096-Al-‘Alaq: Utangulizi Wa Suwrah

 

096-Al-‘Alaq: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

Imeteremka: Makkah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.

 

Idadi Za Aayah: 19

 

Jina La Suwrah: Al-‘Alaq

 

Suwrah imeitwa Al-‘Alaq (Pande La Damu Linaloning’inia), na yanodalilisha ni kutajwa kwake katika Hadiyth zilizonukuliwa katika Fadhila, na pia kutajwa kwake pia katika Aayah namba (2).

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Kumuelezea mwanaadam kati ya kuongoka kwake kupitia Wahy, na kupotoka kwake kupitia kiburi na ujahili. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Kumthibitisha Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) na kumtishia kila mwenye kuipinga Risala ya Allaah na kumfanyia uadui Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم).    

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

1-Suwrah imefunguliwa kwa kuamrishwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) asome Qur-aan ilipoanza kuteremshwa mara ya kwanza kwake, pindi alipojitenga mbali na watu akawa katika pango la Hiraa akimwabudu Allaah. Akaamrishwa asome. Naye akajibu: “Mimi sijui kusoma.” Akaamrishwa asome kwa Jina la Rabb wake Aliyemuumba, na Aliyemuumba binaadam kwa pande la damu linaloning’inia, na kwamba Rabb wake ni Mwingi wa Ukarimu, Ihsaan na Wema, na Ambaye Amefundisha wanaadam kwa kalamu, Akawafundisha mambo ambayo hawakuwa wanayajua, kwani wamezaliwa kutoka matumbo ya mama zao hawakuwa wana ujuzi wa lolote, kisha Akawajaaliwa Nuru za ilimu.

 

2-Akaonywa binaadam aliyedhania kuwa ametosheka kwa utajiri wake, akavuka mipaka kumkanusha Muumba wake kwamba, mwisho wake ni kurudia kwa Rabb wake aliyemuumba.

 

3-Allaah (سبحانه وتعالى) Amemliwaza Rasuli Wake Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kwamba, Yeye ni Mwenye kujua yale wanayompangia njama maadui zake. Na hii amekusudiwa Abu Jahl, laana ya Allaah iwe juu yake, kwani aliazimia kwa kuapia masanamu yao kuwa atausigina uso wa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) atakaposwali mbele ya Al-Ka’bah. Lakini Allaah (سبحانه وتعالى) Alimtisha kwa kumfanya aone mbele yake kuna khandaqi (shimo) la moto na Malaika waliokuwa wamekaa kidete kumwangamiza Abu Jahl. Basi Allaah (سبحانه وتعالى) Akamdhalilisha Abu Jahl na Akamnusuru Nabiy Wake (صلى الله عليه وآله وسلم), na Akaahidi kumuingiza Abu Jahl motoni kwa paji lake la uso lenye sifa ya uongo, kukadhibisha na madhambi ikiwa ataendelea kumfanyia uadui Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم). Na Akamtishia awaite wasaidizi wake wamsaidie, na Allaah Ataita Malaika Wake wenye kuadhibu vikali.  Basi  kwa vile Abu Jahl aliendelea kumfanyia uaudi Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم), aliuwawa katika Vita vya Badr kwa namna ya kudhalilishwa kabisa, kwani baada ya kujeruhiwa, Ibn Mas’uwd (رضي الله عنه) alimwendea na kumkata kichwa chake na kukipeleka kwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم). Basi akastahiki kuingizwa motoni.  

 

4-Suwrah imekhitimishwa kwa Amri ya Allaah (سبحانه وتعالى) kwa Nabiy Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) asimtii kafiri yeyote, na aendelee katika kubalighisha Risala ya Allaah, na aswali na ajikurubishe kwa Rabb wake.

 

Fadhila Za Suwrah:

 

1-Aayah Tano Za Mwanzo Ni Za Kwanza Kuteremshiwa Wahy Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم):  

 

