083-Al-Mutwaffifiyn: Utangulizi Wa Suwrah

 

083-Al-Mutwaffifiyn: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

Imeteremka: Makkah au Madiynah kwani ‘Ulamaa wamekhitilafiana kuhusu wapi imeteremshwa.

 

Idadi Za Aayah: 36

 

Jina La Suwrah: Al-Mutwaffifiyn

 

Suwrah imeitwa Al-Mutwaffifiyn (Wanaopunja), na inayodalilisha ni kutajwa kwake katika Aayah namba (1).

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Kuwatahadharisha wanaokadhibisha, wanaodhulumu (katika kipimo) na (yatakayowapata) Siku ya Qiyaamah, na kuwapa bishara Waumini juu hilo. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Kutahadharisha kupunja vipimo.

 

3-Kuelezea kuhusu watu waovu na watu wema na kulinganisha mafikio ya kila mmoja wao.

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

1-Suwrah imefunguliwa kwa onyo na ahadi ya adhabu, kwa wenye kupunja vipimo vya ujazo mezani, na kuwathibitishia Siku Tukufu ya kufufuliwa na kusimamishwa mbele ya Allaah kuhesabiwa.

 

2-Kimetajwa kitabu cha waovu, mafasiki, wanafiki kuwa kiko Sijjiyn, ambako ni mahali pa dhiki mno! Na imesemwa kuwa Sijjiyn ni chini ya ardhi saba ambapo ni makazi mabaya ya kudumu, waadhibiwe humo madhalimu na waovu hao kwa kukadhibisha Siku ya Malipo, na  kukanusha Aayah za Allaah, kwa kudai kuwa ni hekaya za kale. Na humo ndipo walipoandikiwa wafike, na humo ndipo yalipoandikwa na kurekodiwa barabara matendo yao, na hapana kitakachozidishwa wala kupunguzwa.

 

3-Ikaelezewa kuwa nyoyo za hao madhalimu na wakadhibishaji zimezibwa na kufunikwa madhambi, hivyo basi hawatamuona Allaah (سبحانه وتعالى).

 

4-Kisha kikatajwa Kitabu cha Al-Abraar (Waumini watendao mema kwa wingi), kwamba kipo ‘Illiyyiyn (daraja za juu). Na kwamba hakizidishwi kitu humo wala hakipunguzwi. Wanayatazama yaliyomo ndani yake, Malaika waliokurubishwa. Na wakasifiwa Al-Abraar kwamba watakuwa katika Jannah yenye neema za kila aina. Nyuso zao zina mng’aro, na watanyweshwa kinywaji safi, mchanganyo wake unatokana na chemchemu iliyoko Peponi. Kinywaji hicho kinajulikana kwa ubora wake kwa jina la Tasniym. Na kinywaji hicho kimetengezewa katika vyombo kwa ustadi na mwishowe kuna harufu ya misk.

 

5-Imeelezewa jinsi walivyokuwa wakiwadharau Waumini na kuwafanyia dhihaka, shere na istihzai na kuwaudhi.  

 

6-Suwrah imekhitimishwa kwa kuwabashiria Waumini ya kwamba, wao Siku ya Qiyaamah watakuwa katika hali ya juu ya taadhima. Na watawacheka makafiri kama walivyokuwa wao wakiwacheka na kuwafanyia shere walipokuwa duniani. Basi makafiri na wanafiki watalipwa malipo muwafaka na yale waliyoyafanya duniani.

 

 

 

 

Share