (رضي الله عنه) amesema: Tulipokuwa tunakusanya nyaraka katika Mswahafu, niliikosa Aayah katika Suwrah Al-Ahzaab niliyokuwa nikimsikia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akiisoma. Sikuipata Aayah hiyo kwa yeyote isipokuwa kwa Khuzaymah Al-Answaariy ambaye Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alijaalia kuwa ushahidi wake ni sawa na ushahidi wa watu wawili. (Na Aayah yenyewe ni):

مِّنَ الْمُؤْمِنِينَ رِجَالٌ صَدَقُوا مَا عَاهَدُوا اللَّـهَ عَلَيْهِ ۖ

“Miongoni mwa Waumini, wapo wanaume waliotimiza kikweli waliyoahidiana na Allaah.” [Al-Ahzaab (33:23) – Hadiyth ameipokea Imaam Al-Bukhaariy]

 

 

 

Share