03-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Mavazi Na Mapambo Na Hukmu Za Kuangalia: Hukumu Za Kuangalia: Hali Ambazo Mwanaume Anaruhusiwa Kumwangalia Mwanamke

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ اللِّبَاسِ وَالزِّيْنَةِ  وَأَحْكَامُ النَّظَرِ

 

 Kitabu Cha Mavazi Na Mapambo Na Hukmu Za Kuangalia 

  

أَحْكَامُ النَّظَرِ

Hukumu Za Kuangalia 

  

Alhidaaya.com 

 

 

03-Hali Ambazo Mwanaume Anaruhusiwa Kumwangalia Mwanamke:

 

1-  Kuposa:  ‘Ulamaa wamekubaliana wote kwamba ni halali kwa mwanaume kumwangalia mwanamke ambaye anataka kumwoa.  Na hikma ya hilo, ni kumfanya mume mtarajiwa awe na picha kamili ya mkewe mtarajiwa, asije kujuta kama atavamia tu akaoa, kisha akakuta mambo si kama alivyotarajia.  Na kama posa yake itakubaliwa, basi ataoa kwa hamu, shauku na mapenzi.  Mwanaume mwenye busara, haingii kichwa kichwa sehemu yoyote mpaka imbainikie kheri yake na shari yake kabla ya kuingia.

 

2-  Kutibu:  Kimsingi, mwanamke hatibiwi ila na mwanamke mwenzake.  Lakini pamoja na hivyo, hakuna makhitilafiano baina ya ‘Ulamaa juu ya kujuzu mwanaume kumtibu mwanamke na kuangalia sehemu yenye ugonjwa kama italazimika lakini kwa vidhibiti maalum.

 

Sambamba na hilo, mwanamke asiye maharimu anaruhusiwa kumtibu mwanamume katika hali ya dharura. 

 

Ar-Rubayyi’u bin Mu’awwidh amesema: 

 

"كُنَّا نَغْزُو مَعَ رَسُولِ اللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ نَسْقِي الْقَوْمَ، وَنَخْدُمُهُمْ، وَنَرُدُّ الْقَتْلَى وَالْجَرْحَى إِلَى الْمَدِينَةِ"

 

“Tulikuwa tunakwenda vitani pamoja na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kazi yetu ilikuwa kuwapatia maji wanaume, kuwahudumia, na kuwarejesha Madiynah waliouawa na majeruhi”.  [Swahiyh Al-Bukhaariy (2883)]

 

Lakini pamoja na ruksa hiyo, haifai kutanua na kuachilia katika jambo hili kama tunavyoshuhudia hivi leo.  ‘Ulamaa wametaja vidhibiti vya kuruhusiwa daktari mwanaume kumtibu mwanamke.  Vidhibiti hivyo ni:

 

1-  Kama yuko daktari mwanamke, ni sharti yeye atangulizwe kabla ya daktari wa kiume na hususan ikiwa upimaji na ukaguzi unahusiana na sehemu nyeti za uchi mzito.  Ikiwa hakupatikana daktari mwanamke au ikawa haiwezekani kumwendea, basi hapo itakuwa ni dharura mwanamume kutibu.

 

2-  Daktari awe mwaminifu, asiwe na tuhuma yoyote ya uchafu katika tabia yake wala dini yake.

 

3-  Daktari asivuke mpaka wa kutosheleza dharura katika kuangalia, kupima kugusa na kadhalika.  Ni lazima daktari huyu afunike sehemu zote za mwili wa mgonjwa zisizohitajika kuangaliwa.  Inatosha tu kuangalia sehemu husika ya kutibiwa.

 

4-  Kutibiwa kuwe kunahitajika sana kama kuwa mgonjwa hasa, au awe anakabiliwa na maumivu yasiyovumilika, au awe anahofiwa kudhoofu na kudorora afya.  Ama ikiwa si ugonjwa au hali ya dharura inayohitajia kufanyiwa dawa, basi haijuzu kabisa.  Ni kama mwanamke kwenda kwa daktari wa kiume ili kuboresha afya yake, au kupunguza uzito, au kutengeneza na kurembesha mwili wake.  Haya hayako ndani ya wigo wa haja.

 

 

Share