076-Al-Insaan: Utangulizi Wa Suwrah

 

076-Al-Insaan: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

Imeteremka: Makkah au Madiynah kwani ‘Ulamaa wamekhitilafiana kuhusu wapi imeteremshwa.

 

Idadi Za Aayah: 31

 

Jina La Suwrah: Al-Insaan

 

Suwrah imeitwa Al-Insaan (Binaadam) kwa kutajwa kwake katika Aayah namba (1). Na pia kutajwa kwa jina lake jengine katika Hadiyth iliyonukuliwa chini katika Fadhila.

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Kumkumbusha binaadam asili ya kuumbwa kwake na mafikio yake, na kubainisha Aliyoyaahidi Allaah (سبحانه وتعالى) kwa Vipenzi Vyake. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Kutajwa kuumbwa kwa binaadam, na kugawanyika kwao na marejeo yao Siku ya Qiyaamah.

 

3-Kuwafanya wanaadam wawe na At-Targhiyb (Yanayoshajiisha nafsi kuikubali haki na kutenda mema kutokana na fadhila zake) na At-Tarhiyb (yanayotishia na kutahadharisha kutenda maasi kutokana na malipo yake).  

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

1-Suwrah imefunguliwa kwa kumkumbusha mwanaadam Neema za Allaah (سبحانه وتعالى) juu yake, pale alipoumbwa kutokana na tone la manii yaliyochanganyika, na akamfanya mwenye kusikia, mwenye kuona, na akamuongoza njia, basi kuna anayeshukuru na anayekufuru.

 

2-Makafiri wameahidiwa maandalizi ya motoni huku wamefungwa minyororo na pingu.

 

3-Al-Abraar (wenye kutenda mema mengi) wameahidiwa mazuri ya mto wenye kinywaji kizuri cha kafuri. Na zikatajwa sifa zao kadhaa kama kutimiza nadhiri zao, na kukhofu adhabu za Allaah, kulisha kwa mapenzi yao masikini, yatima na matekwa ya vita bila kutaka shukurani au kusifiwa, kuvuta kwao subira duniani. Kisha ikafuatia kutajwa mazuri na Neema kadhaa za Allaah Alizowaandalia Al-Abraar hao katika Jannah vikiwemo vyakula wanavyovitamani, vinywaji safi visivyo na madhara, mavazi na mengineyo kadhaa.

 

4-Imethibitishwa kwamba Qur-aan imetoka kwa Allaah (سبحانه وتعالى) na kumliwaza Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) avute subira kutokana na maudhi ya makafiri, na kumwamrisha amdhukuru Rabb wake asubuhi na jioni, na Kumsujudia na Kumsabbih (Kumtakasa) nyakati nyingi za usiku.

 

5-Suwrah imekhitimishwa kwa kubainishwa kwamba hakuna awezaye kutaka jambo lolote lile isipokuwa liwe kwa Matakwa ya Allaah (سبحانه وتعالى), na kwamba Anamuingiza Amtakaye katika Rehma Yake, na Amewaandalia adhabu kali madhalimu.

 

Fadhila Za Suwrah:

 

Inapendekezwa kuisoma katika Swalaah ya Asubuhi Siku ya Ijumaa katika Rakaa ya pili kwa dalili ifuatayo:

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ ـ رضى الله عنه ـ قَالَ كَانَ النَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم يَقْرَأُ فِي الْجُمُعَةِ فِي صَلاَةِ الْفَجْرِ ‏ الم * تَنْزِيلُ‏  السَّجْدَةَ   وَ‏   هَلْ أَتَى عَلَى الإِنْسَانِ‏

Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akisoma katika Swalaah ya Alfajiri siku ya Ijumaa:

الم ﴿١﴾ تَنزِيلُ

As-Sajdah (32) na

هَلْ أَتَىٰ عَلَى الْإِنسَانِ

Suwrah Al-Insaan (76). [Al-Bukhaariy, Muslim na wengineo]

 

 

Share