105-Al-Fiyl: Utangulizi Wa Suwrah

 

105-Al-Fiyl: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

Imeteremka: Makkah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.

 

Idadi Za Aayah: 5

 

Jina La Suwrah: Al-Fiyl

 

Suwrah imeitwa Al-Fiyl (Tembo), na inayodalilisha ni kutajwa kwake katika Aayah namba (1).

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Kubainisha Uwezo wa Allaah (سبحانه وتعالى) na Nguvu Zake juu ya wale wanaoifanyia vitimbi Nyumba Yake Tukufu (Al-Ka’bah). [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Kubainisha uovu watu wa tembo na maangamizi yao.

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

Suwrah imefunguliwa kwa swali kumwelekea Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kumuuliza: Hivi hukuona jinsi Allaah Alivyowafanya watu wa tembo, Abraha Mhabeshi na jeshi lake kubwa kutoka Habasha na Yemen,  kukusudia kuishambulia Nyumba ya Allaah (Al-Ka’bah)? Na Allaah Hakujaalia njama zao zifeli na zipite patupu? Jeshi hilo kubwa lilipofika karibu na Makkah, Waarabu hawakuwa na nguvu na ulinzi wa kujihami, basi wakakimbia kwa kuhofia maisha yao. Kisha Allaah Akawasalitisha watu wa tembo, kwa ndege waliofuatana makundi kwa makundi yakawazunguka kila upande, wakiwatupia vijiwe vya udongo mkavu mgumu uliookwa motoni, Akawapondaponda wakawa kama majani makavu yaliyoliwa na wanyama kisha kutupwa.

 

Na hiki ni kisa maarufu cha tembo, kilichotokea mwaka aliozaliwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم), ukajulikana mwaka humo kama 'Aamul-Fiyl (Mwaka wa Tembo). 

 

 

 

 

 

Share