18-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Mavazi Na Mapambo: Pambo Kwa Mwanamke Wa Kiislamu: Hukmu Ya Kuvaa Lensi Za Rangi Kama Pambo Na Fasheni

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ اللِّبَاسِ وَالزِّيْنَةِ 

Kitabu Cha Mavazi Na Mapambo

 

 

الزِّيْنَةُ للمَرْأَةِ المُسْلِمَةِ

Pambo Kwa Mwanamke Wa Kiislamu

 

Alhidaaya.com

 

 

18-Hukmu Ya Kuvaa Lensi Za Rangi Kama Pambo Na Fasheni:

 

Sheikh Swaaleh bin Fawazaan aliulizwa hukmu ya kuvaa lensi za rangi kwa ajili ya kujipamba na kwenda na fasheni bila kusahau bei yake ya juu mno, naye akajibu akisema:

 

“Kuvaa lensi kutokana na dharura hakuna ubaya.  Na kama hakuna dharura, basi kuacha inakuwa ni bora zaidi na hususan kama bei yake itakuwa ghali ili kujiepusha na israfu iliyoharamishwa.  Mbali na hivyo, inakuwa ni udanganyifu, kwa kuwa inalionyesha jicho kinyume na uhalisia wake ulivyo.

 

Ama Sheikh Ibn ‘Uthaymiyn, yeye alisema kuhusiana na lensi za kugandisha na jicho kwamba ni lazima kumshauri daktari kujua kama zina madhara kwa jicho au la.  Kama zitakuwa na madhara, basi ni haramu kuzitumia, na madhara yoyote yanayoweza kuupata mwili, ni lazima kuyaepuka kutokana na Neno Lake Ta’aalaa:

 

"وَلَا تَقْتُلُوا أَنفُسَكُمْ ۚ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ بِكُمْ رَحِيمًا "

 

“Wala msijiue.  Hakika Allaah Ni Mwenye Kuwarehemuni”[An-Nisaa: 29]

 

Ama kama madaktari watasema kwamba hazina athari yoyote mbaya wala madhara, hapa itaangaliwa tena, je lensi hizi zinayafanya macho ya mwanamke kuwa kama ya wanyama mfano wa ya kondoo au ya sungura?.  Ikiwa ni hivyo, basi hairuhusiwi, kwa kuwa itakuwa ni kujifananisha na wanyama.  Kujifananisha na wanyama hakujaelezewa ila kwa sifa mbaya ya kukimbiza kama katika Kauli Yake Ta’aalaa:

 

"وَاتْلُ عَلَيْهِمْ نَبَأَ الَّذِي آتَيْنَاهُ آيَاتِنَا فَانسَلَخَ مِنْهَا فَأَتْبَعَهُ الشَّيْطَانُ فَكَانَ مِنَ الْغَاوِينَ    وَلَوْ شِئْنَا لَرَفَعْنَاهُ بِهَا وَلَـٰكِنَّهُ أَخْلَدَ إِلَى الْأَرْضِ وَاتَّبَعَ هَوَاهُ ۚ فَمَثَلُهُ كَمَثَلِ الْكَلْبِ إِن تَحْمِلْ عَلَيْهِ يَلْهَثْ أَوْ تَتْرُكْهُ يَلْهَث"

 

“Na wasomee (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) khabari za yule Tuliyempa Aayaat (ishara, dalili) Zetu, akajivua nazo na shaytwaan akamfuata, na akawa miongoni mwa waliopotoka  ●  Na lau Tungelitaka Tungelimnyanyua kwazo (hizo Aayaat), lakini aligandamana na dunia na akafuata hawaa zake. Basi mfano wake ni kama mfano wa mbwa, ukimhujumu ananing’iniza ulimi nje na kuhema, na ukimwacha pia ananing’iniza ulimi nje na kuhema”.  [Al-A’araaf: 175, 176]

 

Pia Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliposema:

 

"لَيْسَ لَنَا مَثَلُ السَّوْءِ، الْعَائِدُ فِي هِبَتِهِ كَالْكَلْبِ يَعُودُ فِي قَيْئِهِ"

 

“Haitakikani kwetu (sisi Waislamu) kuwa mfano wa sifa mbovu.  Mwenye kurejelea zawadi aliyotoa ni kama mbwa anayerejea kula matapishi yake”.  [Al-Bukhaariy (2589) na Muslim (1622)]

 

Na pia:

 

"مَنْ تَكَلَّمَ يَوْمَ الْجُمُعَةِ وَالْإِمَامُ يَخْطُبُ فَهُوَ كَمَثَلِ الْحِمَارِ يَحْمِلُ أَسْفَارًا" 

 

“Anayezungumza Siku ya Ijumaa na imamu anakhutubu, basi ni kama punda anayebeba vitabu”.  [Ahmad katika Al-Musnad kwa Sanad Dhwa’iyf.  Angalia kwenye Al-Mishkaat nambari (1397)]

 

Hivyo basi, ikiwa lensi hizi zitalifanya jicho kuwa kama la mnyama, basi kuzivaa ni haramu.  Ama ikiwa hazibadilishi umbo la jicho bali zinabadili  rangi yake tu kutoka weusi uliokoza kuja weusi uliofifia na mfano wake, basi hakuna ubaya kuzitumia, kwa kuwa hali hii haizingatiwi kuwa ni ubadilishaji wa uumbaji wa Allaah, kwa sababu si hali ya kudumu muda mrefu kama ilivyo tojo.  Zinakuwa ni kama miwani ambayo wakati wowote akitaka mtu huivua, ingawa tofauti ya viwili hivi ni kuwa miwani haigusani na jicho lakini lensi zinaligusa jicho moja kwa moja. 

 

Alaa kulli hali, ikiwa mwanamke ataachana nazo, itakuwa ni vizuri na salama zaidi kwa macho yake. 

 

 

 

Share