089-Al-Fajr: Utangulizi Wa Suwrah

 

089-Al-Fajr: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

Imeteremka: Makkah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.

 

Idadi Za Aayah: 30

 

Jina La Suwrah: Al-Fajr

 

Suwrah imeitwa Al-Fajr (Alfajiri), na inayodalilisha ni kutajwa kwake katika Aayah namba (1)

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Kubainisha mwisho wa waovu, na hikma ya kuletwa mitihani, na kuwakumbusha Aakhirah. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Kumthibitisha na kumtia nguvu Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم).

 

2-Kuthibitisha Al-Aakhirah (Siku ya Mwisho) na kuhesabiwa kwa malipo ya motoni au kuingizwa Jannah.

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

1-Suwrah imefunguliwa kwa Kiapo cha Allaah (سبحانه وتعالى) Kuapia Alfajiri, na masiku kumi ya mwanzo wa mwezi wa Dhul-Hijjah, ambayo ni masiku bora kabisa ya Allaah. Akaendelea Allaah (سبحانه وتعالى) Kuapia kwa shufwa (idadi inayogawanyika kama mbili, nne, sita n.k). Na witr (idadi pweke isiyogawanyika kama moja, tatu, tano n.k). Na kwa usiku unapopita na giza lake. Ikafuatia uhakikisho wa kiapo ambao ni adhabu na maangamizo yaliyowapata kina ‘Aad ambao ni kaumu ya Nabiy Huwd (عليه السّلام). Hawa waliumbwa kwa umbo kubwa la nguvu, na hawakuumbwa mfano wao katika ardhi. Na wakatajwa kina Thamwud ambao ni kaumu ya Nabiy Swaalih (عليه السّلام) waliojaaliwa uwezo wa kuchonga jabali na kufanya nyumba ndani yake. Na Firawni aliyekuwa na askari waliouhami ufalme wake na kuutilia nguvu. Basi hao wote waliotajwa, walivuka mipaka wakawakanusha Rusuli wao na wakafanya ufisadi katika ardhi, basi Allaah (سبحانه وتعالى) Akawaangamiza kwa adhabu kali kabisa.

 

2-Imebainishwa hali ya binaadam asiye na shukurani kwamba, pindi Allaah (سبحانه وتعالى) Anapomkunjuliwa riziki hujivuna. Na Anapomjaribu kwa kumdhikisha rizki, basi hughalifika na kulalamika kuwa kadhalilishwa.

 

3-Wamekemewa wanaadam kama hao, kwa kutokuwakirimu mayatima na kutowatendea wema, wala hawafanyi hima kulisha masikini, na kula kwao mali za kurithi bila ya haki, na kupenda kwao mali kupita kiasi.

 

4-Wamekumbushwa watu vitisho vya Siku ya Qiyaamah, na matukio yake kama kuteremka Malaika na Kuteremka Allaah (سبحانه وتعالى), Mteremko unaolingana na Utukufu Wake, ili Awahesabie viumbe matendo yao na kuwalipa; ima waingizwe motoni au Jannah. Na watu wa motoni siku hiyo watadhihirisha majuto yao ya kutaka kutubia na kutamani kurudi  duniani!

 

5-Suwrah imekhitimishwa kuwabashiria wenye nafsi zilizotulia kwamba wataridhika na Allaah, na Allaah Atawaradhia, na wataambiwa waingie katika Jannah ya Allaah (سبحانه وتعالى). 

 

 

 

 

 

Share