17-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Mavazi Na Mapambo: Pambo Kwa Mwanamke Wa Kiislamu: Hukmu Ya “Plastic Surgery”

 

 Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ اللِّبَاسِ وَالزِّيْنَةِ 

Kitabu Cha Mavazi Na Mapambo

 

 

الزِّيْنَةُ للمَرْأَةِ المُسْلِمَةِ

Pambo Kwa Mwanamke Wa Kiislamu

 

 

Alhidaaya.com

 

17-Hukmu Ya “Plastic Surgery”:

 

“Plastic Surgery” ina hali mbalimbali.  Baadhi yake zinaruhusiwa, kuna ambazo ni lazima, na nyingine ni haramu.

 

1-  Zinazoruhusiwa ni kama kuziba jeraha la kina kirefu, kukarabati jeraha lililopasuka, na kutia kiraka sehemu iliyoungua vibaya na hususan uso au sehemu za mwili zinazoonekana zaidi.  Upasuaji wote huu unaingia ndani ya duara la kutengeneza kilichoharibika na kurejesha umbile la asili katika mwili.  Haya yote hayana ubaya, bali baadhi yake yanaweza kuwa ni waajib.

 

2-  Kuondosha kasoro ambazo huenda zikawa zimetokea wakati wa ujauzito kutokana na mjamzito kutumia madawa au vinginevyo.  Pia kuondosha kilicho kinyume na maumbile ya kawaida kama kidole cha sita na mfano wake.  Haya tunataraji kwamba hayana ubaya kwa kuwa hayaingii kwenye duara la kubadili uumbaji wa Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa.

 

3-  Kila linaloingia kwenye duara la kubadili uumbaji wa Allaah linakuwa ni haramu.  Allaah Ta’aalaa Ameumba watu wakiwa wametofautiana.  Ameumba warefu, wafupi, weusi, weupe, wazuri na wabaya wa sura.  Haya yote ni katika alama za kupwekeka Kwake na ubunifu Wake.  Yeye Ndiye Mola Mwenye Kutia sura kama Alivyosema: 

 

 "هُوَ الَّذِي يُصَوِّرُكُمْ فِي الْأَرْحَامِ كَيْفَ يَشَاءُ ۚ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ "

Yeye Ndiye Anayekusawirini umbo katika matumbo ya uzazi vile Atakavyo. Hapana mwabudiwa wa haki ila Yeye, Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye hikmah wa yote.  [Aal ‘Imraan: 06]

 

Na hakuna shaka kwamba kukiuka uumbaji wa Allaah kwa kubadili sura, au rangi, au umbo, kunaingia kwenye duara la kuingilia uumbaji wa Allaah ‘Azza wa Jalla.  Hilo Amelikataza Aliposema:

 

"لَا تَبْدِيلَ لِخَلْقِ اللَّـهِ"

“Hakuna kubadilisha Uumbaji wa Allaah”.  [Ar-Ruwm: 30]

 

Sehemu hii ya Aayah ni agizo, kwa maana kwamba msibadili uumbaji wa Allaah.  Na Allaah Ashatujulisha kwamba ibliys atamwamuru mwanadamu abadili uumbaji wa Allaah pale Aliposema:

 

"إِن يَدْعُونَ مِن دُونِهِ إِلَّا إِنَاثًا وَإِن يَدْعُونَ إِلَّا شَيْطَانًا مَّرِيدًا ﴿١١٧﴾ لَّعَنَهُ اللَّـهُ ۘ وَقَالَ لَأَتَّخِذَنَّ مِنْ عِبَادِكَ نَصِيبًا مَّفْرُوضًا ﴿١١٨﴾ وَلَأُضِلَّنَّهُمْ وَلَأُمَنِّيَنَّهُمْ وَلَآمُرَنَّهُمْ فَلَيُبَتِّكُنَّ آذَانَ الْأَنْعَامِ وَلَآمُرَنَّهُمْ فَلَيُغَيِّرُنَّ خَلْقَ اللَّـهِ ۚ وَمَن يَتَّخِذِ الشَّيْطَانَ وَلِيًّا مِّن دُونِ اللَّـهِ فَقَدْ خَسِرَ خُسْرَانًا مُّبِينًا ﴿١١٩﴾"

 

