068-Al-Qalam: Utangulizi Wa Suwrah

 

068-Al-Qalam: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

Imeteremka: Makkah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.

 

Idadi Za Aayah: 52

 

Jina La Suwrah: Al-Qalam

 

Suwrah imeitwa Al-Qalam (Kalamu), na inayodalilisha ni kutajwa kwake katika Aayah namba (1)

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Ushuhuda wa Allaah kwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) juu ya tabia njema, na kumtetea na kumthibitisha. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Kubatilisha shutuma za washirikina kwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) na kubainisha upotevu wao.

 

3-Kuthibitisha utimamu wa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) duniani na Aakhirah, na kumthibitisha.

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

1-Suwrah imefunguliwa kwa herufi zinazojulikana kama Al-Huruwf Al-Muqatw-twa’ah ambazo, hakuna ajuaye maana zake isipokuwa Allaah. Rejea Al-Baqarah (2:1). Na ikafuatia kiapo cha Allaah (سبحانه وتعالى) kwa Al-Qalam (Kalamu) inayoandikwa na Malaika na watu, mambo wanayoyaandika ya kheri na manufaa.  

 

2-Kisha ikafuatia jibu la kiapo nalo ni kumsifia Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kwa sifa bora kabisa za khulqa na tabia zake, na kwamba atapata ujira usiokatika, na kumliwaza kwa Kuradd shubha za washirikina waliokuwa wakimpachika sifa ovu Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم).  

 

3-Allaah (سبحانه وتعالى) Amemkataza Nabiy Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) kutokuwatii waliokadhibisha, na kwamba wametamani lau angeliwalegezea na kulainisha baadhi ya misimamo yao, nao wawe laini kwake. Amemkataza pia kutokumtii mtu anayeapa kwa wingi.  Kisha zikatajwa sifa kadhaa ovu za mtu huyo aliyejaaliwa utajiri akatakabari kuikubali haki.

 

4-Washirikina wa Makkah wametahiniwa kwa njaa na ukame kama walivyotahiniwa watu waliomiliki shamba. Ikaelezewa kisa chao walivyoapa kutilia niya kuwazuia maskini wasipate rizki ya mavuno ya shamba hilo. Wakapania kuliendea shamba asubuhi mapema bila ya kusema In Shaa Allaah, wapate kuvuna mazao ya shamba kabla ya kuingia maskini na mafuqaraa. Lakini Allaah (سبحانه وتعالى) Akaliangamiza shamba hilo kwa kulipelekea moto nyakati za usiku hali wao wakiwa wamelala. Walipoamka asubuhi na kuliendea, walidhania wamepotea, kisha wakatanabahi kuwa  wameharamishwa nalo. Na mwishowe watu hao wa shamba wakabakia kujuta na wakajirudi kwa Rabb wao. Na hiyo ni adhabu ndogo  ya dunia ambayo ni afadhali kuliko adhabu ya Aakhirah.

 

5-Waumini wanaomcha Allaah (سبحانه وتعالى) wamebashiriwa Jannaat za neema.

 

6-Imetofautishwa kati ya wanaomnyenyekea Allaah (سبحانه وتعالى) na wahalifu. Kisha Allaah (سبحانه وتعالى) Akawaradd hao wahalifu kwa kutoa hukmu ya dhulma kulinganisha baina yao na Waumini katika malipo, na kuwahoji walete dalili zao kama wana haki ya hayo wanayojihukumia.

 

7-Imetajwa baadhi ya matukio ya Siku ya Qiyaamah ambayo mambo yatakuwa magumu mno! Na ikatajwa Kufika kwa Allaah Awahukumu viumbe vyote, Afunue Muundi Wake usiofanana na kitu chochote, kisha hapo Waumini waliokuwa wakimsujudia Allaah (سبحانه وتعالى) duniani kwa khiari na kupenda kwao, wataweza kumsujudia Allaah Siku hiyo. Ama makafiri, wanafiki na wahalifu ambao walikanusha duniani kumsujudia Allaah ilhali walikuwa wazima, watataka kusujudu Siku hiyo, lakini hawataweza kusujudu kamwe! Uti wa mgongo wao utakuwa kama mfupa mmoja usioweza kupinda! 

 

8-Allaah (سبحانه وتعالى) Amemliwaza Nabiy Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) kwamba Amwachie Yeye mambo yote ya makafiri wanaokanusha Qur-aan, na kwamba Atawavuta pole pole kwenye adhabu kwa namna wasiyoijua, na hakuna atakayeweza kuikwepa.

 

9-Kisha Allaah (سبحانه وتعالى) Akamliwaza tena Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) kwa kumtaka avute subira, na kumkataza asije kuwa mwenye kukosa kuvuta subira, kama alivyokosa subira Nabiy Yuwnus (عليه السّلام) aliyemezwa na samaki alipoghadhibika na watu wake, akamuomba Allaah (سبحانه وتعالى) Awaharakizie adhabu kwa kukanusha Risala ya Allaah. Na lau kama si Neema ya Allaah kumwafikia kutubia, basi angelitupwa ufukoni   kutoka tumboni mwa chewa, akitesekea na akiwa mwenye kulaumiwa kwa kuteleza kwake. Lakini Allaah (سبحانه وتعالى) Akamjaalia kuwa miongoni mwa Swalihina.   

 

10-Suwrah imekhitimishwa kwa kutahadharishwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) na jicho baya la uhasidi wa washirikina wanapoisikia Qur-aan, na kwamba Allaah Amemhami na hayo. Na ikatajwa mojawapo wa ada zao za kumpachika sifa ovu Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kama kumwita majnuni. Kisha Allaah (سبحانه وتعالى) Anamthibitishia Nabiy Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) kwamba  Qur-aan ni Ukumbusho na mawaidha kwa walimwengu wote miongoni mwa  wanaadam na majini.

 

 

 

Share