100-Al-‘Aadiyaat: Utangulizi Wa Suwrah

 

100-Al-‘Aadiyaat: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

Imeteremka: Makkah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.

 

Idadi Za Aayah: 11

 

Jina La Suwrah: Al-‘Aadiyaat

 

Suwrah imeitwa Al-‘Aadiyaat (Waendao Mbio Za Kasi), na inayodalilisha ni kutajwa kwake katika Aayah namba (1).

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Kumpa tahadhari mwanaadam ya kutokuwa na tamaa na ukaidi, kwa kumkumbusha Aakhirah. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Kutahadhrishwa mwanaadam kutoa haki za mali anayoruzukiwa na kukumbuka kwamba Allaah (سبحانه وتعالى) Ni Mjuzi wa matendo yote na yatahesabiwa Siku ya Qiyaamah.

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

1-Suwrah imefunguliwa kwa Kiapo cha Allaah (سبحانه وتعالى) Kuapia farasi,  ambao ni neema mojawapo kwa wanaadam, kwa sababu ya kutumika na kufaa mno katika kupigana Jihaad. Farasi hao wanakimbia kwa mwendo kasi katika kumkabili adui wakitoa sauti kutokana na kasi ya kukimbia. Na kuapia kwa farasi wanaotoa cheche za moto kwa kwato zao ngumu wanapokimbia kwa kasi, wenye kushambulia maadui kipindi cha asubuhi, na wakarusha vumbi kutokana na mbio za kasi. Likawa vumbi limewagubika maadui kwa vipando vyao, hata wakaingiwa kiwewe na kufazaika. Kisha ikafuatia uthibitisho wa kiapo kwamba, hakika binaadam ni mkanushaji mno wa Neema za Rabb wake, kwa kutokutoa haki anazopaswa kama Zakaah na swadaqa. Na kwamba Allaah Anashuhudia hayo. Au huyo binaadam bakhili atakuja kushudia hayo mwenyewe Siku ya Qiyaamah. Na kwamba binaadam huyo ni mpenda mno wa mali na ni mwenye kuipupia, hadi aache kutoa haki apasazo kuzitoa, kwa sababu ya kughafilika kwake na Aakhirah.

 

2-Kisha anaulizwa huyo binaadam aliyekosa shukurani kwa Neema za Allaah kwamba, kwani hajui linalomngojea mbele yake, pindi Allaah (سبحانه وتعالى) Atakapowatoa wafu makaburini waende kuhesabiwa na kulipwa? Na kwamba yatafichuliwa yaliyomo vifuani, mema na maovu?

 

3-Suwrah imekhitimishwa kwa uthibitisho kwamba Allaah (سبحانه وتعالى) Ni Mjuzi wa dhahiri na siri kwa kila wanachokifanya waanaadam, na kwamba Atawafanyia hesabu ya matendo yao Siku ya kufufuliwa.   

 

 

 

 

 

Share