16-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Mavazi Na Mapambo: Pambo Kwa Mwanamke Wa Kiislamu: Tojo (Tattoo) Ni Haramu

 

 Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ اللِّبَاسِ وَالزِّيْنَةِ 

Kitabu Cha Mavazi Na Mapambo

 

 

الزِّيْنَةُ للمَرْأَةِ المُسْلِمَةِ

Pambo Kwa Mwanamke Wa Kiislamu

 

Alhidaaya.com

 

 

16-Tojo (Tattoo) Ni Haramu:

 

Ibn Mas-‘uwd (Radhwiya Allaah ‘anhu) amesema:  “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"لَعَنَ اللَّهُ الْوَاشِمَاتِ وَالْمُسْتَوْشِمَاتِ، والنَّا مِصَاتِ وَالْمُتَنَمِّصَاتِ، وَالْمُتَفَلِّجَاتِ لِلْحُسْنِ، الْمُغَيِّرَاتِ خَلْقَ اللَّهِ"

 

“Allaah Amewalaani wanawake wenye kuwafanyia tattoo wengine na wenye kufanyiwa, na wenye kuwachonga nyusi wenzao na wenye kuchongwa, na wenye kupasua mwanya wa meno ili waonekane wazuri, hao ni wenye kubadili uumbaji wa Allaah”.  [Al-Bukhaariy (4886) na Muslim (2125)]

 

Tojo kwa kawaida hufanywa kwa kuingiza sindano au mfano wake kwenye mgongo wa kiganja, au mdomo, au sehemu yoyote ya mwili wa mwanamke mpaka damu ikachuruzika, kisha mahala kusudiwa hujazwa hina au mfano wake mpaka pakawa kijani.  Tojo hii athari yake inabakia, na haiondoki kwa kuosha au kupita wakati.  Na kwa ajili hiyo, imekuwa ni haramu kwa mtendaji na mtendewa aliyetaka kwa hiari yake. Na anayemfanyia hivyo binti mdogo anapata yeye madhambi, lakini binti hapati kwa kuwa bado hajavunja ungo.

 

Hivi leo pameenea mtindo mpya kwa wasichana wa kuchorwa tojo kwenye kifua na tumbo.  Wakati wa kuchorwa, mchoraji ni lazima afunuliwe sehemu hizo ambaye anaweza pia kuwa mwanaume kwenye masaluni ambayo baadhi yake yametenga chumba maalum cha kazi hiyo na kwa bei za juu kabisa!!  Kama hiyo haitoshi, akitoka hapo, msichana huanika wazi sehemu hizo kwa watu ili waone michoro hiyo.  Haya ndiyo mambo!!

 

Angalizo:

 

Ingawa Hadiyth ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) imewalenga wanawake tu, lakini pia hata kwa wanaume ni haramu kuchora tattoo.  Kwa kuwa wanawake maumbile yao ni kujipamba na kujiremba, na maumbile hayo yamewapeleka hadi kufikia kwenye tattoo.  Na mwanaume akifanya hilo, bila shaka itakuwa ni mbaya zaidi.

 

Faida:  Athari Mbaya Za Kitiba Za Kuchora Tojo Kwenye Ngozi:

 

Bingwa wa magonjwa ya ngozi na uzazi Dk. ‘Abdul Haadiy Muhammad ‘Abdul Ghaffaar anasema kwamba mada ngeni ambazo zinaingia ndani ya ngozi husababisha aleji ya ngozi.  Na kama mada hizo zitakuwa na mchanganyiko wa petroli, basi zitasababisha saratani ya ngozi na hatimaye ngozi itapoteza uhai wake.  Na utumiaji wa sindano katika kuweka tojo husababisha maambukizi ya homa ya ini (hepatitis) na ukimwi ikiwa itatumiwa na zaidi ya mtu mmoja. 

 

Angalizo:

 

Siku hizi pameibuka aina nyingine ya tojo ambayo huchorwa kwenye ngozi mfano wa hina, lakini hii inaweza kutoka kwa usahali.  Hii kama haina madhara kwa ngozi, basi haina ubaya, kwa kuwa si ugeuzaji wa uumbaji wa Allaah, bali ni kama hina tu, lakini mwanamke anatakiwa asiruhusu kuonwa na yeyote zaidi ya mumewe ingawa kuacha inakuwa ni akiba zaidi ili awe mbali na kujifananisha na wanawake waliolaaniwa kwenye Hadiyth. 

 

 

Share