047-Muhammad: Utangulizi Wa Suwrah

 

047-Muhammad: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

Imeteremka: Madiynah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.

 

Idadi Za Aayah: 38

 

Jina La Suwrah:  Muhammad

 

Suwrah imeitwa Muhammad (Jina la Nabiy صلى الله عليه وآله وسلم), na inayodalilisha ni Jina lake katika Aayah namba (2).

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Kuwahimiza Waumini juu ya suala la kupigana vita, kwa kuwatia nguvu, na kwa kuwadhoofisha makafiri. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Kuwatangazia watu kwamba Allaah (سبحانه وتعالى) Anabatilisha matendo ya makafiri kwa sababu wanang'ang'ania kufuata batili, wanapinga wito wa haqq (ukweli) na kuwaweka mbali na Dini ya Allaah.  

 

3-Kuvutia kwenye Jihaad katika Njia ya Allaah, na kuunga mkono haqq (ukweli) na kushikamana na yale ambayo Allaah (سبحانه وتعالى) Ameyateremsha kwa Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) na hili ndilo linalowahakikishia Waumini ushindi dhidi ya maadui zao.

 

4-Kubashiriwa Waumini kuwa wao ni vipenzi vya Allaah na kubashiriwa Jannah na neema zake na makafiri kubainishwa adhabu zao motoni.

 

5-Kudhihirisha hali za wanafiki na sifa zao, sura zao na Waislamu kutahadharishwa nao.

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

1-Suwrah imefunguliwa kwa kubainisha mwisho mbaya wa makafiri, na mwisho mzuri wa Waumini walioamini aliyoteremshiwa Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم).

 

2-Imewahimiza Waumini kufanya ugumu katika kupambana na makafiri, na kuwachukua mateka.

 

3-Waumini wameahidiwa ushindi pale watakapomnusuru Allaah (سبحانه وتعالى) na Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم), na kuwabashiria Jannah na neema ambazo wameshajulishwa nazo. Kisha makafiri wakatishiwa maangamizi na kuharibikiwa amali zao, na kuwakemea juu kuchukia kwao waliyoteremshiwa. Basi Allaah (سبحانه وتعالى) ni Mlinzi wa Waumini na makafiri hawana yeyote wa kuwalinda.

 

4-Waumini wamebashiriwa Jannah na neema zake humo za mabustani yenye kupitia mito chini yake, na mito yenye vinywaji aina nne safi venye kuburudisha. Juu ya hivyo watapata matunda na maghfirah. Basi hao si sawa na watu wa motoni ambao wao, vinywaji vyao ni maji yachemkayo yatakayowakatakata machango yao!

 

5-Imetajwa baadhi ya misimamo ya wanafiki kwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) na da’wah yake na kutaja baadhi ya sifa zao mbaya, kama vile udanganyifu wao na adabu mbaya, na uwoga wao pindi wanapoitwa katika vita vya Jihaad.

 

6-Imebainishwa kuwa unafiki wa wanafiki ulikua kwa sababu ya shaytwaan kuwatawala, na kuwatisha kwa mafikio mabaya katika maisha yao na baada ya mauti yao.

 

7-Imetaja vitisho kwa makafiri ya kuharibika matendo yao, na kwamba wana maradhi nyoyoni mwao na Allaah (سبحانه وتعالى) Atafichua chuki na niyya zao ovu.

 

8-Waumini wameamrishwa kumtii Allaah na Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) na kuwakataza kukata tamaa, na kuwabashiria nusra na ushindi. Na wameamrishwa wasinyong’onyee kutaka suluhu na makafiri, kwani Allaah Yu pamoja nao.

 

9-Imetanabahishwa kuwa uhai wa dunia ni mchezo na pumbao tu lakini kwa Allaah ndiko kwenye ujira mzuri.

 

10-Suwrah imekhitimishwa kwa kuwatahadharisha Waumini kutokana na ubakhili, na kuwalingania katika kutoa kwenye njia ya Allaah, na pindi wakikengeuka, basi Allaah (سبحانه وتعالى) ni Mkwasi na Mweza wa kuwabadilisha watu bora kuliko wao.    

 

 

 

 

 

Share