059-Al-Hashr: Utangulizi Wa Suwrah

 

059-Al-Hashr: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

Imeteremka: Madiynah kwa itifaki ya ‘Ulamaa wengi.

 

Idadi Za Aayah: 24

 

Jina La Suwrah:  Al-Hashr

 

Suwrah imeitwa Al-Hashr (Mkusanyiko), na inayodalilisha ni kutajwa kwake katika Aayah namba (2). Na pia imeitwa Suwrah Bani An-Nadhwiyr kwa kutajwa katika Hadiyth ifuatayo:

 

عَنْ سَعِيدٍ، قَالَ قُلْتُ لاِبْنِ عَبَّاسٍ ـ رضى الله عنهما ـ سُورَةُ الْحَشْرِ قَالَ قُلْ سُورَةُ النَّضِيرِ‏.‏

Amesimulia Sa’iyd Bin Jubayr: Nilimuuliza Ibn ‘Abbaas kuhusu Suwrah Al-Hashr, Akajibu: Sema Suwrah (Bani) An-Nadhwiyr. [Al-Bukhaariy]

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Kudhihirisha Nguvu na Utukufu wa Allaah katika kuwadhoofisha Mayahudi na wanafiki, na kudhihirisha utengano wao unaokuja baada ya kudhihiri mshikamano kwa Waumini. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Mazungumzo kuhusu vita ya Bani Nadhwiyr, na Nusra ya Allaah kwa Waja Wake Waumini na kuwafedhehesha madhalimu.

 

3-Kutaja baadhi ya Majina Mazuri kabisa ya Allaah na Sifa Zake Tukufu.

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

1-Suwrah imefunguliwa kwa kutajwa kuwa viliomo mbinguni na ardhini vyote Vinamsabbih (Vinamtakasa) Allaah (سبحانه وتعالى) kutokana na yale yasiyoendana Naye, na kumalizia kwa Sifa Zake Tukufu.  

 

2-Imeelezwa kuhusu vita ya Bani Nadhwiyr, na jinsi Allaah (سبحانه وتعالى)  Alivyowepesisha kuwaondosha Madiynah kwa namna wasiyoitegemea, na akawatia khofu kubwa.

 

3-Imetajwa hukmu ya al-fay-u (ngawira inayopatikana bila kupigana vita) na Mwongozo wa Allaah (سبحانه وتعالى) kwa Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) katika mgawanyo huo.

 

4-Wamesifiwa Answaariy (wa Madiynah) walionusuru Dini ya Allaah, kwa kuwapokea vizuri kabisa Muhaajiruna (wa Makkah) na kuwakirimu kwa wingi hadi kwamba walijinyima wenyewe walivyovitoa kwao.

 

5-Wamesifiwa waliokuja baada yao, na duaa yao kwa ndugu zao waliotangulia ya kuondoshewa mafundo na chuki nyoyoni mwao.

 

6-Imebainishwa undani wa wanafiki wa kuungana na Mayahudi dhidi ya Waislamu, na kutaja baadhi ya kauli zao za uongo, na ahadi zao za hadaa.

 

7-Imefichuliwa sifa ya wanafiki ya uongo kuwaahidi Bani Nadhiwyr kuwa watawaunga mkono kuwa pamoja nao watakapotolewa Madiynah, lakini wakawatenga kutokana na kuwaogopa kwao Waumini, na kwamba wao wenyewe kwa wenyewe wana uadui nyoyoni mwao. Na umepigwa mfano wao ni kama mfano wa shaytwaan anapomshawishi mwanaadam akufuru kisha anamkanusha na kujitenga naye!

 

8-Waumini wameamrishwa kumcha Allaah, kujitayarisha na Aakhirah, na kuwakataza kujifananisha na wanaopinga Amri za Allaah, na kukumbusha utofauti wa hali za makundi mawili; ya motoni na watakaoingizwa Jannah

 

9-Watu wamepigiwa mfano wa kubainisha Utukufu wa Qur-aan, na kuwataka watu watafakari, kwamba Qur-aan ingeteremshwa juu ya mlima, ungepasukapasuka kwa khofu na kunyenyekea kwa Allaah kutokana na taathira yake. Basi wanaadam wanapaswa wazingatie Qur-aan na wafanyie kazi maamrisho yake na wajiepushe makatazo yake.

 

10-Suwrah imekhitimishwa kwa kutajwa  baadhi ya Majina Mazuri kabisa ya Allaah na Sifa Zake na kwamba vyote viliomo mbinguni na ardhini Vinamsabbih Allaah.

 

 

 

 

 

 

Share