094-Ash-Sharh: Utangulizi Wa Suwrah

 

094-Ash-Sharh: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

Imeteremka: Makkah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.

 

Idadi Za Aayah: 8

 

Jina La Suwrah: Ash-Sharh

 

Suwrah imeitwa Ash-Sharh (Kukunjua), na inayodalilisha ni kutajwa kwake katika Aayah namba (1).

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Kuelezea neema ya Allaah (سبحانه وتعالى) kwa Nabiy (صلى الله عليه وسلم) kwa kutimiza Kwake Neema za kimaana. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Kubainisha Utukufu wa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) mbele ya Rabb Wake.

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

1-Suwrah imefunguliwa kwa kuliwazwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kwamba Allaah (سبحانه وتعالى) Amemkunjulia kifua chake kumtia utulivu na Nuru ya Allaah ili aweze kulingania watu Sharia za Dini, na aweze kujipamba kwa khulqa njema. Na kwamba Allaah (سبحانه وتعالى) Amemuodoshea mazito yaliyoelemea mgongoni mwake Akamsahilishia mambo yake. Akalitukuza jina lake awe anasifiwa na kutajwa Jina lake katika hali nyingi: (i) Katika kutamkwa Shahada watu wanaposilimu kuingia katika Dini hii tukufu. (ii) Katika Adhana na Iqaamah na katika Khutba. (iii) Ndani ya Swalaah (iv) Na kila anapotajwa (صلى الله عليه وآله وسلم), anaombewa Rehma na amani

 

2-Suwrah imekhitimishwa kwa kuendelea kumliwaza Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) aimarike katika kubalighisha Risala ya Allaah, wala asirudi nyuma kwa maudhi ya maadui wake, kwani kwenye dhiki kuna faraja. Na akaamrishwa ajitahidi katika ibaada na duaa anapomaliza mambo yake ya kidunia.

 

 

Share