070-Al-Ma’aarij: Utangulizi Wa Suwrah

 

070-Al-Ma’aarij: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

Imeteremka: Makkah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.

 

Idadi Za Aayah: 44

 

Jina La Suwrah: Al-Ma’aarij

 

Suwrah imeitwa Al-Ma’aarij (Njia Za Kupanda), na inayodalilisha ni kutajwa kwake katika Aayah namba (3), na rejea Tanbihi ya Aayah namba (3) ya Suwrah hii ya Al-Ma’aarij kupata maana nyenginezo.  

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Kubainisha hali ya malipo ya waja Siku ya Qiyaamah. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Kukumbusha Siku ya Qiyaamah na hali zake ngumu, na yatakayotokea pamoja na kuhesabiwa na kulipwa, na thawabu (malipo mema) na adhabu.

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

1-Suwrah imefunguliwa kwa kubainishwa ada mojawapo ya makafiri kuharakiza adhabu, nayo itawashukia tu hakuna wa kuizuia isipokuwa Allaah (سبحانه وتعالى), Mwenye Uluwa na fadhila tele.

 

2-Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) ameliwazwa kwa kutakwa avute subira kwa istihzai za makafiri wanaomkadhibisha na kuharakiza adhabu na kudhania kuwa iko mbali kabisa wala haitatokea, ilhali ipo karibu na hakuna shaka ya kutokea kwake. 

 

3-Kisha yakatajwa baadhi ya matukio ya Siku ya Qiyaamah na majuto ya wahalifu Siku hiyo, watamani kujitolea fidia kwa ahli zake wote kutokana na adhabu.  

 

4-Zimetajwa baadhi ya sifa za moto wenye mwako mkali kwamba unaonyofoa na ngozi za mwili na kuunguza viungo vya mwili.

 

5-Imetajwa hali ya baadhi ya  wanaadam wenye kukosa kuvuta subira na hali yake anapopatwa shari kuwa hupapatika na kuhuzunika. Anapopatwa kheri hufanya uchoyo. Kisha ikafuatilia kuwasifu Waumini wasiokuwa na sifa za mwanaadam huyo aliye na pupa na kukosa subira.

 

6-Zikatajwa sifa za Waumini hao zikianza kuwasifia kuwa ni wenye kusimamisha na kudumisha Swalaah, na sifa nyenginezo kisha kumalizikia pia wenye kuhifadhi Swalaah zao. Na sifa hizi takriban, ni kama zile zilizotajwa mwanzoni mwa Suwrah Al-Muuminuwn (23), na zinamalizikia kwa kuahidiwa Jannah (Pepo).

 

7-Suwrah imekhitimishwa kwa kukemewa makafiri na kutajwa hali zao zitakavokuwa Siku ya Qiyaamah watakapotolewa makaburini kufufuliwa wakiwa madhalili na duni.     

 

 

 

 

 

 

 

 

Share