110-An-Naswr: Utangulizi Wa Suwrah

 

110-An-Naswr: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

Imeteremka: Madiynah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.

 

Idadi Za Aayah: 3

 

Jina La Suwrah: An-Naswr

 

Suwrah imeitwa An-Naswr (Nusura), na inayodalilisha ni kutajwa kwake katika Aayah namba (1).

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Bishara kwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) juu ya ushindi unaokuja na mwisho wa Unabiy. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Kufahamisha kukamilika kwa Dini ya Kiislamu kwa kubashiriwa nusura na ushindi wa Makkah.

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

Suwrah imefunguliwa kwa bishara na Ahadi ya Allaah (سبحانه وتعالى) kwa Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) ya ushindi juu ya ukafiri wa Maquraysh na Fat-h (Ufunguzi wa) Makkah. Na bishara ya makundi kwa makundi ya watu kuingia katika Dini ya Uislamu. Na Suwrah ikakhitimishwa kwa kumuamrisha Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) ashikamane na Tasbiyh (Kumtakasa Allaah) na Tahmiyd (Kumhimidi Allaah), na Istighfaar (Kuomba Maghfirah).   

 

Fadhila Za Suwrah:

 

Ni Suwrah Ya Mwisho Iliyoteremshwa Kamili:

 

عَنْ عُبَيْدِ اللَّهِ بْنِ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ عُتْبَةَ، قَالَ قَالَ لِيَ ابْنُ عَبَّاسٍ تَعْلَمُ - وَقَالَ هَارُونُ تَدْرِي - آخِرَ سُورَةٍ نَزَلَتْ مِنَ الْقُرْآنِ نَزَلَتْ جَمِيعًا قُلْتُ نَعَمْ ‏.‏إِذَا جَاءَ نَصْرُ اللَّهِ وَالْفَتْحُ‏ ‏ قَالَ صَدَقْتَ ‏.‏ وَفِي رِوَايَةِ ابْنِ أَبِي شَيْبَةَ تَعْلَمُ أَىُّ سُورَةٍ ‏.‏ وَلَمْ يَقُلْ آخِرَ ‏.‏

Amesimulia ‘Ubaydullaah Bin ‘Abdillaah Bin ‘Utbah (رضي الله عنه): Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) ameniambia: Je unajua- na katika maneno ya Haaruwn (msimulizi mwengine): “Unajua Suwrah ya mwisho ya Qur-aan kuteremka ikiwa kamili?” Nikajibu: Naam.

 

إِذَا جَاءَ نَصْرُ اللَّـهِ وَالْفَتْحُ ﴿١﴾

“Itakapokuja Nusura ya Allaah na ushindi.”

 

Akasema: Umesema kweli. Na katika usimulilzi wa Abu Shaybha (maneno yalikuwa): “Je unajua Suwrah gani.” Lakini hakutaja “Ya mwisho.” [Muslim]

 

 

 

Share