Yanayopasa Na Yasiyopasa Kutendeka Katika Ndoa

Yanayopasa Na Yasiyopasa Kutendeka Katika Ndoa

 

www.alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Assalam alaykum warahmatullah taala wabarakatuh.

Ombi langu ni kunijulisha yapaswayo kutendeka ktk kukamilika kwa ndoa ya kiislamu, nikiwa na maana ya kuwa bi harusi afanye nini na bwana harusi afanye nini maana nimepata kusikia mambo kama ya kuwa baada ya kufungwa ndoa na kukamilika kwa hotba ya ndoa, bwana harusi yampasa ampe mkono mkewe na kumshika kichwa huku akisoma dua ,na bibie pia yampasa kusali rakaaa mbili za sunna sasa sijui kwa yakini ,kama ni sunna ni ipi na yote kwa jumla Nashukuru na ninatarajia jibu hivi karibuni

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Tunashukuru sana kwa swali lako na ari yako kubwa ya kutaka kujua mas-alah mbalimbali ya dini yako katika mfumo SAHIHI wa kishariy'ah. Allaah Akuzidishie hilo na mengineyo.

 

Ama katika suala la ndoa kuna mambo mengi ya Sunnah ya kuyaeleza ambayo hatutaweza hapa kuyataja yote, ila kuna yanayofanywa yasiyo sahihi na yale sahihi yanaachwa!

 

Kwa kifupi tu tutataja yanayofaa na yasiyofaa.

 

Tutaanza na yasiyofaa kabla na baada ya ndoa:

 

MAMBO YASIYOTAKIKANA KUFANYWA

 

1. Maingiliano ya ndani baada ya watu kuposana, kama vile; kutoka pamoja kutembea, kuwa faragha muda mwingi na tabia hii husababisha watu kuzoeana hadi ikafika pahala panapoitwa 'kujaribiana'! Matokeo ndoa nyingi huharibika kabla hazijafungwa.

2. Ngoma maalum ichezwayo kumfundisha bibi harusi jinsi ya kufanya matendo ya chumbani na mumewe au imezoeleka kuitwa unyago. Matendo yanayofanywa kwenye ngoma hizo ni ya aibu na machafu kupita mpaka, na ajabu wapigaji ngoma ni wanaume wanaoshuhudia mambo yote hayo.

3. Baada ya kuoana kuna sherehe zisizo za Kiislam kama; 

a)   Kuvishana pete

b)  Kutolewa bibi harusi mbele ya hadhara na kuanikwa  mbele ya watu wamuone au 'waone uzuri' na mapambo yake.

c) Kulishana keki hadharani.

d) Kupigwa miziki na watu kucheza, iwe ni 'party' au taarab au aina zozote za mziki.

e) Kuchanganyikana wanaume na wanawake katika kushereheka kwa pamoja.

f) Kupigwa mapicha na kuchukuliwa video wanawake na wanaochukuwa ni wanaume.

g) Kushereheka kwa mtindo wa kikafiri kama kulishana keki, kupigana busu hadharani, kuvishana pete n.k kama tulivyotaja nyuma.

h) Pia kuna tabia ya kumzuia mume asiingie kwenye chumba cha bibi harusi hadi atoe pesa! Na akiruhusiwa kuingia watu wanamfuata ndani na Sheikh anamfundisha jinsi ya kumsomea mkewe dua n.k

i) Baadhi ya mila hadi sasa wana tabia ya kuweka shuka jeupe wakati wa tendo la ndoa ili matokeo yadhihirike kama mke ni bikra au la! Vitendo vya kufedheheshana na aibu.

j) Kuna tabia ya mama mtu mzima kuwa karibu na tendo la ndoa ili kuwasaidia kuwapa mafundisho wanandoa kufanikiwa kuondosha ubikra kama mke ni bikra.

k) Kutoa siri za tendo la ndoa au mambo yafanyikayo kitandani kwa watu wengine. Mke au mume anaenda kuelezea mambo aliyoyafanya na mwenzake au jinsi mwenzake alivyo katika suala lile.

 

 

MAMBO YANAYOTAKIKANA KUFANYWA NA YANAYORUHUSIWA

 

1. Kabla ya ndoa:

a) Kumuona bi/bwana harusi, kumtazama na kuridhika naye.

b) Mahari mepesi yasiyomkalifu mposaji.

c) Kuharakisha ndoa, si kuposa kisha mnaanza kuchunguzana na kusomana 'tabia' au kujijenga kimaisha n.k.

 

2. Baada ya ndoa:

a) Kufanya karamu na kualika watu, na iwe ni watu wa kila tabaka (isiwe matajiri, kabila, au watu maarufu tu)

b) Wanawake kuimba na kupiga dufu (kavu lisilo na chekecheke) wala kusiwe na ala za mziki. Nyimbo ziwe ni za maadili, kumsifu bibi harusi na shughuli nzima kwa ujumla. Zisiwe za mafumbo, matusi, malumbano wala mipasho.

c) Kufanyiana wema kuanzia usiku ule wa ndoa kama kunyweshana kinywaji kama maziwa, alivyofanya Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  kwa mama wa Waumini 'Aaishah رضي الله عنها  

d) Mume kuweka mkono wake juu ya sehemu ya mbele ya kichwa cha mke na kuomba baraka kwa Allah.  

e) Kuswali mume na mke pamoja rakaa mbili na kuomba du'aa Allaah Awape kheri baina yao.

f) Wakati wa tendo la ndoa, mume aombe du'aa wakati anaanza kumuingilia mkewe, du'aa ya kumwepusha Shaytwaan nao na kile watakachoruzukiwa kwa tendo hilo (mtoto).

g) Ni vizuri kumtumia mke mjumbe (yaani kufanya mapenzi (romance) kabla ya tendo) na si kuingiliana kama wanyama.

h) Inaruhusiwa mitindo yoyote ilimradi kufanyike tendo sehemu inayopaswa, penye kumea na kutoa mavuno (uzazi), kusiwe ni sehemu ya nyuma (liwati) ambayo ni haramu.

i) Kuchukua Wudhuu kila baada ya tendo moja la ndoa, yaani kabla hujarudia mara ya pili ni vizuri kuchukua Wudhuu kama wa Swalah kwani unarejesha uchangamfu na usafi na kama kunawezekana kuoga basi ni bora zaidi.

j) Kuoga mume na mke pamoja au kuogeshana. (haya ni katika yanayoruhusiwa) kama ilivyothibiti kwa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  na mama wa Waumini 'Aaishah رضي الله عنها .  

k) Kutawadha tena au kuoga baada ya tendo zima na kabla ya kulala ikiwezekana na ni vizuri zaidi ingawa si lazima.

j) Ni vizuri asubuhi yake mume kwenda kwa jamaa waliomtembelea au kumsaidia kuwashukuru na kuwaombea du'aa, na wao vilevile ni vizuri kwao kufanya hivyo kwa mume. Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alikuwa akifanya asubuhi baada ya ndoa yake chakula na kuwalisha watu kisha akienda kwa wake zake wengine kuwasalimia na kuwaombea du'aa na wao wakimjibu kwa uzuri zaidi.

 

Du'aa zote hizo tulizozitaja zinapatika ALHIDAAYA katika kiungo cha 'Du'aa na Adhkaar' www.alhidaaya.com/sw/duaa.

 

Haya ni baadhi ya mengi yanayofaa na yasiyofaa kufanywa wakati wa ndoa.

Allaah Atujaalie ni wenye kuyafuata katika ndoa zetu na kuyaacha yasiyofaa.

 

Na Allaah Anajua zaidi.

 

Share