092-Al-Layl: Utangulizi Wa Suwrah

 

092-Al-Layl: Utangulizi Wa Suwrah

 

Alhidaaya.com

 

 

Imeteremka: Makkah kwa itifaki ya ‘Ulamaa.

 

Idadi Za Aayah: 21

 

Jina La Suwrah: Al-Layl

 

Suwrah imeitwa Al-Layl (Usiku), na inayodalilisha ni kutajwa kwake katika Aayah namba (1).

 

Miongoni Mwa Makusudio Ya Suwrah:

 

1-Kubainisha hali ya viumbe katika imaan na kutoa (mali kwa ajili ya Allaah) na hali ya kila kundi. [Al-Mukhtaswar Fiy Tafsiyr Al-Qur-aan Al-Kariym]

 

2-Kubainisha umbali kati ya hali ya Waumini na makafiri katika dunia na Aakhirah.

 

Miongoni Mwa Maudhui Ya Suwrah:

 

1-Suwrah imefunguliwa kwa Kiapo cha Allaah (سبحانه وتعالى) Kuapia usiku unapofunika ardhi kwa giza lake pamoja na vilivyomo ardhini. Na giza hilo ni manufaa kwa wanaadam kupata utulivu na kupumzika baada ya tabu za mihangaiko ya mchana. Na Kuapia mchana unapodhihiri mwangaza wake ili watu waangazwe na nuru yake, waweze kutoka nje na kutafuta wanayoyahitajia katika maisha yao. Na Kuapia kuumbwa kila kinachozaliwa kuwa viwili viwili; dume na jike katika wanaadam na wanyama. Hivi ni kutokana na Hikma Yake ili watamaniane na wanufaishane katika uhai wa dunia. Na hali kadhalika kuumbwa dume na jike katika mimea na vinginevyo. Kisha ikatajwa jambo linaloapiwa, kwamba kwa matendo ya wanaadam yametofautiana. Kuna wanaotenda ya kheri kwa ajili ya Aakhirah, na wako wanaotenda ya shari.

 

2-Imebainishwa Utukufu wa Muumini na fadhila za kutoa mali katika Anayoyaamrisha Allaah (سبحانه وتعالى) kama kutoa Zakaah, swadaqa, kuwapa jamaa wenye uhusiano wa damu na wahitaji wengineo. Na pia imebainishwa fadhila za kumcha Allaah, kwa kutekeleza aliyokatazwa na kujiepusha na makatazo, na kutimiza ibaada za fardhi na za Sunnah, na kuamini neno la Tawhiyd; laa ilaaha illa-Allaah. Huyu fadhila zake itakuwa ni kufanyiwa sahali mambo yake katika kumwongoza kutenda ya kheri na kumwepusha na maovu. Ama anayefanyia ubakhili mali yake asitoe katika Aliyoamrisha Allaah, na akawa hana haja na malipo Yake, na akakanusha laa ilaaha illa-Allaah, basi huyo atafanyiwa njia za kutenda maovu apate mashaka ya kudumu.  

 

3-Wanaadam wameonywa moto wa Jahannam wenye kuwaka vikali, ambao wataingia waliokataa kumwamini na kumtii Allaah na Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم). Na ataepushwa na moto wa Jahannam aliyemwamini na kumtii pamoja na Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم).

 

4-Suwrah imekhitimishwa kwa kusifiwa Muumini anayejitakasa kwa kutoa mali yake kutaja Wajihi wa Allaah. Basi huyu atapata malipo ya kumridhisha.    

 

 

Share