61-Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti: Kuzuru makaburi wakati wa matukio maalum

 
Kuzuru makaburi wakati wa matukio maalum:
 
Watu wengi wamefanya mazoea ya kuzuru makaburi nyakati maalum; kwa mfano wakati wa iddi mbili, katika mwezi wa Rajab, katika siku za Alhamisi na mfano wa hayo katika masiku na miezi ambayo watu wamefanya kuwa ni za matukio maalum. Katika masiku hayo watu ambao huenda kufanya ziara makaburini huandaa chakula maalum na kugawa kwa watu wa makaburi na wengine huchukua hata radio, t.v na hupitisha masiku ya sikukuu ya iddi makaburini; wakiimba, kucheza na kufanya laghwi na lahwi na wakasahau kabisa hali za watu wa makaburi na kuwaombea dua kwa Mwenyezi Mungu kinyume chake wanawaudhi na wanawabughudhi watu wa makaburi.
Hii ni bid’a na ni katika mambo yenye kuzushwa. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) hakufanya wala hakuamrisha lakini kinyume chake ameyakataza, haiwanufaishi waliokuwa hai au waliokuwa wafu. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) aliwahi kusema, “Msifanye kaburi langu kuwa ni Iddi.” Kwa maana msizowee kulizuru katika masiku maalum. Ikiwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) analisemea kaburi lake sembuse makaburi ya watu wengine ndio haswa ya mwanzo kuhadharishwa.
Kwa mja ambae anataka kheri kwa ajili ya nafsi yake basi na ajitahidi kuchunga matumizi ya wakati wake asije kutumia katika lahwi na laghwi na mchezo na maasi na mambo yote yaliyo munkari hata atakapomjia malaika wa mauti anakuwa ameshafanya maandalizi wala hajutii wakati wake uliopita, yaliyopita hayarudi, mtu ajitahidi kila analolifanya ahakikishe kuwa linaingia katika mizani ya mambo yake ya kheri na kupunguza mambo ya shari, jitahidi ufanye litakalokufaa kwa siku yako ya mwisho.
Allahumma hdi Qawmi fainahum laa Yaalamun
Ee, Mwenyezi Mungu waongoze watu wangu kwani wao ni watu wasiojua.
Na utusamehe sisi na maiti wetu Ee, Mola wa walimwengu.
Natoshelezwa na haya machache na kumswalia Mtume wetu Muhammad na Aali zake na sahaba zake.
 
 
Share