075-Al-Qiyaamah: Utangulizi Wa Suwrah

 

075-Al-Qiyaamah: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Imeteremka: Makkah kwa itifaki ya ‘Ulamaa

 

Idadi Za Aayah: 40

 

Jina La Suwrah: Al-Qiyaamah

 

Suwrah imeitwa Al-Qiyaamah (Ufufuo), na inayodalilisha ni kutajwa kwake katika Aayah namba (1).

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Kudhihirisha Uwezo wa Allaah (سبحانه وتعالى) wa kuwafufua viumbe, na kuwakusanya Siku ya Qiyaamah. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Kuielezea Siku ya Qiyaamah na maelezo ya baadhi ya vitisho vyake, na hali za watu Siku hiyo.

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

1-Suwrah imefunguliwa kwa kiapo cha Allaah (سبحانه وتعالى) Kuapia Siku ya Qiyaamah, na nafsi inayojilaumu kwa kufanya maovu na kuacha kutenda mema. Na jibu lake limefuatia la kuwaradd wasioamini kufufuliwa, kwa kutolewa dalili ya nguvu kabisa, nayo ni kusawazisha sawasawa ncha za vidole vyao.

 

2-Imethibitishwa tena kufufuliwa kwa viumbe na kutajwa ada za makafiri kukanusha Qiyaamah kwa kuulizia lini kitatokea.

 

3-Kisha ikathibitishwa baadhi ya matukio ya Qiyaamah kama kutokea kwa khusuwf (kupatwa mwezi) na kusuwf (kupatwa jua). Na hapo mtu hatakuwa na pa kukimbilia, na atasimamishwa atambulishwe yote aliyoyatenda na kuhesabiwa. Na Siku hiyo mtu atajishuhudia mwenyewe wala hatoweza kutoa nyudhuru zozote zile. 

 

4-Allaah (سبحانه وتعالى) Amemuongoza Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) adabu za kupokea Wahy.

 

5-Zimetajwa hali za watu kutofautiana; wema na waovu. Wema wataneemeshwa kwa kung’arishwa nyuso zao pindi watakapomwangalia Rabb wao huko Jannah. 

 

6-Imekumbushwa mauti na kwamba (hayo mauti) ndio hatua ya mwanzo ya Aakhirah.

 

7-Suwrah imekhitimishwa kwa kuwathibitishia makafiri waliojigamba na kutakabari na kukanusha kufufuliwa, dalili za wazi kabisa za Uwezo wa Allaah (سبحانه وتعالى) kwamba Yeye Aliyewaumba kutokana na tone la manii, kisha Akaziunda sura na maumbo yao vizuri kabisa, kisha Akajaalie jinsia mbili; ya kiume na kike, kwamba yeye Allaah (سبحانه وتعالى) ni Mweza wa Kuwahuisha baada ya kufa kwao!

 

 

 

Share