090-Al-Balad: Utangulizi Wa Suwrah

 

090-Al-Balad: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

Imeteremka: Makkah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.

 

Idadi Za Aayah: 20

 

Jina La Suwrah: Al-Balad

 

Suwrah imeitwa Al-Balad (Mji), na inayodalilisha ni kutajwa kwake katika Aayah namba (1).

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Kubainisha kuhitajia kwa mwanaadam, na kubainisha vitimbi vyake, na njia za kuokoka kwake. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Kutaja maumbile ya dunia na kile anachosumbuka nacho mwanaadam ndani yake katika kuvumilia kubeba shida, na kile kinachompeleka katika furaha.

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

1-Suwrah imefunguliwa kwa Kiapo cha Allaah (سبحانه وتعالى) Kuapia Al-Balad (Mji) ukikusudiwa mji Mtukufu wa Makkah na kuishi kwake Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) humo akiuzidisha Utukufu wake. Na kuapia kwa mzazi wa wanaadam (Aadam) na kilichozalikana naye (wanaadam). Kisha ikahakikishwa jambo linaloapiwa, nalo ni kuumbwa binaadam katika mashaka na tabu za kilimwengu, tokea mwanzo wa kuzaliwa kwake, kuishi kwake duniani, katika maisha yake ya Al-Barzakh baada ya kufariki, na atakapofufuliwa Siku ya Qiyaamah.

 

2-Imetajwa ubaya wa binaadam kudanganyika kwa nguvu alizonazo na mali, akafanya kiburi na kujivuna na kuvuka mipaka kuitumia mali kwa matamanio yake, akadhania kwamba hakuna awezaye kumdhalilisha, na akadhania kwa matendo yake hayo, kwamba Allaah (سبحانه وتعالى) Hamuoni wala Hatamhesabu juu ya matendo makubwa na madogo. Bali Allaah (سبحانه وتعالى) Anamuona na Amewawakilisha Malaika wanaoandika matendo yote; mema na maovu.

 

3-Binaadam huyo anakumbushwa Neema za Allaah (سبحانه وتعالى) Alizomjaalia aonekane mwenye sura nzuri yenye macho mawili ya kuonea, na midomo miwili ya kusemea, na kumbainishia njia mbili; ya kheri na shari itakayomwongoza ima katika hidaaya au upotovu, na ajichagulie mwenyewe aitakayo. Neema hizo kubwa zinamtaka mja azitimize haki za Allaah kwa kumshukuru na kutoa katika yanayomridhisha na sio kuzitumia kwa dhambi zake. Lakini mtu huyu hakufanya hivyo kujiepusha na janga la Aakhirah kwa kutoa mali yake kwa sababu ya kufuata matamanio yake, kama vile kukomboa Waumini kutokana na utumwa, au kulisha watu siku za njaa, na kumhudumia yatima aliye jamaa, au maskini aliye fakiri kabisa.

 

4-Suwrah imekhitimishwa kwa kubainisha mwisho mwema wa Waumini na makafiri. (i) Aliyekuwa miongoni mwa walioamini akatekeleza amali njema zilizotajwa juu, akaijenga imaan yake, akamtii Allaah na kufuata Amri Zake, akausiana na wenziwe katika kuvuta subira na kuusiana kuwahurumia viumbe na kuwatimizia haki zao. Hawa ndio watu wa kheri watakaopelekewa upande wa kulia kuelekea Peponi. (ii) Makafiri ambao hawakumwamini Allaah wala hawakutenda mema, wala hawakuwahurumia na kuwapa haki zao waja wa Allaah, bali walikanusha Aayaat, Ishara na Dalili za Allaah. Basi hawa watapelekwa upande kwa kushoto kuelekezwa katika Jahannam itakayowafunika na kuwaziba.  

 

 

 

Share