074-Al-Muddath-thir: Utangulizi Wa Suwrah

 

074-Al-Muddath-thir: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

Imeteremka: Makkah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.

 

Idadi Za Aayah: 56

 

Jina La Suwrah: Al-Muddath-thir

 

Suwrah imeitwa Al-Muddath-thir (Mwenye Kujigubika), na inayodalilisha ni kutajwa kwake katika Aayah namba (1).

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Kuamrisha watu kujitahidi katika kuwalingania wanaokadhibisha (Risala ya Allaah), na kuwaonya kwa Aakhirah na Qur-aan. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Kumliwaza Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kwa kuwaradd washirikina wa Makkah na kuwaahidi adhabu kwa kukanusha Risala ya Allaah.

 

3-Kubainishwa sababu za kuingizwa motoni.

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

1-Suwrah imefunguliwa kwa kuamrishwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) aliyenadiwa kwa Al-Muddath-thir (Aliyejigubika nguo) ainuke kwa ajili ya kubalighisha Risala ya Allaah (سبحانه وتعالى)  na kuwaonya watu wake, na Amtukuze Rabb wake, na atoharishe nguo zake. Na akaamrishwa kuendelea kujiepusha na ushirikina.

 

2-Kisha akaongozwa katika misimamo ya da’wah ambayo ni kuwa na ikhlaasw katika da’wah kwa kutokutaraji malipo kutoka kwa watu, na kuvuta subira kwani lazima kuweko maudhi na mateso katika da’wah.

 

3-Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) ameliwazwa kutokana na kukadhibishwa na watu wake wa Makkah, kwa kuwatishia maadui zake kwa aina kali za adhabu. Na ikaelezwa kisa cha mmoja wa Quraysh aliyekuwa tajiri na hadhi kubwa katika Maquraysh, aliyeisikiliza Qur-aan kutoka kwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم), ambayo ilimuathiri kutaka kuiamini, lakini akatafakari na kutafakari, mwishowe akatakabari na kuipachika sifa ovu Qur-aan kuwa ni sihri inayonukuliwa tu! Basi Allaah (سبحانه وتعالى) Akamuahidi kafiri huyo adhabu kali ya moto wa saqar usiobakisha nyama wala mifupa ila kuvichoma, na unaounguza ngozi hadi iwe nyeusi.

 

4-Kisha ikatajwa idadi ya Malaika kumi na tisa (19) ambao ni walinzi wa moto, walio wakali na washupavu, na idadi hiyo ikawa ni jaribio kwa makafiri ili iwe yakini kwa Mayahudi na Manaswara kutambua yanayoafikiana na yale yaliyoandikwa katika Vitabu vyao kuhusu Malaika wa hazina ya moto, na iwazidishie imaan Waumini. Na wale wanafiki wenye maradhi nyoyoni mwao na makafiri waseme: “Ni lipi Alokusudia Allaah kwa idadi hii ya ajabu?” Lakini mfano kama huu, Allaah Humpotoa Amtakaye na Humhidi Amtakaye kwa sababu Ana Ujuzi wa ghaibu wa kujua yalimo nyoyoni mwa watu.

 

5-Kisha ikafuatilia Kiapo cha Allaah (سبحانه وتعالى) kuapia mwezi na usiku unapogeuka kutoweka, na asubuhi inapopambazuka. Na jibu la kiapo ni kuthibitishwa moto kwamba, ni katika mambo makuu na kwa ajili ya kuwatishia watu.

 

6-Imebainishwa mwisho mzuri wa Waumini kuingizwa Jannah. Na ikabainishwa mwisho mbaya kwa wahalifu, na zikatajwa sababu zao kuwa walikuwa hawaswali, wala kulisha masikini, na kunena ya ubatilifu pamoja na wapotevu.

 

7-Makafiri wamekemewa kwa kujiepusha kwao na Qur-aan, na kutaka wateremshiwe kitabu chao kutoka mbinguni, na kutokuiogopa Aakhirah.

 

8-Suwrah imekhitimishwa kwa kuthibitishwa kuwa Qur-aan ni mawaidha ya ufasaha, na kwamba hawaidhiki nayo isipokuwa ambaye Allaah (سبحانه وتعالى) Ameshamjua anayetaka kuwaidhika, hivyo basi Humhidi kwayo Amtakaye, na kwamba Allaah (سبحانه وتعالى) Ndiye Anayestahiki kuogopwa na Mwenye Kustahiki kughufuria madhambi ya waja.

 

 

Share