057-Al-Hadiyd: Utangulizi Wa Suwrah

 

057-Al-Hadiyd: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

Imeteremka: Makkah kwa itifaki ya baadhi ya ‘Ulamaa

 

Idadi Za Aayah: 29

 

Jina La Suwrah: Al-Hadiyd

 

Suwrah imeitwa Al-Hadiyd (Chuma), na inayodalilisha ni kutajwa kwake katika Aayah namba (25).

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Kukuza imaan kwenye nafsi, na kutoa katika Njia ya Allaah. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Ishara zinazodalilisha Qudra na Uwezo wa Allaah (سبحانه وتعالى) na Sifa Zake Jalili (Tukufu). 

 

2-Wito kwa Waumini kushikamana na mafundisho ya Dini yao.

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

1-Suwrah imefunguliwa kwa kumtukuza Allaah (سبحانه وتعالى) kwamba, vyote vilivyopo mbinguni na aridhini vinamsabbih Yeye, Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye Hikmah wa yote.

 

2-Zimetajwa Sifa Zake Allaah (سبحانه وتعالى) nyenginezo Kamilifu, na Uwezo wa kila kitu katika Ufalme Wake na kuenea Ilimu Yake.

 

3-Waumini wamehimizwa kuthibitika katika imaan na kutoa mali zao katika Njia ya Allaah, na Ahadi ya Allaah (سبحانه وتعالى) Kuwalipa maradufu ya wanayotoa.

 

4-Imebainishwa mwisho mwema wa Waumini wa kiume na wa kike Siku ya Qiyaamah, na Nuru itakayowaongoza katika Asw-Swiraatw (Njia) inayoelekea Jannah. Kisha ikabainishwa mwisho mbaya wa wanafiki na mazungumzo baina yao na Waumini; wakiwaomba Waumini wafuatane nao katika Asw-Swiraat ili wapate Nuru yao, lakini hilo hawatakubaliwa, kwa sababu wao walipokuwa duniani, walifuata matamanio na wakafitini nafsi zao. Na unafiki wao ulidhihirika wa kutilia shaka Risala ya Allaah, na kuwatamania Waislamu iwasibu misiba. Na Ibliys akawaghururi kumuasi Allaah.

 

5-Waumini wanahimizwa kumnyenyekea Allaah (سبحانه وتعالى) na kumkhofu, na wamdhukuru Allaah (سبحانه وتعالى), na kuwatahadharisha wasijekuwa kama waliopewa Kitabu ambao zama ziliwarefukia, na nyoyo zao zikawa ngumu wakatoka katika utiifu wa Allaah.

 

6-Wamebashiriwa Waumini wanaotoa swadaqa zao kuwa, hizo swadaqa ni mkopo mzuri wanaomkopesha Allaah, Naye Anawaahidi kuwalipa maradufu na ujira mtukufu. Na pia wamebashiriwa malipo mema wale waliosadikisha Risala ya Allaah, na kumwamini Rasuli wao (صلى الله عليه وآله وسلم). Ama makafiri waliokadhibisha Risala ya Allaah, wao watakuwa watu wa motoni.

 

7-Kisha Allaah (سبحانه وتعالى) Amepiga mfano wa uhai wa dunia na anasa zake kuwa ni kama mfano wa mvua inayohuisha mimea iliyokufa, kisha baada ya kusitawi inakufilia mbali. Hivyo basi ni zingatio kwa watu kwamba, uhai wa dunia si chochote isipokuwa ni starehe fupi za udanganyifu. Ikatajwa ukumbusho kwamba Aakhirah kuna adhabu kali kwa makafiri. Ama Waumini, wao watapata maghfirah na radhi za Allaah. Kisha Waumini wakaamrishwa kukimbilia kuomba maghfirah na wakatambulishwa upana wa Jannah ambayo Allaah (سبحانه وتعالى) Amewaandalia huko Aakhirah.

 

8-Kuthibitisha  kwamba misiba inayowasibu wanaadam ni kutokana na Qadhwaa na Qadar ya Allaah (Yaliyohukumiwa na Yaliyokadiriwa).

 

9-Imebainishwa kwamba Risala ya Allaah ni moja tu, nayo ni kulingania Tawhiyd ya Allaah. Ikatajwa hikma ya kutumwa Rusuli wa Allaah (عليهم السّلام) pamoja na Vitabu.

 

10-Imeelezewa hali za Manaswara waliofuata Injiyl, kwamba walikuwa wenye nyoyo laini na huruma, na kwamba walizusha maisha ya utawa waliojilazimisha nayo ili kutafuta Radhi za Allaah. Lakini wengi wao hawakufuata ipasavyo, basi walioko walioamini na wengineo walitoka nje ya utiiifu wa Allaah, wakamkanusha Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم).

 

11-Suwrah imekhitimishwa kwa kuamrishwa Waumini wamche Allaah kwa kufuata Amri Zake, na kujiepusha na makatazo Yake, na kumwamini Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم), na wakabashiriwa Rehma ya Allaah na Nuru itakayowaongoza, na kwamba wataghufuriwa madhambi yao. Na kwamba hayo yote, Allaah (سبحانه وتعالى) Amewajaalia ili watu wa Kitabu ambao hawakumuamini Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم),  watambue kwamba, hawawezi kupata chochote katika Fadhila za Allaah, na kwamba Allaah Ni Mwenye Fadhila adhimu na hiba tele kwa Viumbe Vyake.

 

 

 

Share