060-Al-Mumtahinah: Utangulizi Wa Suwrah

 

060-Al-Mumtahinah: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

Imeteremka: Madiynah kwa itifaki ya ‘Ulamaa wengi.

 

Idadi Za Aayah: 13

 

Jina La Suwrah: Al-Mumtahinah

 

Suwrah imeitwa Al-Mumtahinah (Majaribio), na inayodalilisha ni kutajwa katika Aayah namba (10), pindi Waumini walipoamrishwa wawajaribu  Waumini wa kike waliohajiri, imaan zao kama kweli wamemwamini Allaah na Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم).

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Kuwatahadharisha Waumini juu ya kuwafanya makafiri kuwa marafiki wa ndani na walinzi wao. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Amrisho la kusawazisha baina ya kutokuwafanya vipenzi maadui wa Allaah, na kufanya uadilifu kwa kuwatendea wema wale ambao hawakupigana vita na Waislamu. 

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

1-Suwrah imefunguliwa kwa kuwakataza na kuwatahadharisha Waumini, kuwafanya vipenzi maadui wa Allaah na maadui wao, yaani: Maadui wa Waumini katika washirikina waliokuweko Makkah. Hii ni kwa sababu mmoja wa Swahaba alituma barua ya siri kwa mwanamke mmoja aliyekuwa baina ya Madiynah na Makkah, ili aipeleke barua hiyo kwa washirikina kuwajulisha khabari za Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم). Ikabainisha  namna maadui wa Allaah wanavyoichukia haki, na mwisho mbaya wa wale wanaowafanya maadui kuwa vipenzi vyao. Na tahadharisho la kwamba Siku ya Qiyaamah, hata wenye uhusiano wa damu hawataweza kusaidiana.

 

2-Wito kwa Waumini, kufuata kigezo kizuri cha Nabiy Ibraahiym (عليه السّلام) kujiweka mbali na baba yake na watu wake, baada ya kumbainikia kuwa wao ni maadui wa Allaah kutokana na kumshirikisha na kukataa kupokea haki.    

 

3-Kuweka wazi ruhusa ya kuwafanyia makafiri muamala mzuri wale ambao hawakuwapiga vita Waislamu na wala hawakuwatoa katika majumba yao.

 

4-Imepambanua hukumu za wanawake ambao wamehajiri hali ya kua ni Waumini, kutokuwarejesha kwa makafiri, na ruhusa ya kuwaoa baada ya kuwaacha waume zao makafiri.  

 

5-Allaah Amemuamrisha Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) kuwafanyia bay’ah (fungamano la utiifu) wanawake Waumini, na kuchukua ahadi juu yao ya kumtii Allaah, na kujiweka mbali na yaliyoharamishwa.

 

6-Suwrah imekhitimishwa kwa kuwakataza Waumini kuwafanya maadui wa Allaah na maadui zao kuwa vipenzi.

 

 

 

 

Share