046-Al-Ahqaaf: Utangulizi Wa Suwrah

 

046-Al-Ahqaaf: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

Imeteremka: Makkah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.

 

Idadi Za Aayah: 35

 

Jina La Suwrah: Al-Ahqaaf

 

Suwrah imeitwa Al-Ahqaaf (Ardhi ya machuguu ya mchanga), na inayodalilisha ni kutajwa katika Aayah namba (21).  

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Kubainisha kuwa wanaadam wanahitaji zaidi Risala ya Allaah (سبحانه وتعالى) na kuwaonya wanaopuuza. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Kuwalingania watu kusahihisha imaan zao kwa kumpwekesha Allaah (سبحانه وتعالى) na kumwamini Rasuli Wake Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) huku wakiamini Risala ya Rusuli waliotangulia, na kuamini Siku ya Mwisho na Aliyoyatayarisha Allaah (سبحانه وتعالى) kwa malipo ya Waumini na adhabu kwa makafiri.

 

3-Kuthibitisha Tawhiyd ya Allaah na Uwezo Wake wa kuumba mbingu na ardhi na vilivyomo baina yake bila ya kushikwa na uchovu. Na kwamba ana Uwezo wa kuwahuisha watu baada ya kufa na kuhesabiwa.

 

4-Radd kwa madai ya makafiri na washirikina kuhusu Qur-aan kuwa sio sihri bali Qur-aan inatoka kwa Allaah (سبحانه وتعالى), na kwamba ni Risala ya wanaadam na majini.

 

5-Kuwasifu Waumini kwa imaan zao juu ya Qur-aan Tukufu, huku ukibainisha baadhi ya sifa za Waumini na sifa zao zilizo kinyume na sifa za makafiri.   

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

1-Suwrah imefunguliwa kwa herufi zinazojulikana kama الحروف المقطعة  (Al-Huruwf Al-Muqatw-twa’ah), ambazo hakuna ajuaye maana zake isipokuwa Allaah (سبحانه وتعالى). Rejea Al-Baqarah (2:1). Kisha imetukuzwa Qur-aan na kuthibitishwa kwamba ni Uteremsho kutoka kwa Allaah (سبحانه وتعالى).

 

2-Imethibitishwa Tawhiyd ya Allaah ya Ar-Rubuwbiyyah (Uola, Uumbaji) na kubainishwa Uwezo Wake (سبحانه وتعالى) wa kuumba mbingu na ardhi. Kisha imewaradd washirikina na kuwataka walete vile walivyoumba waabudiwa wao, au walete dalili ya ushirikiano wao na Allaah (سبحانه وتعالى) mbinguni, ikiwa ni wakweli. Kisha Allaah (سبحانه وتعالى) Akawatolea hoja kwamba wanaoombwa pasi Naye, hawawaitikii duaa zao wala hawatambui maombi yao! Kisha Siku ya Qiyaamah watakapokusanywa wote, waabudiwa wao watakuwa maadui wao, na watakanusha ibaada zao!

 

3-Imetajwa ada za makafiri kupachika sifa ovu Qur-aan kama sihri (uchawi), na pia kumzushia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) kwamba ameitunga Qur-aan, ilhali kuna ushahidi wa wazi wa Allaah (سبحانه وتعالى) kwamba ni Wahy kutoka Kwake.

 

4-Imebainisha mwisho mwema kwa Waumini wa kuingizwa Jannah na kudumu milele kwa sababu ya kumwamini Rabb wao na wakathibitika katika Dini.

 

5-Imetolewa wasia wa kuwatendea ihsaan wazazi wawili, na mwanaadam kukumbushwa shida na tabu anazozipata mama za kubeba mimba mpaka kujifungua na mpaka kumaliza kunyonyesha mwana. Kisha wenye kutii hayo, wamebashiriwa kupokelewa amali zao na kuingizwa Jannah, pindi wakiomba duaa na kushukuru Neema za Allaah na kutubia Kwake wanapofikia umri mkubwa.

 

6-Kisha imebainishwa mwisho mbaya kwa makafiri wa kuingiziwa motoni na kuadhibiwa, kwa kukanusha kwao Risala ya haki, na kuifanyia istihzai kwa kudai kuwa ni hekaya za watu wa kale.

 

7-Imetajwa sehemu ya kisa cha Nabiy Huwd (عليه السّلام) na kaumu yake ambao ni kina ‘Aad, wakaazi wa Ahqaaf (ardhi ya machuguu ya mchanga), na ukanushaji wao wa Risala na Rasuli wao, na kuhimiza kwao adhabu. Basi wakateremshiwa wingu lilotanda upeoni mwao likielekea mabonde yao, wakidhani kuwa ni wingu la mvua ya kawaida, kumbe ulikuwa ni upepo wa dhoruba, wenye adhabu kali uliowaangamiza!

 

8-Ameliwazwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kwa kumkumbusha kuwa, kundi la majini lilihudhuria kusikiliza Qur-aan kwa makini, wakaiamini, na wakamwamini Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم), kisha  wakawaendea majini wenzao kuwalingania, wakubali Ujumbe wa Allaah (سبحانه وتعالى) kuwa ni wa haki na kuwahamasisha kwamba wataghufuriwa madhambi yao, na wataepushwa na adhabu. Na pindi wasipoitikia Risala hiyo, basi hawataweza kukwepa adhabu ya Allaah.

   

9-Imethibitishwa Tawhiyd ya Allaah ya Ar-Rubuwbiyyah (Uola, Uumbaji n.k), na Uwezo wa Allaah (سبحانه وتعالى) wa kufufua wafu. Kisha ikatajwa hali ya makafiri watakapohudhurishwa motoni na kuonjeshwa adhabu kwa kufru zao.

 

10-Suwrah imekhitimishwa kwa kuamrishwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) avute subira, kama walivyovuta subira Rusuli wenzake waliokuwa na azimio madhubuti, na kwamba asitake kuwaharakizia makafiri adhabu, kwani itakapofika Qiyaamah, watahisi kuwa kama waliishi saa moja tu duniani! Kisha itahakiki maangamizo yao.

 

Faida:

 

Al-Ahqaaf ni ardhi ya machuguu ya mchanga ambayo ni Yemen, nayo ni ya kina ‘Aad kaumu ya Huwd (عليه السّلام).

 

 

Share