عَنْ عَائِشَةَ أُمِّ الْمُؤْمِنِينَ، أَنَّهَا قَالَتْ أَوَّلُ مَا بُدِئَ بِهِ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم مِنَ الْوَحْىِ الرُّؤْيَا الصَّالِحَةُ فِي النَّوْمِ، فَكَانَ لاَ يَرَى رُؤْيَا إِلاَّ جَاءَتْ مِثْلَ فَلَقِ الصُّبْحِ، ثُمَّ حُبِّبَ إِلَيْهِ الْخَلاَءُ، وَكَانَ يَخْلُو بِغَارِ حِرَاءٍ فَيَتَحَنَّثُ فِيهِ ـ وَهُوَ التَّعَبُّدُ اللَّيَالِيَ ذَوَاتِ الْعَدَدِ قَبْلَ أَنْ يَنْزِعَ إِلَى أَهْلِهِ، وَيَتَزَوَّدُ لِذَلِكَ، ثُمَّ يَرْجِعُ إِلَى خَدِيجَةَ، فَيَتَزَوَّدُ لِمِثْلِهَا، حَتَّى جَاءَهُ الْحَقُّ وَهُوَ فِي غَارِ حِرَاءٍ، فَجَاءَهُ الْمَلَكُ فَقَالَ اقْرَأْ‏.‏ قَالَ ‏"‏ مَا أَنَا بِقَارِئٍ"‏‏.‏ قَالَ ‏"‏ فَأَخَذَنِي فَغَطَّنِي حَتَّى بَلَغَ مِنِّي الْجَهْدَ، ثُمَّ أَرْسَلَنِي فَقَالَ اقْرَأْ‏.‏ قُلْتُ مَا أَنَا بِقَارِئٍ‏.‏ فَأَخَذَنِي فَغَطَّنِي الثَّانِيَةَ حَتَّى بَلَغَ مِنِّي الْجَهْدَ، ثُمَّ أَرْسَلَنِي فَقَالَ اقْرَأْ‏.‏ فَقُلْتُ مَا أَنَا بِقَارِئٍ‏.‏ فَأَخَذَنِي فَغَطَّنِي الثَّالِثَةَ، ثُمَّ أَرْسَلَنِي فَقَالَ ‏‏اقْرَأْ بِاسْمِ رَبِّكَ الَّذِي خَلَقَ * خَلَقَ الإِنْسَانَ مِنْ عَلَقٍ * اقْرَأْ وَرَبُّكَ الأَكْرَمُ ‏"‏‏.‏ فَرَجَعَ بِهَا رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم يَرْجُفُ فُؤَادُهُ، فَدَخَلَ عَلَى خَدِيجَةَ بِنْتِ خُوَيْلِدٍ رضى الله عنها فَقَالَ ‏"‏ زَمِّلُونِي زَمِّلُونِي ‏"‏‏.‏ فَزَمَّلُوهُ حَتَّى ذَهَبَ عَنْهُ الرَّوْعُ...

 

Amesimulia ‘Aaishah Mama wa Waumini (رضي الله عنها): Wahyi kwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) ulianza kwa ndoto njema usingizini na alikuwa haoni ndoto isipokuwa ni kweli kama ulivyo mwanga wa mchana, na alipendezeshwa kujitenga. Alikuwa akijitenga ndani ya pango la Hiraa akimwabudu (Allaah Pekee) mfululizo kwa siku nyingi kabla ya kwenda kwa familia yake. Na anachukua chakula cha safari cha kutosha, na kisha alirejea kwa (mkewe) Khadiyjah (رضي الله عنها) kuchukua chakula tena mpaka ukweli ulishukia alipokuwa ndani ya pango la Hiraa. Malaika alimjia na alimtaka asome. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) Akajibu: “Mimi sio msomaji.” Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akaendelea kusema: “Malaika akanishika kwa nguvu na akaniminya kwa nguvu mpaka nikapata tabu. Kisha aliniachia, na tena akanitaka nisome na nikamjibu: Mimi si msomaji. Baada ya hapo akanishika tena akaniminya kwa mara ya pili mpaka nikapata taabu. Kisha akaniachia akasema:

 

اقْرَأْ بِاسْمِ رَبِّكَ الَّذِي خَلَقَ ﴿١﴾ خَلَقَ الْإِنسَانَ مِنْ عَلَقٍ ﴿٢﴾ اقْرَأْ وَرَبُّكَ الْأَكْرَمُ ﴿٣﴾

“Soma kwa Jina la Rabb wako Aliyeumba. Amemuumba mwana Aadam kutokana na pande la damu linaloning’inia. Soma na Rabb wako ni Mkarimu kushinda wote.” [Al-‘Alaq: (1-3)] Na kuendelea hadi Aayah namba (5).

 

Kisha Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alirejea na Wahy, na huku moyo ukidunda kwa nguvu. Kisha alikwenda kwa Khadiyjah bint Khuwaylid (رضي الله عنها) akasema: “Nifunikeni! Nifunikeni!” Wakamfunika mpaka khofu ikatoweka…[Al-Bukhaariy]

 

2-Swahaba Walisujudu Pamoja Na Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) Pindi Aliposoma Suwrah Hii:

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ، قَالَ سَجَدْنَا مَعَ النَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم فِي إِذَا السَّمَاءُ انْشَقَّتْ ‏ وَ اقْرَأْ بِاسْمِ رَبِّكَ

 

Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه): Tulisujudu pamoja na Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) pindi aliposoma:   

إِذَا السَّمَاءُ انشَقَّتْ ﴿١﴾

“Mbingu itakaporaruka.” [Al-Inshiqaaq (84)]

 

Na

اقْرَأْ بِاسْمِ رَبِّكَ  

“Soma kwa Jina la Rabb wako,” [Al-‘Alaq (96)]

[Al-Bukhaariy, Muslim na wengineo]

 

 

Share