069-Al-Haaqqah: Utangulizi Wa Suwrah

 

069-Al-Haaqqah: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

Imeteremka: Makkah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.

 

Idadi Za Aayah: 52

 

Jina La Suwrah: Al-Haaqqah

 

Suwrah imeitwa Al-Haaqqah (Tukio la haki lisiloepukika), na inayodalilisha ni kutajwa kwake mwanzo wa Suwrah Aayah namba (1-3)

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Kuthibitisha kutokea Qiyaamah na malipo ni kweli. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Maelezo kuhusu Siku ya Qiyaamah na hali za watu Siku hiyo.

 

2-Kusimamisha dalili juu ya ukweli wa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) uthibitisho wa Qur-aan kutoka kwa Allaah (سبحانه وتعالى).

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

1-Suwrah imefunguliwa kwa kuthibitisha tukio la Qiyaamah ambalo haliepukiki!

 

2-Wametajwa kina Thamuwd ambao ni kaumu ya Nabiy Swaalih (عليه السّلام), na kina ‘Aad ambao ni kaumu ya Nabiy Huwd (عليه السّلام) na kwamba wote hawa walikanusha Risala ya Allaah kupitia Rusuli wao hao na wakakanusha Qiyaamah, na zikatajwa baadhi ya adhabu zao za maangamizi. Kisha wakafuatilia kutajwa Firawni na walio kabla yake, na watu waliopinduliwa chini juu kuadhibiwa, ambao ni watu Nabiy Luutw (عليه السّلام), na wote waliwaasi Rusuli wao basi Allaah (سبحانه وتعالى) Akawaangamiza. Kisha ikatajwa kuokolewa kwa Nabiy Nuwh (عليه السّلام) kwa kupandishwa katika jahazi na kuangamizwa makafiri kwa gharka ili iwe mawaidha na mazingatio kwa watu wenye kusikia na kutia akilini. Rejea Al-‘Ankabuwt (29:40) kwenye maelezo kuhusu aina za kufru za nyumati za awali na aina zao za adhabu na maangamizi.

 

3-Imeelezwa matukio ya  Siku ya Qiyaamah kuanziwa kupulizwa baragumu, na ardhi na milima kupondwapondwa, na mbingu kuraruka. Kisha kuteremka Malaika wanane wakiwa wamebeba ‘Arsh ya Allaah (عزّ وجلّ), na mkusanyiko wa watu ili kuhesabiwa matendo yao.

 

4-Imeelezewa watu watakaopokea Kitabu chao kuliani na furaha zao za kufaulu Siku hiyo tukufu, na jazaa zao za kuingizwa Jannah watakapodumu milele humo wakistareheshwa kwa kila aina za neema.

 

5-Kisha wakatajwa watakaopokea Kitabu chao kushotoni na majuto yao, na jinsi watakavyofungwa pingu na minyororo kuingizwa motoni na kimetajwa chakula chao humo cha usaha.

 

6-Allaah (سبحانه وتعالى) Ameapia kwa vinavyoonekana na visivyoonekana, na jibu la kiapo ni kuthibitisha ukweli wa Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) na aliyoyabalighisha kutoka katika Qur-aan Tukufu, na Allaah Kuziradd sifa ovu za kuisingizia Qur-aan kuwa ni mashairi au kauli za kahini na kuthibitishwa kuwa ni Uteremsho wa Rabb wa ulimwengu.

 

7-Imebainishwa kwamba Qur-aan ni Ukumbusho kwa Waumini na majuto kwa makafiri.

 

8-Suwrah imekhitimishwa kwa amri ya Kumsabbih (Kumtakasa) Allaah (عزّ وجلّ).  

 

 

 

 

 

Share