08-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Mavazi Na Mapambo: Pambo Kwa Mwanamke Wa Kiislamu: Kutumia Mafuta Mazuri Yenye Mchanganyo Wa Alcohol (Cologne)

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ اللِّبَاسِ وَالزِّيْنَةِ 

Kitabu Cha Mavazi Na Mapambo

 

 

الزِّيْنَةُ للمَرْأَةِ المُسْلِمَةِ

Pambo Kwa Mwanamke Wa Kiislamu

 

Alhidaaya.com

 

 

08- Kutumia Mafuta Mazuri Yenye Mchanganyo Wa Alcohol (Cologne)

 

Harufu nyingi za mafuta mazuri zijulikanazo kama “cologne” au “paravan” zinakuwa na mchanganyo wa mada ya alcohol (Ethil).  Imethibiti toka kwa madaktari wenye uzoefu na utaalamu kwamba mada hii inalewesha, na kwa mintarafu hiyo, hairuhusiwi kutumia katika manukato kutokana na Kauli Yake Ta’aalaa:

 

"يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِنَّمَا الْخَمْرُ وَالْمَيْسِرُ وَالْأَنصَابُ وَالْأَزْلَامُ رِجْسٌ مِّنْ عَمَلِ الشَّيْطَانِ فَاجْتَنِبُوهُ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ"

 

“Enyi walioamini!  Hakika pombe na kamari na masanamu na kutazamia kwa mishale ya kupigia ramli, ni najisi na chukizo kutokana na kazi ya shaytwaan.  Basi jiepusheni navyo, mpate kufaulu”.   [Al-Maaidah: 90]

 

Allaah Ta’alaa Ameiita pombe najisi na Akaamuru kuiepuka.  Katazo hili la kujiepusha nayo ni jumuishi, kwa maana kwamba hairuhusiwi kunufaika na chochote chenye kulewesha.  Na hii ndiyo sababu ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuamuru pombe imwagwe baada ya kushuka Aayah ya kuiharamisha.  Na lau kama kungelikuwa na manufaa ndani yake, basi Rasuli angebainisha na asingeliamuru imwagwe kama alivyobainisha ruhusa ya kunufaika na ngozi ya mnyama mfu.

 

Baadhi ya ‘Ulamaa wameruhusu kutumia mafuta haya ikiwa kiwango cha alcohol ni kidogo, na hii itategemea maelezo ya wataalamu wa nyanja hii.  Lakini kiakiba ni bora kutoyatumia, au kutumia yasiyo na mchanganyo wa alcohol.  Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi.

 

 

Share