101-Al-Qaari’ah: Utangulizi Wa Suwrah

 

101-Al-Qaari’ah: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

Imeteremka: Makkah

 

Idadi Za Aayah: 11

 

Jina La Suwrah:  Al-Qaari’ah

 

Suwrah imeitwa Al-Qaari’ah (Janga Kuu Linalogonga), na inayodalilisha ni kutajwa kwake katika Aayah namba (1-3).

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Kuzishtua nyoyo kwa kuzielezea vitisho vya Siku ya Qiyaamha, na hali za watu katika mizani zao (wakati wa kupimwa matendo yao). [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Kutanabahisha tisho la tukio kubwa mno la Siku ya Qiyaamah, na amali za aina mbili katika mizani; za watakaofaulu na za watakaokula khasara.   

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

1-Suwrah imefunguliwa kwa kutajwa mojawapo wa Jina la Siku ya Qiyaamah, nalo ni Al-Qaari’ah ambalo ni tukio linalogongagonga hadi likawafazaisha watu kutokana na tishio lake. Na ikafuatilia swali la kuulizia nini Al-Qaari’ah? Kisha ikaja jibu lake la kuelezea hali za watu na milima itakavyokuwa. Kwa vile kutakuwa na halaiki kubwa ya watu, basi kugawanyika kwao na kuzunguka kwao, ni kama panzi walioenea. Nao ni wale wanaojitupa motoni. Na milima itakuwa kama pamba yenye rangi tofauti inayochambuliwa.

 

2-Suwrah ikakhitimishwa kwa kubainisha hali mbili za mizani za watu; mizani za watu ambao mema yao yamekuwa mazito katika mizani. Hawa ndio watakaopata maisha ya kuridhika Peponi. Mizani ya pili ni za watu ambao maovu yao ni mengi mno katika mizani. Basi hawa makazi yao yatakuwa ni katika moto unaoitwa Haawiyah ambao unawaka mno kwa kuni zilizomo ndani yake.

 

 

 

 

 

Share