082-Al-Infitwaar: Utangulizi Wa Suwrah

 

082-Al-Infitwaar: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

Imeteremka: Makkah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.

 

Idadi Za Aayah: 19

 

Jina La Suwrah: Al-Infitwaar

 

Suwrah imeitwa Al-Infitwaar (Kupasukapasuka), na yanayodalilisha ni kutajwa Hadiyth iliyonukuliwa katika Faida, na kutajwa katika Aayah namba (1).

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Kumtahadharisha mwanaadam kutodanganyika, na kuisahau Siku ya Qiyaamah. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Kuthibitisha kufufuliwa, na kubainisha vitisho vya Siku ya Qiyaamah, na kuwazindua watu kujiandaa nayo.

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

1-Suwrah imefunguliwa kwa kutajwa yatakayotokea Siku ya Qiyaamah, yenye kushtua nyoyo, kama mbingu kupasukapasuka, sayari kuanguka na kutawanyika, bahari kupasuliwa, makaburi kupinduliwa chini juu. Kisha ikafuatia kubainishwa kwamba kila mtu atajua siku hiyo aliyoyatanguliza na aliyoyachelewesha.

 

2-Kisha kafiri anayekanusha kufufuliwa na kuhesabiwa, anaulizwa ni kipi kilichomfanya ahadaike na aghurike kuhusu Rabb wake, Mpaji, Mwenye Kheri nyingi na Anayestahiki kushukuriwa na kutiiwa?  Rabb Ambaye Amemuumba Akamsawazisha umbo, sura na viungo na Akamrekebisha ili aweza kutekeleza nyadhifa zake.?

 

3-Imebainishwa kwamba matendo ya mwanaadam yamewakilishwa kwa Malaika watukufu wenye kuyaandika.

 

4-Imebainishwa wema na waovu na malipo yao; wema wataingizwa Jannah waneemeke humo kwa kila aina za neema. Waovu wataingizwa motoni kuadhibiwa. 

 

5-Suwrah imekhitimishwa kwa kujulishwa kwamba Siku ya Qiyaamah, hakuna kusaidiana au kunufaishana, na Amri zote Siku hiyo ni za Allaah Pekee na hakuna wa kushindana Naye.

 

Faida:

 

Anayetaka Kuitazama Siku Ya Qiyaamah, Asome Suwrah hii:

 

عَنْ عَبْدِ الرَّحْمَنِ، وَهُوَ ابْنُ يَزِيدَ الصَّنْعَانِيُّ قَالَ سَمِعْتُ ابْنَ عُمَرَ، يَقُولُ قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم ‏"‏ مَنْ سَرَّهُ أَنْ يَنْظُرَ إِلَى يَوْمِ الْقِيَامَةِ كَأَنَّهُ رَأْىُ عَيْنٍ فَلْيَقْرَأْ ‏ إِذَا الشَّمْسُ كُوِّرَتْ)‏ و ‏ (‏إِذَا السَّمَاءُ انْفَطَرَتْ)‏ وَ ‏ (‏إذَا السَّمَاءُ انْشَقَّتْ‏"‏ ‏.‏ هَذَا حَدِيثٌ حَسَنٌ غَرِيبٌ

Amesimulia ‘Abdur-Rahmaan naye ni Ibn Yaziyd Asw-Swan’aaniyy (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Mwenye kutaka kuitazama Siku ya Qiyaamah, kana kwamba anaiona kwa jicho hili, basi na asome:

إِذَا الشَّمْسُ كُوِّرَتْ ﴿١﴾

 

“Jua litakapokunjwa kunjwa na kupotea mwanga wake.” [At-Takwiyr (81)]

 

إِذَا السَّمَاءُ انفَطَرَتْ ﴿١﴾

“Mbingu itakapopasuka.” [Al-Infitwaar (82)]

إِذَا السَّمَاءُ انشَقَّتْ ﴿١﴾

“Mbingu itakaporaruka.” [Al-Inshiqaaq (84)]

 

[Ahmad (4806), At-Tirmidhiy (3333), amesema ni Hadiyth Hasan Ghariyb. Ameisahihisha Al-Albaaniy katika Swahiyh At-Tirmidhy] 

 

 

 

 

 

 

Share