056-Al-Waaqi’ah: Utangulizi Wa Suwrah

 

056-Al-Waaqi’ah: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

Imeteremka: Makkah kwa itifaki ya ‘Ulamaa,

 

Idadi Za Aayah: 96

 

Jina La Suwrah: Al-Waaqi’ah

 

Suwrah imeitwa Al-Waaqi’ah (Tukio) la Qiyaamah, na inayodalilisha ni kutajwa kwake mwanzo kabisa, Aayah namba (1).

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Kubainisha hali za waja Siku ya Ufufuo. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Kukiri kufufuliwa na kulipwa, na kukumbusha Siku ya Qiyaamah, na kubainisha vigawanyo vya watu ndani yake.

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

1-Suwrah imefunguliwa kwa kukumbusha Tukio la Siku ya Qiyaamah, ambayo haiepukiki. Na ikatajwa yatakayotokea ya vitisho vya ardhi kutikisika, milima kupondwapondwa hadi iwe chembechembe za vumbi.

 

2-Kisha ikabainishwa aina tatu za watu: (i) Wa kuliani (ii) Kushotoni (iii) Waliotangulia (katika khayraat ambao ni katika ummah huu na wengineo).

 

3-Kisha zikatajwa neema kadhaa za Jannah za hawa waliotangulia, nao ni: Kuwa juu ya makochi ya kifakhari, kukabIliana na wenzao kwa furaha, kuhudumiwa kwa vyombo vya mvinyo na chemchemu, kupata matunda wayapendayo na nyama za ndege watakazozitamani, na kujaaliwa hurulaini (wanawake weupe wazuri kwa umbo na macho). Pia humo hawatasikia ya upuuzi ila maamkizi ya Salaam tu!

 

4-Kisha wakatajwa watu wa kuliani na neema zao kadhaaa za Jannah, nazo ni: Kuwekwa kwenye mikunazi isiyo na miba, na migomba ya ndizi iliyopangwa matabaka, kuwekwa katika vivuli vilotandazwa, kupewa maji ya kumiminwa, kuruzukiwa matunda mbalimbali, kuwekwa katika matandiko mazuri, kuozeshwa hurulaini.

 

5-Kisha wakatajwa watu wa kushotoni na jazaa zao za kuingizwa katika moto unaobabu vikali na maji yachemkayo. Na ikatajwa baadhi ya sababu ya adhabu zao, kuwa wameshughulika na anasa za dunia na kutenda maasi, na kutokuamini kufufuliwa. Zikatajwa hoja za nguvu kubainishiwa kwamba, bila shaka watakusanywa wa mwanzo wao na mwisho wao, na kikatajwa chakula chao cha mti wa zaqquwm, na kinywaji chao cha maji yachemkayo.

 

6-Kisha Allaah (سبحانه وتعالى) Akabainisha Uwezo Wake wa Kuumba wanaadam na kuumba vitu vinginevyo huku Akiwauliza makafiri kama wao ndio walivyoviumba hivyo.

 

7-Kisha Allaah (سبحانه وتعالى) Akaapia kwa jambo muhimu, nalo ni maanguko ya nyota, na jibu la kuapia ni kuthibitisha kwamba Qur-aan ni Tukufu mno na kwamba Imeteremshwa na Allaah (سبحانه وتعالى), na kwamba ni Neema ambayo Allaah Amewaneemesha watu lakini hawakushukuru, na wakakadhibisha yaliyo ndani yake.

 

8-Imetajwa aina tatu za watu wanapotolewa roho. (i) Waliokurubishwa ambao hubashiriwa raha, manukato na Jannaat za neema. (ii) Watu wa kuliani ambao hubashiriwa kwa maamkizi ya Salaam (iii) Waliokadhibisha ambao wanapokelewa kwa maji ya moto yachemkayo na kuingizwa motoni.

 

9-Suwrah imekhitimishwa kwa kuthibitishwa kwamba Qur-aan ni haki na yenye yaqini, kisha Allaah (سبحانه وتعالى) Anaamuamrisha Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) Kumsabbih Allaah Mwenye U’adhwama.

 

 

 

Share