“Hawaombi badala Yake isipokuwa miungu ya kike na hawaombi isipokuwa shaytwaan muasi    Allaah Amemlaani. Na (shaytwaan) akasema: Kwa hakika nitashika katika waja Wako sehemu maalumu  ●  Na hakika nitawapoteza, na nitawashawishi matamanio ya kulaghai, na nitawaamrisha. Basi watakata masikio ya wanyama (wawatukuze), na nitawaamrisha watabadili Uumbaji wa Allaah. Na atakayemfanya shaytwaan kuwa rafiki mwandani badala ya Allaah basi kwa yakini amekhasirika khasara bayana.  [An-Nisaa: 117-119]

 

Na kati ya kazi za shaytwaan za kumpoteza mwanadamu ni kumwamuru abadili umbile la Allaah.

 

Na hakuna shaka yoyote kwamba operesheni ambazo zinalenga kubadili uumbaji wa Allaah kama kubadili jinsia ya mwanaume kuwa mwanamke na kinyume chake, au kubadilisha rangi (kama kujichubua n.k), au kubadilisha sura ya uso au kiungo chochote cha mwili, hayo yote ni matendo ya kumfuata shaytwaan ambaye kazi yake ni kumpoteza mwanadamu na kumchochea akiuke uumbaji wa Allaah kwa kuubadilisha na kuugeuza.

 

Hadiyth ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) imeyaainisha kwa uwazi baadhi ya mambo ya ubadilishaji uumbaji wa Allaah.  Kati ya mambo hayo ni kuchonga meno kwa kuweka mwanya kati ya jino na jino, kuunganisha nywele, kuchonga nyusi zikawa nyembamba, na kuchora tattoo.  Ni pale aliposema:

 

"لَعَنَ اللَّهُ الْوَاشِمَاتِ وَالْمُسْتَوْشِمَاتِ، والنَّا مِصَاتِ وَالْمُتَنَمِّصَاتِ، وَالْمُتَفَلِّجَاتِ لِلْحُسْنِ، الْمُغَيِّرَاتِ خَلْقَ اللَّهِ"

“Allaah Amewalaani wanawake wenye kuwafanyia tattoo wengine na wenye kufanyiwa, na wenye kazi ya kuchonga nyusi na wenye kuchongwa, na wenye kupasua mwanya wa meno ili waonekane wazuri, hao ni wenye kubadili uumbaji wa Allaah”.  [Al-Bukhaariy (4886) na Muslim (2125)]

 

Sababu ya kuharamishwa mambo haya kwa mujibu wa Hadiyth hii ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam), ni kuwa yote ni ubadilishaji wa uumbaji wa Allaah, na kwa hivyo ni haramu kuyafanya.

 

Na hakuna shaka yoyote kwamba ubadilishaji wa uumbaji wa Allaah ulio haramu zaidi, ni kubadili jinsia ya mtu kutoka mwanamume kwenda mwanamke au kinyume chake.  Na hii inakuwa kwa yule ambaye Allaah Amemuumba mwanaume kamili, kisha akataka mwenyewe awe mwanamke na kinyume chake.  Ama yule ambaye ameumbwa akiwa na viungo vya kiume na kike (khuntha), huyu ni halali afanyiwe upasuaji wa kumweka katika jinsia iliyoelemea zaidi kwake.  Upasuaji huu ni halali kwa kuwa hauingii kwenye duara la kubadili uumbaji wa Allaah, bali ni kurekebisha tatizo au kasoro.

 

Ama operesheni za kubadili jinsia kwa mtu ambaye ni mwanaume kamili ili awe mwanamke, au awe jinsia ya tatu kama inavyofanyika kwenye baadhi ya nchi hivi sasa ili kuunda jinsia isiyobeba ujauzito ili iweze kutumika kwa starehe tu, jambo hili ni dhambi chafu mno na uchafuzi mbaya sana katika ardhi.  Huu ni uhalifu uliopandana, kwa kuwa kwanza ni ubadilishaji wa uumbaji wa Allaah ambao ndio ubadilishaji mkubwa zaidi katika mwili wa mwanadamu kuliko ubadilishaji mwingine wowote. Na pili, ni ubadilishaji wenye lengo la kuharibu jamii na kueneza machafu kwa njia mbaya kabisa za kuchukiza.  Ni tendo ovu mno lenye upotevu zaidi kuliko hata hali waliyokuwa nayo kaumu Luwt (‘Alayhis Salaam). 

 

 

 

 

Share