Siwezi Kulipa Mahari Niliyotakiwa Nitoe Nifanyeje?


 

SWALI:

Tafadhali nielezeeni utaratibu wa Nikaah namna inavyofanywa, yaani maneno gani yanasemwa katika khutbatu nikaah pamwe na tafsiriye kwa kiswahili. Mahari hulipwa lini na nifanye nini kama siyawezi mahari aliyotaja harusa. maasalam


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa swali kuhusu suala moja zito la kijamii. Hakika ni kuwa kila ‘Ibaadah ina masharti na utaratibu wake. Nikaah nayo pia ina hayo, hivyo ni juu ya mwenye kutaka kuoa au kuolewa kufuata utaratibu huo la sivyo kutakuwa na mashaka na taabu katika shughuli hiyo nzima. Katika jambo la muhimu kabisa ni kuchagua mume au mke. Tunatakiwa kufuata muongozo wa Dini katika kutekeleza hilo lau sivyo tutakuwa na shida katika maisha ya kindoa.

Baada ya uchaguzi wa mchumba inatakiwa mwanamume apeleke posa kwa wazazi wa msichana. Wazazi wanapopata posa wanafaa wamuite msichana wao na wamuulize kama atapendelea kuolewa na mvulana huyo. Mbali na hilo wazazi wanafaa wafanye juhudi kumchunguza na kumjua mvulana na tabia alizo nazo kama ni za Kiislamu. Hivyo hivyo, kabla ya kupeleka posa wazazi wa msichana wanatakiwa wafanye uchunguzi kumhusu mvulana na maadili yake.

Msichana anapokubali posa hiyo basi yanafuata ni mambo mengine kama:

 

  1. Kusikilizana na kuridhiana mahari atakayotoa mume kumpatia mkewe.
  2. Apatikane walii kwa upande wa msichana akiwa baba, au babu au kaka na mfano wao.
  3. Wakati wa Nikaah kupatikane mashahidi 2 waadilifu.
  4. Kusomwa kwa Khutbah na Walii au mtu atakayechaguliwa na Walii.
Khutbah za kusomwa ni nyingi na mtu anaweza kuchagua anayotaka. Mojawapo ni: “Innal Hamda Lillahi nahmaduhu wa nasta‘inuhu wa nastaghfiruhu wa natuubu ilayhi wa na‘udhu Billahi min shuruuri anfusina wa sayiaati a‘maalina man yahdihi Llaahu fala mudhilla lahu wa man yudhlil falaa haadiya lahu wa ashhadu an laa ilaaha illa Llaahu wa ashhadu anna Muhammadan ‘abduhu wa Rasuuluhu. (Sifa zote njema anastahiki Allaah, tunamuhimidi, kutaka msaada, kuomba msamaha na kutaka msaada Kwake. Tunajilinda kwa Allaah na shari ya nafsi zetu na amali zetu mbaya. Anayeongozwa na Allaah hakuna wa kumpoteza na mwenye kupotezwa hakuna wa kumuongoza. Nakiri kuwa Allaah pekee ndie wa kuabudiwa na kuwa Muhammad ni mja na mjumbe Wake). Baada ya hiyo Khutbah ya ufunguzi kama alivyokuwa akisoma Mtume (Swalla Allaahu ‘alayki wa aalihi wa sallam) kwenye vikao vyake, atasoma Aayah za Surah zifuatazo: Al-‘Imraan: 102; An-Nisaa: 1; na Al-Ahzaab: 70-71. Mwenye kutoa Khutbah anaweza kusoma Aayah na Hadiyth nyingine zinazonasibiana na shughuli hiyo.

Baada ya Khutbah ni kupata Ijaab (ulizo la kama amekubali kumuoa mke) kutoka kwa Walii wa mke na Qabuul (itikio la kukubali) kutoka kwa bwana harusi.

Mahari hulipwa kama mlivyosikilizana na bibi harusi, na ni haki ya mwanamke mwenyewe na wala sio ya mzazi. Mahari hayo yanaweza kulipwa kabla ya harusi au baada yake kutegemea masikilizano yenu. Baada ya kukubaliana hakuna tena kusema kuwa siwezi. Inakuwa ni wajibu kwako kumlipa hata kama ni kidogo kidogo mpaka umalize deni hilo au mke mwenyewe akusamehe bila kumlazimisha.

Ni muhimu wazazi wa mke watambue kwamba haipasi kutaka mahari makubwa kwani ni kinyume na mafunzo ya Mtume Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam.

Linalotakiwa ni kabla ya kuingia katika Nikaah msikilizane kuhusu mahari mpaka mkubaliane. Baada ya kukubaliana katika hilo usiwe ni mwenye kutoa udhuru mwengine au kufanya hiyana. Kufanya hilo itakuwa ni dhambi kubwa upande wako.

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share