093-Adhw-Dhwuhaa: Utangulizi Wa Suwrah

 

093-Adhw-Dhwuhaa: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

Imeteremka: Makkah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.

 

Idadi Za Aayah: 11

 

Jina La Suwrah: Adhw-Dhwuhaa

 

Suwrah imeitwa Adhw-Dhwuhaa (Dhuha), na inayodalilisha ni kutajwa kwake katika Aayah namba (1).

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Kubainisha kuwa Allaah Alimlinda Nabiy Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) kutoka mwanzo wa jambo lake hadi mwisho. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Kubainisha kuwa maisha ya Aakhirah ni bora kuliko ya dunia hii.  Na jinsi alivyoishi Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kama yatima na Allaah Akamtunza.

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

1-Suwrah imefunguliwa kwa Kiapo cha Allaah (سبحانه وتعالى) Kuapia wakati mchana jua linapopanda na kuenea mwanga wake. Na kuapia usiku unapotulia na giza lake likatanda. Ikatajwa jambo la kuhakikisha kiapo kumwambia Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kwamba Allaah Hakumchukia kwa kuchelewesha kumteremshia Wahy.   

 

2-Akaliwazwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kwa kujulishwa kwamba Aakhirah kwake ni bora kuliko dunia, na kwamba Allaah Atampa yatakayomridhisha, kwani alikuwa yatima Akamtunza, na alikuwa hajui Kitabu wala imaan Akamfundisha na akaweza kufanya mema. Na Alipokuwa masikini Allaah (سبحانه وتعالى) Alimjaalia rizki na Akamfanya atosheke na awe mwenye kuvuta subira.

 

3-Suwrah imekhitimishwa kwa amri ya kutokumkaripia yatima, bali kumtimizia haja zake. Na pia kuhadithia Neema za Allaah (سبحانه وتعالى).

 

 

Share